Jan 10, 2018 01:04 UTC
  • Jumatano, Januari 10, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 22 Mfunguo Saba Rabiuthani 1439 Hijria sawa na Januari 10, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 365 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Januari 1653 lilitolewa kwa mara ya kwanza gazeti linaloandika habari za ulimwengu lililopewa jina la ‘Gazzetta' nchini Italia. Gazeti hilo lilipewa jina hilo kwa sababu bei yake ilikuwa ni sawa na Gazetta moja iliyokuwa sarafu ya Venice. Baada ya hapo jina hilo likawa limesambaa katika nchi nyingine ambazo zilianza kusambaza magazeti. 

Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita inayosadifiana na 10 Januari 1824, Joseph Aspdin mwanakemia wa Uingereza, alifanikiwa kutengeneza saruji na kwa utaratibu huo kupatikana mabadiliko makubwa katika shughuli za ujenzi. Hatua hiyo ilitambuliwa kama tukio kubwa katika shughuli za kimaendeleo na ujenzi mpya wa nyumba. Joseph Aspdin ambaye alikuwa akifanya utafiti kwa miaka kadhaa ili kutengeneza mada ambayo ingesaidia kuimarisha msingi wa nyumba, hatimaye alifanikiwa kutengeneza saruji baada ya majaribio chungu nzima.

Joseph Aspdin

Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, inayosadifiana na 10 Januari 1920, Jumuiya ya Mataifa ilianza shughuli zake rasmi huko Geneva, Uswisi. Jumuiya hiyo, iliundwa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa shabaha ya kuimarisha amani na usalama duniani. Mwanzoni mwa shughuli za jumuiya hiyo, nchi za Kiafrika na Urusi hazikujiunga na jumuiya hiyo, na badala yake nchi za Uingereza na Ufaransa ndizo zilizobeba jukumu la kuzisaidia nchi hizo. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mnamo mwezi Aprili 1946, uliundwa Umoja wa Mataifa, na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa, ingawa matatizo yaliyokuwa yakiikumba Jumuiya ya Mataifa bado yanaendelea kuukumba Umoja wa Mataifa hadi hii leo.

Jumuiya ya Mataifa

Na tarehe 10 Januari miaka 55 iliyopita, ilibuniwa saa ya elekroniki na wataalamu wa Uswisi, Solvil na Titus baada ya kupitisha miaka 12 ya juhudi zao, hatimaye walifanikiwa kutengeneza chombo hicho kwa kuweka vifaa kadhaa muhimu na makini. Aina hii ya saa haina mipaka kwa watoto wadogo na imetengenezwa kwa umakini mno na inafanya makosa machache sana ikilinganishwa na saa nyingine.