Jan 04, 2018 23:12 UTC
  • Ijumaa tarehe 5 Januari 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 17 Mfunguo Saba Rabiuthani 1439 Hijria sawa na 5 Januari 2018.

Siku kama ya leo miaka 327 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1691, ilichapishwa na kusambazwa noti ya kwanza huko Ulaya. Noti hiyo ilichapishwa na Benki ya Stockholm na kutumiwa kama fedha. Kabla ya kuchapishwa noti hiyo nchini Sweden, miamala ya kibiashara ilikuwa ikifanyika kwa kutumia sarafu za dhahabu zenye pembe nne. Moja kati ya noti za awali kabisa kuchapishwa nchini Sweden, inahifadhiwa kwenye makumbusho ya Benki ya Stockholm.

Noti ya kwanza kuchapishwa barani Ulaya

Miaka 105 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ayatullah Sheikh Muhammad Ali Nakhjavani mmoja wa maulama watajika na wapokezi wakubwa wa hadithi aliaga dunia huko Karbala nchini Iraq. Alikuwa mtu wa Nakhjavan katika Azerbaijan ya leo na alijifunza Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 11 na baada ya hapo akaanza kusoma masomo ya mantiki na elimu nyingine kama fasihi ya lugha ya Kiarabu na kuyapa umuhimu masomo hayo. Hatimaye mwanazuoni huyo alifanikiwa kufikia daraja ya Ijitihad na kuwa Marjaa Taqlidi wa Waislamu. Ayatullah Nakhjavani ameacha athari mbalimbali za vitabu alivyoalifu katika taaluma na mauidhui mbalimbali.

Tarehe 15 Dei miaka 39 iliyopita wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran waligoma kwenda madarasani na kufunga masomo wakionesha upinzani wao dhidi ya safari ya rais wa wakati huo wa Marekani, Jimmy Carter hapa nchini na uungaji mkono wake kwa utawala wa Shah. Wakati huo Carter alikuwa akidai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu na mpinzani wa suala la kuziuzia silaha tawala za kidikteta. Hata hivyo serikali ya Washington ilichukua uamuzi wa kufunga mikataba ya kuuzia silaha nzito utawala wa kidikteta wa Shah na kupuuza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa nchini Iran. Jimmy Cater alifikia kiwango cha kumwita Shah kuwa ni kiongozi anayependwa na wananchi na kwamba Iran ni kisiwa cha amani. Hata hivyo muda mfupi baadaye wananchi walianza harakati za kudai uhuru na kujitawala na miezi 13 baada ya safari ya Carter mjini Tehran Shah aliondolewa madarakani na ikaanzishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Jimmy Carter akwia safarini nchini Iran

Na siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1985, utawala wa Kizayuni wa Israel uliwachukua maelfu ya Mayahudi wa Ethiopia "Mafalasha' kupitia ardhi ya Sudan. Mafalasha hao ambao idadi yao ilikuwa watu 8,000 walipelekwa huko Israel. Nchi za Kiarabu ziliikasirikia Sudan kwa kushirikiana na Israel katika kuwahamisha Mayahudi wa Kiethiopia na kuwapeleka Israel.

Mafalasha wananyanyaswa Israel