Jan 21, 2018 23:32 UTC
  • Jumatatu, Januari 22, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 4 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na 22 Januari, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Pili Bahman 1357 Hijria Shamsia, watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa, baada ya kujitokeza mapigano ya barabarani kati ya wananchi wa Iran na askari wa utawala wa Kifalme hapa nchini. Wananchi Waislamu wa Iran walikuwa kwenye maandalizi ya kumpokea Imam Khomeini. Wananchi wa matabaka mbalimbali kutoka mijini na vijijini walikuja mjini Tehran kwa shabaha ya kumlaki Imam Khomeini akitokea uhamishoni nchini Ufaransa. Wakati harakati hiyo ya wananchi ikiendelea, maafisa wasiopungua elfu nne wa Jeshi la Anga, walionyesha uungaji mkono wao kwa wananchi, na kutangaza mgomo wa kula chakula, sanjari na kutaka washauri wa Kimarekani waliokuwepo hapa nchini waondoke haraka iwezekanavyo.

Miaka 68 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia msomi wa Kiislamu Haidarqoli Khan Afghani maarufu kwa jina la Sardar Kaboli. Alibobea sana katika elimu za hisabati, nujumu, historia, jiografia, falsafa na fasihi ya Kiarabu. Sardar Kaboli aliwapenda sana Ahlulbait na watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) na ameandika kitabu kuhusu sifa ya historia ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) na watukufu wengine wa nyumba hiyo tukufu. Miongoni mwa vitabu vingine vya Sardal Kaboli ni Sherhe ya Duaa ya Nubda na al Munadharaat.

Sardar Kaboli

Siku kama ya leo miaka 457 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Januari 1561, alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabati wa Uingereza Francis Bacon. Awali, Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye alikamatwa na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza sayansi na elimu nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya. Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis. Msomi huyo wa Uingereza alifariki dunia mwaka 1626.

Francis Bacon

Siku kama ya leo miaka 884 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alizaliwa huko nchini Iraq Ibn Athir Jazari mwanahistoria na mwanafasihi mahiri wa Kiislamu. Ibn Athir alisoma mjini Mosul, Sham na Baghdad kwa maulama watajika kama Khatib Tusi. Alipendelea sana kufanya uhakiki kuhusiana na historia, na kwa sababu hiyo athari zake nyingi zinahusiana na historia. Kitabu mashuhuri zaidi cha Ibn Athir ni kile kinachojulikana kwa jina la "al-Kamil fi Taarikh." Msomi na mwanahistoria huyo wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 630 Hijria katika mji wa Mosul huko Iraq.