Jumapili, 4 Februari, 2018
Leo ni Jumapili tarehe 17 Jamadil-Awal mwaka 1439 Hijria, inayosadifiana na tarehe 4 Februari, mwaka 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1148 iliyopita, alifariki dunia Abul-Abbas Ahmad Ibn Yahya Tha’lab, msomi mashuhuri wa lugha na nahau. Tha’labi aliyekuwa na asili ya Iran ya alizaliwa mwaka 200 Hijiria mjini Baghdad. Kutokana na kumbukumbu yake nzuri alijifunza kwa haraka elimu ya nahau, lugha ya Kiarabu, kusoma Qur’ani na hadithi mbele ya walimu wa zama hizo. Akiwa kijana mdogo tayari alikuwa amehifadhi fasihi ya lugha ya Kiarabu ambapo alilipa umuhimu suala hilo huku akifikia daraja ya juu katika uga huo. Miongoni mwa athari zilizosalia hii leo kutoka kwa Abul-Abbas Ahmad Ibn Yahya Tha’lab ni kitabu cha ‘Majaalisu Tha’labi’ ‘Kitaabul-Faswiih’ na ‘Qawaaidu al-Shi’r.’
Siku kama ya leo miaka 989 iliyopita, alifariki dunia msomi na mwanafalsafa mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu na mwenye asili ya Iran, Abu Hamid Muhammad Ghazali. Alisoma kwa Abu Nasr Ismail elimu ya fiqhi na kwa muda mfupi akainukia kielimu katika elimu za zama zake na kwa utaratibu huo akiwa na umri wa miaka 28 akatokea kuwa msomi mkubwa wa Kiislamu zama hizo. Umashuhuri wa Abu Hamid Muhammad Ghazali ulipelekea khawajah Nizam al-Mulk, mtawala wa wakati huo kumtaka afundishe katika shule ya utawala wake mjini Baghdad. Ghazali alikubali mwito huo, hata hivyo mwaka 488 Hijiria aliacha kufundisha kutokana na matatizo ya kisaikolojia na kifikra ambapo alielekea Hijazi kwa ajili ya kufanya ibada ya Hija na kisha baadaye akaelekea Baitul-Muqaddas, Palestina. Hatimaye alirejea nchini kwake Iran na kuendelea na kazi ya ufundishaji na kufanya uchunguzi wa kielimu. Miongoni mwa athari zake ni kitabu cha ‘Ihyaau Ulumud-Din’ ‘Kimyaau Saadat’ ‘Naswiihatul-Muluuk’ na ‘Maqaaswidul-Falaasifah.’
Siku kama hii ya leo miaka 330 iliyopita Pierre Marivaux mwandishi wa riwaya na michezo ya kuigiza wa Kifaransa alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa. Pierre alianza kujishughulisha na kazi ya sanaa tangu akiwa kijana na kwa muda fulani alishiriki pia katika michezo ya kuigiza hadi pale alipoanza kuandika michezo hiyo. Marivaux alipata umashuhuri mkubwa kutokana na ukosoaji wake katika uandishi wa riwaya. Ameacha athari nyingi za kimaandishi zikiwemo riwaya na michezo ya kuigiza ambapo miongoni mwake tunaweza kuashiria zile alizozipa majina kama ya The Prudent na Equitable Father, The Triumph of Love na The Life of Marianne.
Siku kama ya leo miaka 181 iliyopita, alizaliwa Sayyid Muhammad Ali Shah Abdul-Adhimi, mashuhuri kwa jina la Hidaayat Husseini, faqihi na msomi mkubwa wa Waislamu. Alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya masomo na kwa miaka kadhaa alikuwa akisoma kwa Allamah Sheikh Murtadha Answari mmoja wa wasomi wakubwa wa zama hizo. Baada ya hapo Sayyid Muhammad Ali Shah Abdul-Adhimi alitokea kuwa alimu mkubwa katika uga wa hadithi na elimu ya wapokezi wa hadithi ambapo katika uwanja huo aliandika pia vitabu kadhaa. Kati ya vitavu hivyo ni kile kinachofahamika kwa jina la ‘Wasiilatur-Ridhwaan.’ Sayyid Muhammad Ali Shah Abdul-Adhimi alifariki dunia mwaka 1343 Hijiria na kuzikwa mjini Najaf.
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita nchi ya Sri Lanka ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Nchi hiyo iliyoko kusini mashariki mwa India, ilivamiwa na wakoloni wa Kireno katikati mwa karne ya 16 na baadaye wakoloni wa Kiholanzi, na tangu mwaka 1798 iliunganishwa rasmi na makoloni ya Uingereza. Mapambano ya kupigania uhuru wa Sri Lanka yalianza mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia. Mwaka 1931 Uingereza ililazimika kutoa haki ya kutoa maoni kwa wananchi wa Sri Lanka na kuasisi baraza la kutunga sheria na baraza la utekelezaji. Hata hivyo nchi hiyo ilikuwa bado haijapata uhuru kamili katika masuala ya kigeni. Kwa msingi huo mapambano ya wananchi yaliendelezwa hadi kisiwa hicho kilipopata uhuru kamili mwaka 1948.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita wakati mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah yalikuwa yamefika kileleni, Waziri Mkuu wa utawala wa kifalme hapa nchini Shapor Bakhtiyar alifanya jitihada za kuwatuliza wananchi bila ya mafanikio yoyote. Bakhtiyar alisema katika mahojiano na vyombo vya habari kwamba hangemruhusu Imam Khomeini kuunda serikali ya mpito. Wakati huo uasi wa kiraia, kukimbia wanajeshi na kujiunga na safu za wananchi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na kujiuzulu wabunge, viongozi wa ngazi za juu serikali na kadhalika kuliifanya serikali ipoteze udhibiti wa mambo ndani ya nchi.