Jan 13, 2018 00:16 UTC
  • Jumamosi, 13 Januari 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Saba Rabiuthani 1439 Hijria sawa na tarehe 13 Januari 2018 Miladia.

 

Mwaka 288 Hijria katika siku kama ya leo, alifariki dunia Thabit bin Qurrah Swabi, mtaalamu wa hisabati, nyota na tabibu katika kipindi cha utawala wa Bani Abbas. Alizaliwa mwaka 221 Hijria mjini Harran uliopo eneo la Mesopotamia nchini Iraq. Thabit bin Qurrah Swabi alikuwa akizungumza lugha za Kigiriki, Kisiriyan na Kiarabu. Alisafiri kwenda mjini Baghdad, Iraq kwa lengo la kusoma na kwa usimamizi wa Muhammad bin Mussa aliyekuwa mtaalamu mkubwa Mwislamu wa hisabati na nyota kipindi hicho, Thabit bin Qurrah Swabi akaingia katika uwanja wa elimu hizo. Alibuni nadharia mpya katika uwanja wa hisabati. Aidha katika utaalamu wa nyota yeye ni katika watu wa kwanza kurekebisha chombo cha Ptolemaic. Thabit bin Qurrah Swabi aliandika vitabu vingi katika uwanja wa tiba, hisabati na nyota, vilivyofasiriwa kutoka lugha ya Kigiriki kwenda Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na kile kiitwacho "Adh Dhakhiratu fii Ilmi al Twib" na "Kitabul Mafrudhaat." ***

Thabit bin Qurrah Swabi

Miaka 1071 iliyopita mwaka 368 Hijiria, alizaliwa mjini (Corduba, Qurtuba) Uhispania, faqihi, mtaalamu wa hadithi, fasihi na mwanahistoria Abu Omar Yusuf bin Abdallah mashuhuri kwa jina la Abdul Birr. Alipata masomo ya msingi kutoka kwa baba yake na walimu wengine wakubwa wa kipindi hicho. Ibnu Abdul Birr aliupa umuhimu mkubwa utafiti, ambapo kwa kipindi cha muda mfupi alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa mjini Andalusia. Kufuatia kukosekana amani na usalama katika mji wa Corduba, Ibn Abdul Birr alilazimika kuhamia mji mwingine wa Daynah ambao kipindi hicho ulikuwa moja ya vituo muhimu vya elimu vya Andalusia, na huko alifanikiwa kuandika vitabu vyake. Miongoni mwa athari za msomi huyu mashuhuri ni kitabu cha "al Istiiab" ambacho kinahusu maisha ya masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw). ***

Abu Omar Yusuf bin Abdallah  Abdul Birr.

Katika siku kama ya leo miaka 568 iliyopita, alizaliwa baharia na mvumbuzi wa Kireno kwa jina la Bartholomew Diaz. Baada ya kusafiri katika Bahari ya Atlantic kuelekea kusini mwaka 1488, Diaz aligundua Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) katika sehemu ya kusini zaidi ya bara la Afrika. Miaka kumi baadaye baharia mwenzake kwa jina la Vasco Da Gama naye pia alifanikiwa kugundua njia ya baharini kuelekea India kupitia eneo hilo.***

Bartholomew Diaz

Siku kama ya leo miaka 327 iliyopita aliaga dunia George Fox mrekebishaji wa Kikristo wa nchini Uingereza. Fox alizaliwa 1624 katika familia ya kidini. George Fox hakuwa akiweza kustahamili mgongano uliokuwako katika maneno na vitendo vya makasisi na wafuasi wa Ukristo na vilevile vita vya watawala wa zama hizo. Akiwa na miaka 19, Fox alikata shauri kufanya utafiti kwa ajili ya kutafuta ukweli. George Fox alikuwa akiamini kwamba, kuna ulazima wa kurejea katika mafundisho asili ya Ukristo na kujiepusha na umwagaji damu na wakati huo huo kusimama kidete kukabiliana na dhulma. Hata hivyo, Fox nae pia alitumbukia katika makosa kwenye itikadi zake. Pamoja na hayo, fikra zake zilipingana na mafundisho ya Ukristo katika zama hizo. Mara kadhaa George Fox alitiwa mbaroni na kutupwa jela na mamia ya wafuasi wake walikuwa wakiteswa gerezani. Harakati yake ya kupigania mabadiliko ya kidini iliendelea baada ya kuaga kwake dunia na harakati hiyo ingalipo. ***

George Fox

Miaka 77 iliyopita katika siku kama ya leo, mkutano wa kihistoria wa nchi waitifaki za Ulaya katika Vita vya Pili vya Dunia ulifanyika mjini London, Uingereza. Mkutano huo ulifanyika kufuatia pendekezo la waziri mkuu wa wakati huo wa Uingereza Winston Churchill, lengo kuu lilikuwa kuratibu siasa za wakuu wa nchi za Ulaya katika medani za vita dhidi ya nchi mbili za Ujerumani na Italia. Vilevile nchi za Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Norway, Luxembourg na Denmark zilishiriki katika mkutano huo.***

Vita vya Pili vya Dunia

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita yaani tarehe 23 Dei 1357 Hijria Shamsia, kulitokea mapigano makali baina ya askari wa utawala wa Shah na wananchi wa Iran na watu kadhaa kuuawa shahidi na kujeruhiwa wakati wa kujiri maandamano ya miji kadhaa ya Iran. Aidha katika siku hii wananchuo na wananchi wa Tehran ambao walikuwa katika mkusanyiko wao mkubwa katika Chuo Kikuu cha Tehran walitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa Shah na waking'ang'ania msimamo wao wa kurejea hapa nchini Imam Khomeini MA aliyekuwa uhamishoni Ufaransa. ***

Na miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, shambulio la kwanza la kemikali la jeshi la utawala wa wakati huo wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam lilitekelezwa dhidi ya Iran ikiwa ni chini ya miezi minne tu tangu Iraq ianzishe vita vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Shambulio hilo lisilo la kibinadamu ambalo lilitekelezwa kilomita 50 magharibi mwa mji wa Ilam magharibi mwa Iran, lilipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa. Jeshi la utawala wa Baath likipata himaya na misaada ya madola ya Magharibi na Umoja wa Kisovieti lilitumia mara chungu nzima silaha zilizopigwa marafuku dhidi yya wananchi na wapiganaji wa Iran katika kipindi chote cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya taifa hili. Takribani watu elfu kumi waliuawa shahidi na laki moja na elfu 30 kujeruhiwa kufuatia mashambuluio hayo ya silaha zilizopigwa marufuku. ***

Silaha za kemikali