Jan 31, 2018 23:11 UTC
  • Alkhamisi tarehe Mosi Februari 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe Mosi Februari 2018.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah sanjari na kutangaza kuunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi. Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".

Imam Khomeini baada ya kuwasili Tehran

Tarehe Mosi Februari miaka 60 iliyopita iliundwa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu ya Syria na Misri. Baada ya kumalizika vita vya Suez na kurudi nyuma askari wa Uingereza, Ufaransa na utawala ghasibu wa Israel kutoka katika ardhi ya Misri, Gamal Abdul Nasser alitambuliwa kuwa kiongozi dhidi ya ukoloni wa Magharibi na dhidi ya Uzayuni katika ulimwengu wa Kiarabu na kupata umashuhuri mkubwa. Hatua ya kwanza ya kuanzisha muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi ilichukuliwa tarehe Mosi Februari 1958 baada ya Syria kutia saini makubaliano ya kuungana na Misri na muungano huo ulianza rasmi baada ya kura ya maamuzi ya tarehe 22 Februari 1958 katika nchi hizo mbili. 

Gamal Abdul Nasser akisaini hati ya muungano wa Misri na Syria

Katika siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, alifariki dunia mjini Tehran dunia Haj Mulla Ismail Sabzawari, mpokezi wa hadithi na hatibu mkubwa wa karne ya 13 Hijria. Mulla Sabzawari alizaliwa katika eneo la Sabzawar lililoko kaskazini mashariki mwa Iran. Alijifunza falsafa kwa Mulla Hadi Sabzawari aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya Mwanafalsafa wa Mashariki. Baadaye alihamia katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu zaidi na kupata daraja ya ijtihad. Msomi huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Majmaun Nurain" na "Nawadirul Aathar". 

Na siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, kulitokea vita vikali na vya umwagaji damu mkubwa maarufu kwa jina la Routier katika eneo lenye jina kama hilo karibu na Mto Ob kati ya jeshi lililokuwa na askari laki moja na 60 elfu la vikosi vya waitifaki wa nchi za Prussia, Austria na Sweden na jeshi lililokuwa na askari elfu 42 la Ufaransa chini ya uongozi wa Napoleon. Katika vita hivyo jeshi la Ufaransa lilishindwa vibaya na waitifaki kutokana na kutokuwa na moyo wa kupigana na uchache wa wapiganaji wake.

Napoleon