Dec 30, 2017 02:45 UTC
  • Jumamosi, 30 Desemba, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Saba Rabiuthani 1439 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe 30 Desemba 2017 Miladia.

 

Siku kama ya leo miaka 1219 iliyopita yaani tarehe 11 Mfunguo Saba Rabiuthani 220 Hijria, alifariki dunia Abu Ali Khayyat, mnajimu na mtaalamu wa hisabati wa Kiislamu. Abu Ali ni mmoja wa shakhsia aliyekuwa na nafasi kubwa wakati wake, huku jina lake likiwekwa mstari wa mbele katika kitabu cha majina ya wasomi wakubwa na mashuhuri wa dunia. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Mawaalid'. Vitabu vingi vya Abu Ali Khayyat vimetarjumiwa kwa lugha ya Kilatini. ***

 

Tarehe 11 Mfuo Saba Rabiu Thani 608 Hijria yaani miaka 831 iliyopita, alizawa mjini Mosul, moja ya miji mashuhuri ya Iraq, Ibn Khallekan (Ebn-e Xallakan), kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Akiwa kijana alisoma elimu za awali katika mji alikozaliwa na kisha kufanya safari mbalimbali na kukutana na kupata elimu kwa wataalamu wa fiqhi na wanahistoria wakubwa wa Kiislamu. Kwa muda mrefu Ibn Khallekan alikuwa kadhi mjini Damascus, Syria na akiwa mtaalamu katika elimu za historia, fasihi ya Kiarabu na mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwezi wa Rajab mwaka 681 Hijiria na kuzikwa chini ya mlima Qasioun ulioko Damascus ambako pia wamezikwa wasomi wengi. Miongoni mwa vitabu muhimu vya Ibn Khallekan ni Wafahyatul A'yaan. ***

Ibn Khallekan (Ebn-e Xallakan),

 

Miaka 70 iliyopita, magaidi wa mashirika mawili ya kijasusi ya Israel walishambulia kitongoji cha Balad al-Sheikh huko Palestina na kuchoma moto nyumba za kitongoji hicho. Moto huo uliwateketeza na kuwaua shahidi Wapalestina 60. Siku hiyo hiyo kundi jingine la kigaidi la Israel lililojulikana kwa jina la Irgun lilidondosha mabomu katikati ya kundi la Wapalestina na kuwaua shahidi 17 kati yao. Mashambulio hayo yaliyoshadidi mwishoni mwa mwaka 1947 na mwanzoni mwa 1948, yalikuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kuwafukuza kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao ili kuasisiwa utawala pandikizi na ghasibu wa Israel katika ardhi hizo. ***

Jinai za utawala ghasibu wa Israel

 

Katika siku kama leo miaka 70 iliyopita, uongozi wa kifalme wa Romania uling'olewa madarakani kufuatia kujiuzulu mfalme wa nchi hiyo na badala yake kukaundwa mfumo wa jamhuri nchini humo. Hadi kufikia mwaka 1862, Romania ilijiamualia utawala wa ndani chini ya utawala wa Othmania na kujipatia uhuru wake taratibu hadi kufikia mwaka 1877. Romania ni moja ya nchi masikini za Ulaya ya Mashariki huku siasa za Kikomonisti zinazotawala, zikishindwa kumaliza matatizo ya nchi hiyo. ***

Bendera ya Romania

Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, baada ya serikali ya kijeshi chini ya uongozi wa Jenerali Azhari hapa nchini Iran kushindwa kukandamiza vuguvugu la mapinduzi la wananchi Waislamu, Muhammad Reza Shah mfalme wa mwisho wa Iran, alimteuwa Shapour Bakhtiar kuwa Waziri Mkuu. Reza Shah na Marekani walikuwa na matumaini kwamba, Bakhtiar kwa kutumia nara na kaulimbiu zenye mielekeo ya utaifa na siasa ambazo kidhahiri zilikuwa zikionekana kama za kutaka mabadiliko, angeweza kuzuia harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran. Hata hivyo, wananchi wanamapinduzi wa Iran walitambua hila na hadaa hiyo, hivyo walimpinga vikali Bakhtiar na kumuita kuwa kibaraka wa mabeberu. Imam Khomeini (MA) alitoa taarifa na kutangaza kuwa, serikali ya Bakhtiar haikuwa halali na kuwataka wananchi wapambane na serikali hiyo. ***

Shapour Bakhtiar

 

Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, yaani tarehe 30 Disemba mwaka 2006, Saddam Hussein mtawala mwagaji damu na dikteta wa zamani wa Iraq, alinyongwa baada ya kutolewa hukumu ya kifo dhidi yake. Saddam alizaliwa mwaka 1937 karibu na mji wa Tikrit uliopo umbali wa kilomita 140 kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kujiunga na chama cha Baath akiwa na umri wa miaka 20. Dikteta huyo alifanikiwa kuwa naibu wa Ahmad Hassan al-Bakr kufuatia mapinduzi yaliyojiri ndani ya chama hicho cha Baath mnamo mwaka 1968. Mwaka 1979 Saddam alikuwa Rais wa Iraq na muda mfupi baada ya kushika madaraka alianzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisaidiwa na madola ya Magharibi na kufanya mauaji na maafa mengi. Kwa msaada wa madola hayo, Saddam alipata silaha za kemikali na kuzitumia dhidi ya mataifa ya Iran na Iraq. Saddam aliendelea kufanya mauaji ya kila aina dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na nchi jirani, chini ya himaya na uungaji mkono wa madola ya Magaharibi ikiwemo Marekani. ***

Saddam Hussein dikta wa zamani wa Iraq

 

Tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Desemba, mamilioni ya wananchi wa Tehran na miji mingine hapa nchini walifanya maandamano kulalamikia machafuko ya barabarani na himaya ya madola ya Magharibi kwa machafuko hayo. Baada ya uchaguzi wa Rais wa Juni 30, wagombea wawili walioshindwa walilalamikia matokeo ya uchaguzi, lakini hawakuwa tayari kufuatilia malalamiko yao kupitia njia za kisheria. Uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa wagombea hao ulipelekea kutokea machafuko mjini Tehran. Licha ya kuwa machafuko na vurugu za mitaani hazikuwa kubwa lakini ziliathiri amani na utulivu wa wananchi na kuibua tamaa ya Wamagharibi ya kubadilisha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini. Maandamano ya mamilioni ya wananchi wa Iran dhidi ya wafanya vujo waliokuwa wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais yalithibitisha kwamba, kinyume na propaganda za maadui, akthari ya wananchi walikuwa wakiyatambua na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo. Kwa hakika siku ya tarehe 9 Dei (30 Disemba 2009) ilikuwa siku ya kudhihirika uadui na uhasama wa wazi na wa nyuma ya pazia wa maadui wa ndani na nje ya nchi, mkabala wa utawala wa Kiislamu hapa nchini, ambapo maadui wa ndani na nje walilenga shabaha Uislamu, itikadi za kidini, maadili, uongozi wa Iran na mengine mengi ya thamani. Siku hii ya tarehe 9 Dei imepewa jina la "Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali". ***

Siku ya Ung'amuzi