Jan 03, 2018 00:29 UTC
  • Jumatano tarehe 3 Januari, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 15 Mfunguo Saba Rabiuthani 1439 Hijria mwafaka na tarehe 3 Januari mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi. Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu." Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu."

Mikhail Gorbachev

Katika siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, inayosadifiana na Januari 3, 1993 kulitiwa saini makubaliano ya Start-2 kati ya Marais wa zamani wa Russia na Marekani, Boris Yeltsin na Bill Clinton. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi hizo mbili zinapaswa kupunguza theluthi mbili za silaha zao za nyuklia. Makubaliano ya Start-1 yenye lengo hilohilo yalitiwa saini mwaka 1987 kati ya Marais Mikhael Gorbachev wa Russia na Ronald Reagan wa Marekani. Hata hivyo badala ya kuanza kuharibu silaha zake za nyuklia, Marekani ilijilimbikizia sialaha zaidi za aina hiyo suala ambalo liliilazimisha pia Russia kusitisha mpango wa kuanza kuharibu silaha zake za atomiki.

Makombora ya nyuklia

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita inayosadifiana na 13 Dey 1358 Hijria Shamsia, kulifanyika kongamano la kwanza la harakati za kupigania uhuru duniani mjini Tehran na kuhudhuriwa na wawakilishi wa harakati hizo. Lengo kuu la kuitishwa kongamano hilo, lilikuwa kuitambulisha harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa walimwengu, sambamba na kuandaa mazingira ya kujenga umoja na mshikamano wa harakati hizo katika kukabiliana na dhuluma na mabeberu duniani.

Na miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo kulifanyika mkutano wa Guadeloupe kati ya viongozi wa serikali za marekani, Uingereza, Ujerumani ya Magharibi na Ufaransa kwa ajili ya kuchunguza masuala kadhaa muhimu ya kimataifa hususan Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Mkutano huo ulifanyika katika kisiwa cha Guadeloupe kilichoko magharibi mwa Bahari ya Atlantic ambacho ni koloni la Ufaransa. Katika mkutano huo uliofanyika siku 40 kabla ya ushindi kamili wa harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran washiriki wote walikiri kwamba, Mfalme wa wakati huo wa Iran Shah Pahlavi ataondolewa madarakani isipokuwa Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani ndiye pekee aliyekwua na matumaini ya kubakia madarakani utawala wa Shah kwa msaada wa jeshi. Haya hivyo mkutano huo wa Guadeloupe haukuwa na mbinu ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya wanancdhi wa iran na iliishia kukiri nguvu kubwa ya mapinduzi hayo na mustakbali wake mwema.

Mkutano wa Guadeloupe