Aya na Hadithi (6)
Asslaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kipindi hiki kama mnavyojua huchambua na kuzungumzia Aya za Qur'ani na Hadithi ambazo hufafanua na kutafsiri Aya hizo takatifu.
Katika vipindi viwili vilivyopita katika mfululizo wa makala haya ya Aya na Hadithi tulizungumzia Hadithi iiyopokelewa kupitia vitabu vya kuaminika vya Hadithi kutoka kwa Imam wetu Ja'ffar as-Swadiq (as) ambaye anatuongoza kuhusiana na tiba nne muhimu za Qur'ani Tukufu ambazo zinapasa kumnufaisha mwanadamu katika kutatua matatizo sugu yanayomkabili maishani. Katika hadithi hiyo Imam (as) anatufundisha jinsi ya kunufaika na Qur'ani Tukufu katika kupata kile kinachoweza kutuongoza na kutubakisha katika njia nyoofu inayotuelekeza kwenye mambo yanayomridhisha Mwenyezi Mungu. Tulichambua tiba tatu kati ya hizo katika vipindi vilivyopita na leo tutachunguza tiba ya nne kuhusiana na suala hilo, karibuni.
**********
Ndugu wasikilizaji, Hadithi ya Imam Swadiq (as) inayozungumziwa hapa ni kati ya Hadithi muhimu na tukufu zaidi kati ya Hadithi za mji wa elimu ya Mtume Mtukufu (saw) na ni muhimu kwa kila muumini kuihifadhi. Kwa msingi huo tunaanza kwa kuinukuu Hadithi hiyo ambayo imepokelewa na kunukuliwa na Sheikh Swaduq (MA) katika kitabu chake cha al-Aamali. Imam Swadiq amenukuliwa akisema katika Hadithi hiyo: ''Ninamshangaa mtu anayehofia mambo manne ni vipi hakimbilii mambo manne: Ninashangazwa na mtu aliye na woga vipi hakimbilii kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya liliowagusa (173-174).
Ninashangazwa na mtu aliyehuzunika ni vipi hakimbilii kauli yake (Mwenyezi Mungu inayosema: Hapana mungu isipokuwa Wewe Subhanaka uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu Mtukufu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na ghamu (dhiki). Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa waumini (Anbiyaa 87-88).
Ninashangazwa na mtu anayefanyiwa makri, ni vipi hakimbilii kauli yake (Mwenyezi Mungu) inayosema: Nami ninamkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja wake. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa makri (hila) walizozifanya (al-Mu'min 44-45).
Na Ninamshangaa mtu anayetaka dunia na mapambo yake ni vipi hakimbilii kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu Mtukufu akisema mara tu baada ya kauli hii: Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe, basi asaa (huenda) Mola wangu akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako (al-Kahf 39-40). Na asaa hapa ina maana ya wajibu, yaani inayowajibisha (inayoleta) heri.'

Ndugu wasikilizaji, al-Imam as-Swadiq (as) anapata tiba ya nne ya Qur'ani Tukufu katika Aya za 32 hadi 44 za Surat al-Kahf ambazo zinazungumzia kisa cha mtu mmoja aliyekuwa muumini na mwingine ambaye alipotoshwa na utajiri wake na kumfanya kuwa na majivuno kupindukia. Kutokana na maana ya Aya hizi, Imam (as) anatufundisha jinsi ya kutamka dhikri ya Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kulinda mali na utajiri wa mmiliki wake au kupatikana kwa utajiri huo kwa mtu asiyekuwa nao. Hebu na tuzingatie kwa pamoja Aya hizo za Qur'ani ambapo Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema: Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimpa vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende, na kati yake tukatia mimea ya nafaka. Na hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hayo kilichopungua. Na ndani yake tukapasua mito. Naye alikuwa na mazao mengi. Basi akamwambia mwenzake naye akibishana naye: Mimi nimekushinda wewe kwa mali na nguvu za watu! Akaingia kitaluni kwake, naye hali anajidhulumu nafsi yake. Akasema: Sidhani kabisa kuwa haya yataharibika milele. Wala sidhani kuwa hiyo Saa (ya Kiyama) itatokea. Na ikiwa nitarudishwa kwa Mola wangu, bila ya shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya. Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je! Unamkufuru aliyekuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya kuwa mtu kamili? Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu. Wala simshirikishi na yeyote. Na lau kuwa ulipoingia kitaluni kwako ungelisema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe, Basi asaa Mola wangu akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako, na kukipelekea maafa kutoka mbinguni na kugeuka ardhi tupu inayoteleza. Au maji yake yadidimie usiweze kuyagundua. Yakaangamizwa matunda yake, akabaki akipinduapindua viganja vyake, kwa vile alivyoyagharimia, na miti imebwagika juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti nisingelimshirikisha Mola wangu na yeyote! Wala hakuwa na kundi la kumsaidia kinyume na Mwenyezi Mungu, wala mwenyewe hakuweza kujisaidia. Huko usaidizi ni wa Mwenyezi Mungu wa Haki tu. Yeye ndiye mbora wa malipo, na mbora wa matokeo.
Wapenzi wasikilizaji, kwa kuzingatia kwa makini Aya hizi tukufu katika mwanga wa sehemu ya mwisho ya Hadithi hii ya Imam Ja'ffar (as) tunaweza kutambua hakika zifuatazo zinazohusiana na tiba ya Qur'ani ya kulinda utajiri wa mtu na kadhalika kumletea utajiri mtu asiyekuwa nao. Hakika ya kwanza ni kwamba kutamka dhikri hii yenye baraka kubwa ya Qur'ani Tukufu inayosema Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu huimarisha itikadi ya Umola wa Mwenyezi Mungu kwenye moyo wa mwanadamu na kumfahamisha kwamba kila anachopata humu duniani katika utajiri hutokana na mapenzi na uwezo wake Mungu Muumba. Kwa msingi huo tajiri huweza kulinda utajiri wake kutokana na imani hii na kujizuia kukana itikadi hiyo kutokana na majivuno yasiyo na msingi yanayotokana na utajiri wake. Akienda kinyume na itikadi hiyo ni wazi kuwa atapatwa na yale yaliyompata tajiri yule aliyeharibiwa mazao ya shamba lake kama tulivyoona katika kisa hicho cha Qur'ani Tukufu kutokana na majigambo yasiyo na msingi. Baada ya kuona ukweli wa jambo hilo tajiri huyo alijuta kwa kusema: Laiti nisingelimshirikisha Mola wangu na yeyote!
Hakika ya pili ni kuwa ukithirishaji wa dhikri ya Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu huimarisha maana yake kwenye moyo wa mja na kufungua milango mingi ya neema na heri kwa masikini asiyekuwa na utajiri kama huo na kumbashiria kwamba Mwenyezi Mungu atampa moja ya heri hizo kutokana na imani yake juu ya Umola wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kuerehemu ambaye hapana nguvu ila Kwake.
***********
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafiki amwisho wa kipindi chetu hiki cha Aya na Hadithi ambacho mmekuwa mukikitegea sikio kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. La ziada hatuna isipokuwa kukuageni huku tukikutakieni kila la heri maishani. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.