Jumanne, Januari 30, 2018
Leo ni Jumanne tarehe 12 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1439 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 30 Januari mwaka 2018.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita yaani tarehe 10 Bahman 1357 Hijria Shamsia, wahadhiri na matabaka mengine ya wananchi walitangaza mshikamamo wao na kuamua kuungana na viongozi wa kidini waliokuwa wamekusanyika katika msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran nchini Iran kuupinga utawala wa Shah. Katika hali ambayo idadi ya watu katika mkusanyiko ilikuwa ikiongezeka kila dakika, Shapour Bakhtiyar, Waziri Mkuu kibaraka wa utawala wa Shah alilazimika kukubali Imam Khomeini arejee nchini Iran kutoka uhamishoni nchini Ufaransa. Sambamba na hayo ndege za kijeshi za Marekani zilianza kuwaondoa raia wa nchi hiyo nchini Iran.
Katika siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali. Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini. Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi.
Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani. Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya Bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo. Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo.
Na Siku kama ya leo miaka 486 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu Ibn Tulun Dimashqi, aliyekuwa faqihi, mwanafasihi na mwanahistoria huko mjini Damascus, Syria. Ibn Tulun alizaliwa mwaka 880 Hijiria mjini Damascus na katika umri wake wote alifanya jitihada kubwa za utafiti, kufundisha na kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali. Ibn Tulun Dimashqi ameandika vitabu vingi vya thamani kuhusiana na historia ya Kiislamu na pia katika uwanja wa tafsiri ya Qur'ani Tukufu, hadithi, lugha, tiba na irfani. Aidha kitabu cha 'as-Safiinatu al-Tuluuniyyah' ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo.
