Jan 22, 2018 22:56 UTC
  • Jumanne, tarehe 23 Januari, 2018

Lei ni Jumanne tarehe 5 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe 23 Januari 2018

Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa nchini Iran siku ya kuzaliwa Bibi Zainab (a.s) husherehekewa kama 'Siku ya Wauguzi'.

Siku kama ya leo, miaka 1431 iliyopita kulijiri vita vya Mu'utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake. Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) huko Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Kiislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, miongoni mwa sababu zilizomfanya Mtume (saw) kutuma jeshi la wapiganaji 3,000 kukabiliana na utawala wa Roma katika eneo hilo ni kuuawa shahidi walimu 14 wa Qur'an Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham. Katika vita hivyo Mtume alimteua Jaafar bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaaha kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo. Jeshi la Kiislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu'utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo la Kiislamu. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, ambapo naye alitoa amri ya kuwataka Waislamu kurudi nyuma. Hata kama jeshi la Kiislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu za jeshi la adui hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo la adui katika vita vya baadaye.

Januari 23 mwaka 1556 yaani miaka 462 iliyopita, moja kati ya mitetemeko mikubwa kabisa ya ardhi duniani ulitokea katika jimbo la Shaanxi nchini China. Zilzala hiyo ilisababisha hasara kubwa katika jimbo hilo lililokuwa likihesabiwa kuwa na wakazi wengi zaidi nchini China. Watu wapatao 830,000 walipoteza maisha kufuatia janga hilo kubwa na la kutisha la mtetemeko wa ardhi katika jimbo hilo la Shaanxi.

Siku kama ya leo miaka 457 iliyopita, alifariki dunia, Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la 'Abus-Suud', faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu. Abus-Suud alizaliwa karibu na mji wa Istanbul, magharibi mwa Uturuki na kuanza kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu ambapo alipanda daraja na kuanza kufundisha. Mbali na msomi huyo wa Kiislamu kufahamu lugha ya Kituruki, alikuwa hodari pia katika lugha ya Kifarsi na Kiarabu ambapo aliweza hata kusoma mashairi kwa lugha hizo. Miongoni mwa athari za Abus-Suud ni pamoja na 'Tafsir Abis-Suud' 'Dua Nameh' 'Qanun Nameh' na 'Mafruudhaat.'

Katika siku kama ya leo miaka 99 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao. Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye kushika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo akaanza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashti. Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa.

Benito Mussolini

Miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Beitul Muqaddas ambao kibla cha kwanza cha Waislamu kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv. Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu. Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Bunge la utawala haramu wa Israel

Na katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita baada ya kupatikana uhakika kamili wa uamuzi wa Imam Khomeini muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kurejea hapa Iran akitokea uhamishoni Ufaransa, nchini Iran kuliundwa Kamati ya Mapokezi ya Imam. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 50 na ilijumuisha wananchi kutoka vyama na makundi mbalimbali ya mapinduzi. Jukumu kuu la kamati hiyo lilikuwa ni kumpokea Imam na kuchunga usalama wake, kuhakikisha kunakuweko nidhamu, usalama na kuandaa sherehe za mapokezi ya kurejea Imam Khomeini hapa nchini.