Jumamosi, 6 Januari, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 18 Mfunguo Saba Rabiuthani 1439 Hijria sawa na tarehe 6 Januari 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 837 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alizaliwa Abul Qasim Jafar bin Hassan Hilli maarufu kwa lakabu ya Muhaqiq Hilli, mmoja wa wanazuoni wakubwa na faqihi wa Kiislamu, katika mji mashuhuri wa Hillah, nchini Iraq. Muhaqiq Hilli alikuwa msomi aliyekuwa na nafasi ya juu na mtaalamu wa sheria za Kiislamu na alibobea pia katika fasihi na uandishi wa mashairi. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na kupaa daraja za juu za kiroho, alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha Muhaqqiq al-Hilli ni Sharaiul Islam, fii masaailil-Halal wal-Haraam'. Mwanazuoni huyo pia ameandika vitabu vya "Al Nafi', Maarij na al Tanbih". Muhaqqiq al-Hilli alifariki dunia mwaka 676 Hijria akiwa na umri wa miaka 74. ***
Katika siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, yaani sawa na tarehe 6 Januari mwaka 1861 kuliasisiwa nchi ya Romania. Mpango wa kupatikana nchi hii msingi wake ulikuwa kutiwa saini kwa muungano wa miji miwili midogo iliyojulikana kwa jina la Moldavia na Wallachia, makubaliano yaliyofikiwa tarehe 13 Disemba mwaka 1859. Baada ya miaka miwili majimbo na miji mingine ya jirani ikajiunga na muungano huo. Kwa utaratibu huu ikapatikana nchi iliyokuja kutambulika kwa jina la Romania.***
Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Theodore Roosevelt Rais wa zamani wa Marekani. Theodore Roosevelt Rais wa 26 wa Marekani alizaliwa Oktoba 27 mwaka 1857. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana. Alikuwa mwanachama wa chama cha Republican. Alikuwa Makamu wa Rais na baada ya kuuawa William McKinley aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Theodore Roosevelt akawa Rais muda wa nchi hiyo. Mwaka 1901 alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani. Mwanzoni mwa utawala wake, Theodore Roosevelt aliimarisha uwepo wa vikosi vya Marekani nchini Cuba iliyokuwa ikikaliwa kwa mabavu na Washington na akaitangaza rasmi nchi hiyo kuwa chini ya mamlaka na himaya ya Marekani. ***
Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, Ayatullah Mirza Ali Shirazi aliaga dunia huko Najaf moja kati ya miji ya Iraq akiwa na miaka 68. Ayatullah Shirazi alijifunza elimu ya fiqhi na masomo mengine ya Kiislamu kutoka kwa maustadhi wakubwa kama vile Ayatullah Fisharki Isfahani na Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi na kufikia daraja ya Ijtihad akiwa na miaka 22. Mbali na kubobea katika elimu za fiqhi na usul, Ayatullah Mirza Ali Shirazi alikuwa mahiri pia katika elimu ya kalam au itikadi, tiba, historia na fasihi. Aidha alikuwa pia Marja Taqlidi wa Waislamu kwa kipindi fulani. ***
Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yooshij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yooshij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh". ***

Na katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, serikali ya kijeshi ya Gholam Reza Azhari ilianguka nchini Iran na nafasi yake ikachukuliwa na serikali ya Shapour Bakhtiar. Baada ya Shapour Bakhtiar kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa utawala wa Kipahlavi, katika siku kama ya leo alitangaza baraza lake na mawaziri na hivyo akawa amechukua rasmi hatamu za uongozi. Baraza la Mawaziri la Shapour Bakhtiar lilianza kazi katika hali ambayo, harakati ya Kiislamu ilikuwa imeshika kasi katika kila kona ya Iran na hakukuwa na nguvu yoyote ya kuweza kukabiliana na harakati hiyo ya wananchi. Shapour Bakhtiar akiwa Waziri Mkuu wa mwisho katika kipindi cha utawala wa Kifalme wa Kipahlavi hapa nchini alijaribu kuwapatia wananchi baadhi ya mambo na upendeleo ili kwa njia hiyo aweze kupunguza malalamiko ya wananchi. Hata hivyo, ujumbe wa Imam Khomeini kuhusiana na serikali ya Bakhtiar ulisambaratisha njama za utawala wa Kifalme zilizokuwa na lengo la kusambaratisha harakati ya mapinduzi ya wananchi. Katika ujumbe wake huo, Imam Khomeini MA aliitaja serikali hiyo kwamba, si halali. ***