Jumatatu 25 Disemba, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 6 Mfunguo Saba Rabiuthani 1439 Hijria sawa na tarehe 25 Disemba 2017.
Siku kama ya leo miaka 2018 iliyopita, Nabii Issa Masih (AS) alizaliwa katika mji wa Bait Laham (Bethlehem) huko Palestina. Nabii Issa Masih alipewa uwezo na Mwenyezi Mungu wa kufanya miujiza mingi. Issa Masih AS alianza kuzungumza akiwa mdogo na kujibashiria unabii. Mwenyezi Mungu anaashiria tukio la kuzaliwa kwa Nabii Issa katika Qur'ani Tukufu katika Suratu Aal Imran aya ya 45 kwa kusema: Kumbukeni waliposema Malaika: "Ewe Mariam! Mwenyezi Mungu anakubashiria mwana kwa neno litokalo kwake; jina lake ni Masih, Issa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera na miongoni mwa waliokurubishwa." Inafaa kuashiria hapa kwamba, tarehe 25 Disemba kila mwaka inajulikana kote duniani hasa kwa Wakristo kuwa ni Sikukuu ya Krismasi. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa wafuasi wa kweli wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu.

Siku kama ya leo miaka 1314 iliyopita, alifariki dunia Hisham Bin Abdul-Malik, kiongozi wa 10 katika silsila ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuwa madarakani kwa karibu kipindi cha miaka 20. Hisham aliyekuwa dikteta alizaliwa mwaka 72 Hijiria na kushika uongozi wa Waislamu mwaka 105 Hijiria. Aidha Hisham anafahamika kwa kuwa bahili, katili na dhalimu, ambaye aliwakandamiza Waislamu wa zama zake hususan wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume (saw) yaani Mashia. Mtawala huyo wa Bani Umayyah aliishi katika kipindi cha Imam Muhammad Baqir (as) mmoja wa wajukuu watukufu wa Nabii wa Uislamu ambapo alimfanyia maudhi mengi mtukufu huyo na baadaye kutoa amri ya kuuawa kwake. Mbali na hapo Hisham alifanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya harakati za Zaid bin Ali, mjukuu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuliwa Zaid, mtawala huyo dhalimu alitoa amri ya kuchomwa moto mwili wa mtukufu huyo. Licha kwamba katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah, Uislamu ulienea maeneo ya mashariki na magharibi mwa dunia, lakini kulishuhudiwa harakati kadhaa za Kiislamu za kupinga dhulma, kutokana na kushadidi dhulma na ukandamizaji wa Hisham bin Abdul-malik, harakati ambazo zilipelekea kudhoofika kwa dola hilo la Bani Umayyah.

Siku kama ya leo miaka 623 iliyopita alifariki dunia Mir Sayyid Sharif Gorgani, mtaalamu wa fasihi wa Iran huko Shiraz. Gorgani alizaliwa mwaka 740 Hijiria karibu na mji wa Gorgani ya leo, kaskazini mwa nchi hii. Mir Sayyid Sharif Gorgani alihesabika kuwa msomi mkubwa katika zama hizo hususan katika uga wa elimu ya fasihi. Ameacha athari mbalimbali mojawapo ikiwa ni kitabu kiitwacho "Risaalatul-Kubra fil-Mantiq" na "Sharhu Mawaaqif Qadhi Adhdud-Diin Iji."
Siku kama ya leo miaka 587 iliyopita, sawa na tarehe sita Rabiuth-Thani mwaka 852 Hijiria, alizaliwa Ibn Iyas, mwanahistoria mashuhuri wa nchini Misri. Ebn e-Eyas alinakili habari mbalimbali za kihistoria kwa mfumo wa nathari nyepesi, mfumo ambao ulikuwa hautumiwi na wanahistoria wengine. Mfumo huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwenye fani ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari muhimu ya kihistoria za Ibn Iyas ni pamoja na kitabu cha "Badaaiuz-Zuhuur fii Waqaai' Duhuur" ambacho kinaelezea historia ya Misri tangu karne za nyuma hadi kipindi chake. Vilevile alifafanua maisha ya watawala wa Misri, ujenzi na uimarishwaji wake na mambo mbalimbali yaliyowahi kuikumba nchi hiyo katika karne za nyuma.

Miaka 374 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Isaac Newton, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika na alitambuliwa kama mwanasayansi mkubwa aliyepata umashuhuri. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy. Ugunduzi wa Isaac Newton ulikuwa msingi mkuu wa ugunduzi wa wasomi wengine kuhusu kanuni kuu za hisabati na uhandisi.
Miaka 352 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 25 Disemba 1665, Ufaransa ilianzisha French East India Company katika kipindi cha utawala wa Mfalme Louis II ili kushindana kisiasa, kiuchumi na kikoloni na serikali ya Uingereza huko India. Uingereza ilikuwa imeasisi British East India Company miaka 66 kabla ya hapo. Vilitokea vita kadhaa baina ya tawala hizo mbili za kikoloni kwa shabaha ya kuikoloni ardhi ya India.

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Disemba 1979, viongozi watatu wa ngazi za juu wa Palestina waliuawa kigaidi na Shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Viongozi hao walikuwa Ali Hassan Salamah, afisa wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliyeuawa Beirut baada ya kutegwa bomu ndani ya gari lake, Samir Touqan mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya PLO huko Cyprus na Ali Nasser Yassin, shakhsia mwingine wa Palestina aliyekuwa mwakilishi wa PLO nchini Kuwait. Jinai hiyo ilidhihirisha tena jinsi utawala katili wa Israel unavyotumia ugaidi katika maeneo mbalimbali dunia kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu.