Jumapili, 14 Januari 2018
Leo ni Jumapili tarehe 26 Rabiu al-Thani mwaka 1439 Hijria sawa na tarehe 14 Januari 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 974 iliyopita, alizaliwa mjini Marv, moja ya miji ya Khurasan ya zamani ya Turkmenistan ya sasa, Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi, mtaalamu wa hesabati, tabibu na mwanafalsafa wa Kiislamu. Qatwan Marvazi alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu za hesabati, falsafa, fasihi na elimu ya dini ya Kiislamu. Hata hivyo binafsi alipendelea sana elimu ya tiba. Marvazi ambaye alikuwa akijishughulisha na kutoa huduma ya tiba katika mji wa Marv aliandika vitabu kadhaa na moja ya vitabu hivyo ni 'Kiihaan Shenokht' ambacho kinahusu elimu ya hesabati. Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi alifariki dunia mwaka 548 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 921 iliyopita alifariki dunia Hassan al-Sabbah mwasisi wa utawala wa Ismailiyah nchini Iran. Sabbah alizaliwa mwaka 445 Hijiria mjini Qum na akiwa mtoto pamoja na familia yake alielekea mjini Ray, kusini mwa mji wa Tehran. Akiwa mjini hapo alijifunza masomo ya dini ya Kiislamu na Ushia. Hata hivyo akiwa kijana alijiunga na madhehebu ya Ismailiyah. Wafuasi wa kundi hilo kinyume na Mashia wengine baada ya Imam Swadiq (as) walikataa kumtambua mtoto wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) yaani al-Imam al-Kadhim (as) kuwa Imam na badala yake wakamtambua mtoto mwingine wa Imam Swadiq, yaani Ismail kuwa ndiye Imam. Baada ya Hassan al-Sabbah kujiunga na kundi hilo alielekea nchini Misri kwa lengo la kujifunza mafundisho zaidi ya Ismailiyah. Wakati huo viongozi wa Ismailiyah walikuwa ni makhalifa wa utawala wa Fatwimiyah nchini Misri. Mwaka 473 Hassan al-Sabbah alirejea Iran na kuanza kueneza mafundisho ya kundi hilo katika maeneo tofauti ya Iran. Mwaka 483 alidhibiti ngome imara ya Alamūt karibu na mji wa Qazvin na ukawa mwanzo wa harakati ya mapambano dhidi ya utawala wa Seljuk uliokuwa unatawala Iran. Utawala wa Ismailiya chini ya uongozi wa Hassan al-Sabbah ulidhibiti pia ngome tofauti za kaskazini mashariki, kusini na hata katikati ya Iran sambamba na kuua viongozi wengi wa utawala wa Seljuk. Sabbah alifahamika kwa ubora huku akitabahari katika elimu za theolojia, falsafa na elimu ya nyota. Aliwaaachia wafuasi wake vitabu kadhaa.
Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita alizaliwa Albert Schweitzer katika mji wa Alsace-Lorraine huko Ufaransa. Schweitzer ambaye alikuwa daktari na mtaalamu wa muziki, alielekea barani Afrika baada ya kukamilisha elimu katika fani ya udaktari na kuasisi hospitali nchini Gabon. Hadi mwishoni mwa umri wake, Schweitzer alijitolea kuwasaidia na kutibu wananchi maskini wa Kiafrika. Tabibu huyo aliyekuwa na hisia za kibinadamu, ameandika vitabu kadhaa muhimu zaidi kikiwa ni kile alichokipa jina la "Falsafa ya Ustaarabu". Mwaka 1952 Schweitzer alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kutokana na huduma zake kubwa kwa wagonjwa. Alifariki dunia mwaka 1965.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita ulianza mkutano wa kihistoria wa kimataifa wa Casablanca nchini Moroco. Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na Rais wa wakati huo wa Marekani Franklin Roosevelt na Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill, wakiwa viongozi wa nchi muhimu za waitifaki, ulijadili mpango wa mashambulizi dhidi ya Sicily huko Italia, misaada ya nchi waitifaki kwa Russia na masuala mengine ya vita. Mwishoni mwa mkutano huo uliodumu kwa siku kumi, wawakilishi wa nchi zilizoshiriki walitoa taarifa ya pamoja wakiahidi kuendeleza vita hadi wakati wa kusalimu amri bila ya sharti nchi zilizoungana.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita maafisa wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walitekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Salah Khalaf maarufu kwa jila la Abu Iyad akiwa pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Salah Khalaf alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na kiongozi nambari mbili wa Fat'h baad ya Yaser Arafat. Mauaji ya viongozi hao wa ngazi za juu wa PLO tena yaliyofanyika kwa kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi nyingine yaani Tunisia, yalionyesha kwamba utawala haramu wa Israel hauheshimu sheria yoyote ile katika suala la kuwafuta wapinzani wake.
Na siku kama ya leo miaka 7 iliopita, sawa na tarehe 14 Januari 2011 Rais Zainul Abidin Bin Ali wa Tunisia na dikteta wa nchi hiyo alikimbilia Saudi Arabia kufuatia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi. Kukimbia nchi Zainul Abidin, kulihitimisha utawala wa kiimla uliodumu kwa nusu karne wa Habib Bourquiba pamoja na Zainul Abidin Bin Ali na wananchi wa Tunisia wakaonja ladha ya uhuru. Zainul Abidin aliingia madarakani mwaka 1987 kupitia mapinduzi ya kijeshi bila umwagaji damu na kumwondoa madarakani Habib Bourguiba aliyekuwa amejitangaza kuwa rais wa maisha wa nchi hiyo. Bin Ali aliiongoza Tunisia kwa mkono wa chuma kwa miaka 23 huku akiendeleza siasa za kutegemea Wamagharibi na kupiga vita Uislamu. Kujichoma moto kijana mmoja muuza mboga katika kulalamikia dhulma na ukatili wa maafisa usalama wa utawala wa nchi hiyo, kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa Bin Ali na hatimaye kupelekea kupinduliwa dikteta huyo.