Jan 21, 2018 10:36 UTC
  • Aya na Hadithi (4)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kutegea sikio kipindi cha nne katika mfululizo wa vipindi hivi kwa Aya na Hadithi.

Wapenzi wasikilizaji, tumekuchagulieni katika kipindi cha leo mojawapo ya Hadithi Tukufu ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as), muenezaji wa Sunna za Mtume Muhammad (saw) na ambayo inatufundisha jinsi ya kunufaika na Aya nne za Qur'ani Tukufu katika kutatua matatizo tofauti ya maisha yetu ya kila siku. Hadithi hii kwa hakika inamfungulia mwanadamu njia ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye tu katika kukabiliana na hali nne tofauti ambazo huenda zikamkabili maishani, nazo ni hofu kutokana na hatari, huzuni inayotokana na balaa inayomkumba, huzuni inayotokana na njama za maadui na ya nne ni umasikini unaomkumba na kutojua la kufanya.

 

Tunaanza wapenzi wasikilizaji kwa kukunukulieni Hadithi ambayo imenukuliwa na Sheikh as-Swaduq katika kitabu chake cha al-Khiswaal na vilevile cha Aamali kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq bin Muhammad (as) ambaye anasema: 'Ninashangazwa na mtu anayehofia mambo manne ni vipi hakimbilii mambo manne: Ninashangazwa na mtu aliye na woga vipi hakimbilii kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya liliowagusa (173-174).

Ninashangazwa na mtu aliyehuzunika ni vipi hakimbilii kauli yake (mwenyezi Mungu inayosema: Hapana mungu isipokuwa Wewe Subhanaka uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu Mtukufu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na ghamu (dhiki). Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa waumini (Anbiyaa 87-88).

Ninashangazwa na mtu anayefanyiwa makri ni vipi hakimbilii kauli yake (mwenyezi Mungu) inayosema: Nami ninamkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja wake. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa makri (hila) walizozifanya (al-Mu'min 44-45).

Na Ninamshangaa mtu anayetaka dunia na mapambo yake ni vipi hakimbilii kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Hii nikwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu Mtukufu akisema mara tu baada ya kauli hii: Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe, basi asaa (huenda) Mola wangu akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako (al-Kahf 39-40). Na asaa hapa ina maana ya wajibu, yaani inayowajibisha (inayoleta) heri.'

 

Wapenzi wasikilizaji, tunaona hapa nukta ya kuvutia katika maneno ya Imam Swadiq (as) anaposisitiza kauli ya: 'Nimesmikia Mwenyezi Mungu akisema mara tu baada ya kauli hiyo.' Bila shaka kwenye sisitizo hilo kuna utanabahishaji wa kuvutia nao ni kwamba tunapokuwa tunasoma Qur'ani Tukufu tunapasa kutanabahi na kuzingatia kwa makini yale tunayoyasoma ni kana kwamba tunazungumziwa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu, ili kwa njia hiyo tuweze kunufaika inavyopasa na maneno yake matukufu ambayo hatimaye yatatunusuru na kutuwezesha kukabiliana vilivyo na changamoto mbalimbali zinazotukabili katika maisha yetu ya kila siku. Kisha Imam (as) anatufahamisha njia ya kutekeleza kimatendo suala hilo kwa kutunasihi tusome kwa wingi dhikri ya, Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa, tunapohofia jambo fulani kutokana na wingi wa maadui. Hii ni kwa sababu dhikri hii ya Qur'ani ni njia ya kutuletea amani na kutufanya tuhisi kuwa tumesalimika kutokana na hatari hiyo. Na hili ndilo jambo tunalojifunza kutokana na kauli yake Mweyezi Mungu Mtukufu katika aya mbili za 173 na 174 za Surat al-Imran ambazo zinasema: Walioambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni, waogopeni! Hayo yakawazidishia imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa. Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya liliowagusa, na wakafuata yanayomridhisha Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.

Na kama mnavyoshuhudia wapenzi wasikilizaji, Aya mbili hizi zinazungumzia suala lilelile tulilolijadili katika Hadithi tunayoijadili kuhusiana na hofu ambayo watu walio na udhaifu wa Imani hujaribu kuisambaza kwenye nyoyo za waumini kwa kuwatisha kwamba maadui huwa wamejikusanya na kujizatiti kwa silaha kubwa na hatari ambazo wao huwa hawana uwezo wa kukabiliana nazo kwa njia yoyote ile. Na Imam Swadiq (as) anatufundisha kwamba tunapasa kueneza maana hii na kuihusisha na hofu nyinginezo zote ambazo huenda zikaingia kwenye nyoyo zetu kutokana na hatari tofauti zinazotukabili. Kwa msingi huo tunapasa kutibu na kukabiliana na hofu hizo kwa njia hii ya Qur'ani ambapo tunatakiwa kuzibadili hofu hizo na kuwa njia ya kujiongezea imani kwa kukithirisha kauli na dhikri ya Mwenyezi Mungu inayosema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa. Hivi ndivyo tunapoapata kutambua ahadi ya kweli ya Mwenyezi Mungu kwa mja yoyote anayetekeleza jambo hilo, nayo ni kwamba atatuondolea hatari na hofu na kutuepusha na ubaya wowote unaotukabili. Yote haya yanatimia kutokana na baraka za kumtegemea Yeye tu katika kila jambo. Huu ndio ukweli unaodhaminiwa na dhikri ya Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa.

 

Ama kuhusiana na Aya nyingine tatu ambazo zinahusiana na Hadithi hii tukufu iliyopokelewa kutoka kwa Imam Swadiq (as) tutazizungumzia katika kipindi chetu kijacho cha Aya na Hadithi Inshallah. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki. Kutoka Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran hatuna la ziada isipokuwa kukutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia huku tukukitakieni kila la kheri maishani. Basi hadi juma lijalo panapo majaliwa yake Mola, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.