Jumamosi, Januari 20, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe Pili Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1439 Hijria mwafaka na tarehe 20 Januari 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1048 iliyopita, alifariki dunia malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Alizaliwa mwaka 341 Hijria katika mji wa Marv, moja kati ya miji ya Iran ya zamani, ambao kwa sasa unapatikana katika ardhi za Turkmenistan. Malenga huyu aliishi katika zama za mwisho za utawala wa Kisaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Maghaznavi. Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi kukisifu kizazi cha Mtukufu Mtume Muhammad (saw) hususan Imam Ali bin Abi Twalib (as). Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha diwani kadhaa za mashairi. ***
Miaka 118 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia John Ruskin mwandishi, mwanafalsafa na mkosoaji mashuhuri wa Uingereza. Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Ruskin alizaliwa mwaka 1819 mjini London. Awali Ruskin alifunzwa na wazazi wake akiwa nyumbani kabla ya kujiunga na chuo cha mjini London na akiwa huko akaanza kutunga mashairi. Malenga huyo wa Uingereza alikuwa mkosoaji wa sekta ya sanaa na alibainisha mitazamo yake kuhusu sanaa katika kitabu chake alichokipa jina la "modern painters". ***
Katika siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, alizaliwa mtengeneza filamu mashuhuri wa Italia, Federico Fellini. Alikuwa mtayarishaji filamu mwenye mbinu makhsusi. Fellini alianza kuandika rasimu ya filamu (scenario) mwaka 1938 na baadaye akaingia katika uwanja wa kutayarisha filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Fellini alishirikiana na mtengenezaji filamu mwingine wa Italia, Roberto Rossellini, katika utengenezaji wa filamu ya "Rome, Open City" (Roma, Mji Usiokuwa na Ulinzi). Miezi sita kabla ya kufariki dunia, Federico Fellini alitunukiwa tuzo ya fahari ya Oscar kutokana na kazi zake kubwa katika medani ya filamu. Filamu mashuhuri zaidi za Fellini ni "Saa Mbili na Nusu", "Juliet of the Spirits" na "The Sweet Life".***
Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo ya leo 30 Dei mwaka 1357 Hijria Shamsia, habari ya kukaribia safari ya kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini kutoka uhamishoni nje ya nchi ilienea kati ya wananchi wa Iran. Habari hiyo ilizusha furaha na vifijo kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Mazungumzo na mijadala kuhusu suala la kurejea nchini Imam Khomeini na jinsi ya kumpokea shujaa huyo ilitanda kona zote na vikao vya wananchi. Katika upande mwingine uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini ulitikisa nguzo za utawala wa kifalme wa Shah. Vibaraka wa utawala huo walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa na wengi miongoni mwao walijiuzulu nyadhifa zao na kukimbilia nje ya nchi. Baadhi ya majenerali wa jeshi waliokuwa karibu na Shah waliwashambulia wananchi katika jitihada za mwisho za kulinda utawala huo wa kifalme. Mashambulizi hayo yalizidisha azma na moyo wa mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. ***
Katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khonsari, faqihi na marjaa mkubwa wa kidini. Baada ya kumaliza masomo yake yya awali kwao alikozaliwa, alisafiri na kuelekea Isfahan na Najaf na kuhudhuria masomo na darsa za walimu watajika wa zama hizo. Baada ya hapo alianza kufundisha. Ayatullah Ahmad Khonsari alikuwa miongoni mwa wanazuoni waliokuwa wakimuunga mkono Imam Khomeini MA wakati wa harakati zake dhidi ya utawala wa Shah nchini Iran na alikuwa mstari wa mbele katika kusukuma mbele gurudumu na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Alimu huyo ametoa wanafunzi wengi waliokuja kuondokea kuwa wasomi na wanazuoni mahiri kama Ayatullah Shahidi Murtadha Mutahhari, Imam Mussa Sadr, Sayyyid Ridha Sadr na wengineo. Ayatullah Khonsari hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi na kualifu vitabu. ***
Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita sawa na tarehe 30 Dei 1357 Hijria Shamsia, Mhandisi Mehdi Bazargan, Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifariki dunia. Mhandisi Bazargan alizaliwa mjini Tehran na kuhitimu masomo yake ya uhandisi wa magari huko nchini Ufaransa. Alikuwa mhadhiri pia katika Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika harakati za kisiasa wakati wa kujiri tukio la kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa. Muda mchache kabla ya mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Mehdi Bazargan alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na kwa pendekezo la baraza hilo alitakiwa kuunda serikali ya muda. Hata hivyo serikali yake ilidumu kwa muda wa miezi 9 tu kutokana na kuwa na tofauti za kimsingi na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kupenya katika serikali hiyo vibaraka waliokuwa dhidi ya mapinduzi. Hatimaye Bazargan aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kuugua maradhi ya moyo.***