Jumatatu tarehe 8 Januari, 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 20 Rabiuthani 1439 sawa na Januari 8, 2018.
Siku kama ya leo miaka 376 iliyopita alifariki dunia msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia Galileo Galilei akiwa na umri wa miaka 78. Alizaliwa katika mji wa Pisa na alisoma fasihi hadi alipofikisha umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Mwislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, Kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa ni kafiri na akahukumiwa. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Siku kama ya leo miaka 305 iliyopita, alizawa Haji Lutfi Ali Bik Azar Bigdeli, malenga na fasihi wa Iran huko mjini Isfahan, moja ya miji mashuhuri ya nchi hii. Haji Bik Azar Bigdeli aliishi kipindi fulani mjini Qum na Shiraz na hatimaye akaweka makazi yake eneo alikozaliwa ya Isfahan, baada ya kutoka safari yake ya Hija. Katika kipindi hicho alijikita katika shughuli ya kufundisha vijana wa mji huo na hakuwa tayari kuacha shughuli hiyo licha ya kuwepo ukame mkali na machafuko yaliyotokana na kujiri kwa vita nchini Iran. Miongoni mwa athari mashuhuri za msomi huyo ni pamoja na vitabu vya mashairi alivyovipa jina la 'Atashkadeh Azar' ambavyo vimekusanya mashairi ya wakati huo na ya kabla yake.

Na Tarehe 18 Dei mwaka 1385 Hijria Shamsia yaani miaka 11 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mhakiki na mwanahistoria wa Iran Hujjatul Islam Ali Dawwani. Msomi huyu alizaliwa mwaka 1308 Hijria Shamsia karibu na mji wa Kazerun ulioko kusini mwa Iran. Alielekea Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kupata elimu za Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na kurejea nchini miaka mitano baadaye. Ali Dawwani aliendelea kutafuta elimu katika mji mtakatifu wa Qum na kusoma kwa wanazuoni wakubwa kama Imam Ruhullah Khomeini na Ayatullah Borujerdi hadi alipopata daraja ya ijtihadi. Alibobea sana katika elimu ya historia na ameandika vitabu vingi katika uwanja huo. Miongoni mwa vitabu vyake ni "Fakhari za Uislamu", "Mbora wa Wanawake Duniani" na "Harakati ya Wanazuoni wa Iran".