Ulimwengu wa Michezo, Jan 15
Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu katika dakika hizi chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti, yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, ndani na nje ya nchi.
Handiboli: Iran yamaliza ya 2
Timu ya taifa ya handiboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya pili katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo yaliyopigwa nchini Qatar. Timu hiyo iliizaba Algeria 31-28 katika mchuano wake wa tatu, na kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili. Iran ilianza vyema mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama Qatar Four-Team International Tournament, kwa kuigaragaraza Oman 32-24, kabla ya kulemewa 33-28 na na mwenyeji Qatar. Algeria ilimaliza ya tatu huku Oman ikivuta mkia. Wiki iliyopita, timu ya taifa ya handiboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali kushindwa na Slovenia katika mchuano wa kirafiki ugenini katika mji wa Ljubljana, ambapo ililemewa na mwenyeji Slovenia kwa kuzabwa magoli 31-19.
Vijana hao wa Kiirani wa mkufunzi Borut Macek wanapasha misuli moto kwa ajili ya duru ya 18 ya Mashindano ya Ubingwa wa Handiboli ya Asia itakayopigwa kuanzia Januari 18 na kumalizika 28 nchini Korea Kusini. Iran ipo katika Kundi A pamoja na Iraq na Japan, huku Kundi B likizijumuisha Australia, Bahrain, Oman na Uzbekistan. Mwenyeji Korea Kusini ipo katika Kundi C pamoja na Bangladesh, Imarati na India huku Kundi D likizileta pamoja China, New Zealand, Qatar na Saudi Arabia. Duru ya 18 ya mashindano hayo ya kikanda itapigwa mjini Suwon, huko Korea Kusini kati ya Januari 18 na 28, na mabingwa wataliwakilisha bara Asia katika mashindano ya dunia mwaka ujao 2019.
Michuano ya CHAN
Michuano ya soka ya CHAN kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani, ilianza kutifua vumbi Jumamosi kati ya wenyeji Morocco na Mauritania. Na kwa kuwa mcheza kwao hutuzwa, vijana wa Kiarabu waliwapeleka mchakamchaka wenzao wa Mauritania, na kuwanyoa kwa chupa. Morocco imeanza vizuri michuano hii kwa kupata ushindi mnono wa mabao 4-0. Mabao ya Morocco yalifungwa na Ismail El Haddad (2), Ayoub El Kaabi huku Achraf Bencharki akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Mauritania.
Huku hayo yakirifiwa, Sudan iliichabanga Guinea mabao 2-1 katika mchuano wao wa ufunguzi siku hiyo hiyo ya Jumamosi katika Uwanja wa Mfalme Mohammed V mjini Casablanca. Mabao ya Morocco yalifungwa na viungo matata Omar Omar na Saifuddin Bakhit. Bao la kufutia machozi la Guinea lilifungwa na Sekou Camara. Morocco ipo kileleni mwa Kundi A ikifuatiwa na Sudan. Michuano ya Kundi A inachukua mapumziko hadi Jumapili ijayo, wakati ambapo Wasudani watavaana na wenyeji Morocco, huku Mauritania ikitoana udhia na Guinea. Hii ni mara ya nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009. Mwaka 2014, Morrocco ilifika katika hatua ya robo fainali ya michuano hii. DRC imeshinda mara mbilli mwaka 2009 na 2016, Tunisia mwaka 2011. Mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya tano bingwa mtetezi akiwa DR Congo.
Kombe la Mapinduzi: Azam yahifadhi taji lake
Ndoto za klabu ya Azam kutetea Kombe la Mapinduzi zimetimia baada ya kuifunga URA ya Uganda kwa penalti 4-3, baada ya dakika za kawaida Azam FC wamefanikiwa kutetea ubingwa wao wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga timu ya URA ya Uganda kwa penalti 4-3, katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye uwanja wa Amaan Zanzibar. Timu hizo zilizokuwa zinakutana kwa mara ya pili kwenye michuano ya mwaka huu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika URA, ndio walioonekana kulishambulia sana lango la Azam lakini hawakuweza kuzitumia nafasi walizozipata. Mshambuliaji Nicholas Kagaba na Kalama Deboss waliweza kufanya mashambulizi ya hatari kwenye lango la Azam lakini kipa Razak Abolora alifanya kazi kubwa ya kuyapangua na kuwa kona ambazo hazikuweza kuisaidia URA. Katika dakika ya kwanza hadi ya tano Azam walipoteza nafasi mbili za wazi kupitia kwa mshambuliaji wake Bernald Arthur ambaye sikunde ya 50 akiwa analiangalia lango la URA alipiga mpira laini uliodakiwa kirahisi na Alianzi Nafian lakini beki wa kushoto Bruce Kangwa naye alipata nafasi nzuri dakika ya pili lakini shuti lake lilishia mikononi mwa kipa huyo. Kipindi cha pili Azam walionekana kurudi kwa kasi na kulishambulia mfululizo lango la URA lakini walinzi wake walikuwa imara na kuondosha hatari zote langoni mwao. Arthur ndiyo aliyekuwa mwenye bahati ya ushindi wa Azam katika muda wa kawaida kutokana na kupata nafasi nyingi za kufunga lakini alishindwa kuzitumia nafasi hizo na kujikuta anampa kazi rahisi kipa wa URA. Baada ya muda wa kawaida kumalizika mwamuzi aliamuru mikwaju ya penati kupigwa na hapo ndipo Azam ilipofanikiwa kutetea taji lao kwa kufunga penati nne huku URA ikifunga penalti tatu na kukosa mbili. Wafungaji wa penalti za Azam ni Himid Mao,Agrey Moris,Yakubu Mohamed na Shabani Idd huku aliyekosa ni Bruce Kangwa.
Kwa upande wa URA wafungaji ni Shafik Kagimu, Charles Ssempa na Jimmy Kulaba wakati waliokosa ni Patrick Mbowa na Brian Majwega. Katika mchezo huo kipa wa Azam Razak Abalora, ndiyo amechaguliwa kuwa kipa bora wa michuano hiyo kutokana na kiwango alichokionyesha kwenye michuano hiyo. Kocha mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amesema kuwa na kipa bora kumesaidia wao kutwaa ubingwa wa michuano ya 12 ya Kombe la Mapinduzi ambayo imemalizika kwa kuifunga URA ya Uganda kwa penalti 4-3, baada ya kutoka sare katika muda wa kawaida.
Hili linakuwa taji la nne kwa Azam kutwaa katika mashindano haya na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo mara nyingi zaidi toka lilipoanzishwa mwaka 1998. Januari 2, mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Mapinduzi, Simba, walianza vibaya mashindano hayo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mwenge kwenye Uwanja wa Amaan.
Mkenya wa kwanza kupiga hat-trick La Liga
Mshambuliaji wa klabu ya Girona nchini Uhispania, Mkenya Michael Olunga ameweka historia siku ya Jumamosi, na kuwa mchezaji wa kwanza wa Kenya kufunga hatrick katika ligi ya Uhispania huku wakiishinda klabu ya Las Palmas 6-0. Olunga aliingia kama mchezaji wa ziada na kufunga katika dakika ya 57, 70 na 79 na kuwa mshambuliaji wa kwanza wa klabu ya Girona kufunga hat-rick katika msimu wake wa kwanza katika ligi ya La Liga. Ushindi huo ulikuwa mkubwa kwa klabu hiyo ya Catalan tangu iingie katika ligi ya La Liga. Olunga mwenye umri wa miaka 23 anaichezea Girona kwa mkopo kutoka klabu ya China ya Guizhou Hengfeng.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta baada ya kuona taarifa hiyo hakukaa kimya, kupitkia ukurasa wake wa Facebook amempongeza Olunga kwa kuandika: “Hongera Michael Olunga kwa kuweka historia kuwa Mkenya wa kwanza kufunga goli katika ligi ya Hispania La Liga na kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick kwa klabu ya Girona katika ligi ya Spain.” Aidha kiongozi wa Muungano wa Upinzania nchini Kenya Raila Odinga ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuhusu kadhia hiyo kuwa: Nampongeza mzawa wa Kenya Michael Olunga, kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa Girona FC kufunga hat-trick katika Ligi ya Uhispania La Liga.
Ligi ya Premier
Liverpool imewazuia Manchester City katika jitihada zao za kumaliza msimu wa Ligi ya Uingereza bila kupoteza mchezo. Jurgen Klopp amesimamisha utawala wa Pep Gurdiola Premier League, baada ya michezo 30 bila kupoteza mechi hata moja hatimaye hii leo Liverpool wamefanikiwa kuipiga Manchester City bao 4 kwa 3. Ni Arsenal Mae 2003 hadi Oktoba 2004 na Chelsea Mei2013 hadi Oktoba 2014 (Mechi 40), ndio ambao wamecheza mechi nyingi zaidi bila kupoteza kuliko rekodi hii ya City iliyodumu kuanzia Aprili mwaka jana. Baada ya matokeo ya leo sasa Liverpool wanakuwa wanaendeleza rekodi yao ya kutofungwa na Manchester City katika uwanja wao wa nyumbani na kufikia mechi 15, idadi kubwa zaidi kwa City kutopata ushindi kwa timh moja ugenini. Kabla ya hapo Arsenal walipoteza mchezo dhidi ya FC Bournamouth, mchezo wa leo ilikuwa mechi ya kwanza kwa Bournemouth kuipiga Arsenal katika michezo yao 6 iliyopita na hii ikiwa mara ya kwanza kwa Bournemouth kupata alama mbele ya timu top 6.
Huku hayo yakirifiwa, Arsenal walikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka Bournmouth katika mchezo mwingine wa Jumapili. Mabao kutoka kwa Callum Wilson na Jordon Ibe yalitosha kuikosesha Gunners pointi tatu muhimu. Sasa kikosi cha Arsene Wenge kina mechi tano bila ushindi na kubaki nyumba kwa pointi tano wakati Bournemoutha wakiendelea na mechi nne bila ya kushindwa. Mlinzi Hector Bellerin aliwapatia wageni waliocheza bila ya Alexis Sanchez, uongozi wakati Alex Iwobi alipomimina kombora kumzidi Asmir Begovic. Lakini Wilson alitumia fusra ya makosa yake Petr Cech na kutumbukiza mpira wavuni. Upande wa Eddie Howe ulipata ushindi wa kwanza kabisa dhidi ya Arsenal na kupanda hadi nafasi ya 13 na pointi 4 kutoka hatarini. Kwa matokeo ya leo msimamo wa ligi umebadilika katika nafasi nne za juu ambapo sasa Liverpool wamepanda hadi nafasi ya tatu ya msimamo huo wakiwa na alama 47 huku wakiwazidi Chelsea kwa tofauti ya mabao.
…………………………TAMATI…………………