Jan 29, 2018 01:03 UTC
  • Jumatatu, 29 Januari 2018.

Leo ni Jumatatu 11 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na 29 Januari 2018.

 Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita sawa na tarehe 9 Bahman mwaka 1357 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, watu wengi wa mji wa Tehran walielekea katika msikiti wa chuo Kikuu cha Tehran, baada ya wanaharakati wa kidini kukusanyika katika chuo hicho wakipinga hatua ya utawala wa Shah ya kumzuia Imam Khomeini (M.A) asirejee hapa nchini. Watu waliandamana katika miji mingine ya Iran kupinga hatua hiyo, na kutaka kupinduliwa utawala wa kidhulma wa Shah na kurejea Imam Khomeini (M.A) hapa nchini. Siku hiyo wanajeshi wa utawala wa Shah kwa mara nyingine waliwashambulia wananchi na kujeruhi na kuua shahidi Waislamu wengi miongoni mwao.

Mgomo wa wanazuoni katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran

Tarehe 29 Januari miaka 55 iliyopita alifariki dunia mshairi wa Kimarekani Robert Frost. Malenga huyo alizaliwa mwaka 1874. Kipaji chake kikubwa katika sanaa ya mashairi kilimuwezesha kuandika diwani yake ya kwanza ya mashairi akiwa na umri wa miaka 20. Frost aliipa diwani hiyo ya mashairi jina la "A Boy's Will". Malenga huyo mara kadhaa alitunukiwa tuzo ya usanii ya Pulitzer.

Robert Frost

Siku kama ya leo miaka 76 baada ya vikosi vya Uingereza na Umoja wa Kisovieti kuivamia Iran tarehe 20 Shahrivar mwaka 1320 Hijria Shamsia, kukatiwa saini makubaliano ya pande tatu baina ya nchi hizo. Kwa mujibu wa mkataba na makubaliano hayo, serikali ya wakati huo ya Iran ikawa haina budi ghairi ya kukubali kuruhusu njia zake za mawasiliano za ardhini, angani na majini kwa ajili ya nchi waitifaki ili zitumie njia hizo kwa ajili kuipelekea suhula kambi ya Umoja wa Kisovieti iliyokuwa ikipigana dhidi ya Ujerumani ya Kinazi. 

Vita vya Pili vya Dunia

Na miaka 842 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Khoja Nasruddin Tusi, mwanafalsafa, mwanahisabati, mnajimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiirani katika mji wa Tusi kaskazini mashariki mwa Iran. Katika maisha yake aliasisi kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran. Aalimu huyo aligundua namna mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya kituo hicho. Kituo hicho kilikuwa na suhula muhimu zaidi ambazo kwa miaka 300 baada ya hapo hazikuweza kushushudiwa katika nchi za Magharibi.