Jumapili, 28 Januari, 2018.
Leo ni tarehe10 Jamadil-Awwal 1439 Hijira, mwafaka na tarehe 28 Januari 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, na kufuatia serikali ya waziri mkuu wa wakati huo wa utawala wa Shah, Shapour Bakhtiar kuzuia kuwasili nchini Iran Imamu Ruhullah Khomein (MA), kundi kubwa la shakhsia wa kidini walikusanyika katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran na kufanya mgomo mahala hapo. Wasomi hao wa kidini waliweka sharti la kuondoka chuoni hapo kwa kurejea Imamu Khomein. Mgomo huo ni miongoni mwa hatua zilizokuwa na taathira chanya katika historia ya mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Hii ni kwa kuwa serikali ya Bakhtiyar ambayo ilikuwa inaungwa mkono na Marekani ilikuwa inafanya njama kwa upande mmoja, kumzuia Imamu Khomein (MA) kurejea nchini na kwa upande mwingine kupitia ahadi tofauti kuweza kuwatawanya wananchi. Miongoni mwa shakhsia wakubwa walioshiriki katika mgomo huo walikuwa wanamapambano kama vile shahidi Beheshti na shahidi Morteza Motahhari.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, waziri mkuu wa wakati huo wa utawala wa Shah, Shapour Bakhtiar alitanganza azma yake ya kufanya safari mjini Paris, Ufaransa kwa ajili ya kukutana na Imamu Khomein (MA). Hata hivyo mkabala wake Imamu Khomein aliitaja hatua hiyo kuwa ya hadaa kwa kusema: "Kile kilichoelezwa na Shapour Bakhtiar kwamba nimekubali kukutana naye ni uongo, bali ni kwamba asipojiuzulu sitomkubali." Kadhalika siku hiyo wakazi wa mji wa Tehran waliendelea kuratibu maandalizi ya marasimu ya kumpokea Imamu Khomein katika maeneo ya uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran.
Siku kama ya leo miaka mitano iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika kuendeleza utafiti wa anga, kwa mara ya kwanza ilituma angani kiumbe hai katika roketi ya kubebea satalaiti. Kiumbe huyo alikuwa ni ngedere ambaye baadaye alirejea salama ardhini. Majaribio hayo yaliyofanikiwa kwa mara nyingine yaliiweka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo hadi sasa ingali inakabiliwa na mazingira magumu ya vikwazo vya kidhalimu kutoka kwa Marekani na waitifaki wake, katika nchi zilizoendelea kielimu duniani.
Na siku kama ya leo, yaani Jumapili ya mwisho ya kila mwezi Januari, inaadhimishwa duniani kama siku ya kimataifa ya kuwasaidia wagonjwa wenye maradhi ya ukoma. Siku hii iliitwa kwa jina hilo na Raul Follivero, raia wa Ufaransa, yapata nusu karne iliyopita wakati ambapo kulikuwa na idadi ya watu milioni 15 duniani waliokuwa wanaugua maradhi hayo. Kufuatia hali hiyo, Shirika la Afya Duniani WHO liliitaja tarehe 28 ya Januari kuwa siku ya kupambana na ugonjwa wa ukoma duniani. Tangu yalipoanza mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatimaye waathirika wa maradhi hayo wamepungua na kufikia watu milioni mbili kwa sasa. Hata hivyo licha ya juhudi hizo, ugonjwa wa ukoma bado haujatokomezwa kabisa.