Jumatano tarehe 7 Februari, 2018
Leo ni Jumatano tarehe 20 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na Februari 7, 2018.
Siku kama ya leo miaka 757 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Jamadil Awwal 682 Hijria, alizaliwa Muhammad bin Hassan Hilli mwenye lakabu ya Fakhrul Muhaqiqiin katika mji wa Hilla nchini Iraq. Allamah Hilli alibobea na kutabahari kwenye elimu za Tafsiri ya Qur’ani, Fiqh na Usuulul Fiqh. Mwanachuoni huyo alipata elimu ya kidini kutoka kwa mzazi wake Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqiqiin ameandika vitabu vingi miongoni mwavyo ni "Sharh Mabadiul Usul" na "Tahswilul Najat" na “al Kafiya”." Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 771 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 702 iliyopita yaani tarehe 20 Jamadil Awwal mwaka 737 alifariki dunia faqihi wa Kiislamu Abu Abdullah Muhammad ibn Hajj al-Abdari al-Fasi mashuhuri kwa jina la Ibn Hajj. Al Fasi awali alipata elimu kwa maulamaa wa mji wa Fas huko Morocco ya leo. Baadaye alielekea Cairo na kuishi huko hadi mauti yalipomfika. Faqihi Abu Abdullah al Fasi ameandika vitabu vingi vya thamani kikiwemo kile cha al Madkhal. Katika kitabu hicho, Ibn Hajj amechunguza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiakhlaqi, kifiqi, kijamii na kiuchumi.

Siku kama ya leo miaka 540 iliyopita, alizaliwa Thomas More, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Uingereza. Mwanzoni More alisomea elimu ya sheria na baada ya kujiunga bungeni akapewa mazingatio na malkia wa wakati huo na kutunukiwa hadhi ya Ulodi. Hata hivyo Thomas More alitofautiana kinadharia na mfalme wa wakati huo wa Uingereza na hivyo akatiwa jela na kuhukumiwa kifo. Hatimaye More akanyongwa mnamo tarehe sita Julai mwaka 1535 Miladia akiwa na umri wa miaka 57.
Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, alizaliwa mjini Newcastle Edward Granville Browne, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, mtafiti na fasihi wa nchini Uingereza. Awali Browne alisomea fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Cambridge na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Hata hivyo kutokana na kupendelea kwake kusoma tamaduni za mashariki mwa dunia alifanya safiri nchini Iran akiwa na umri wa miaka 25. Aidha mtafiti huyo aliitaja lugha ya Kifarsi kuwa njia bora ya kunakili fikra na tamaduni za Wairan kuelekea maeneo mengine ya dunia. Ni kwa msingi huo ndio maana akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na historia na utamaduni wa Wairani. Mwishoni Edward Granville Browne alijikita katika kufundisha lugha ya Kifarsi na Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, na kufariki dunia mwaka 1926 akiwa na umri wa miaka 54.
Na siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Februari 1974, nchi ndogo ya Grenada iliyoko Amerika ya Latini ilijipatia uhuru wake. Nchi hiyo iliyoko kisiwani, ilivumbuliwa mwaka 1498 na mvumbuzi mashuhuri wa Kihispania Christopher Columbus. Amma baada ya kutokea sutafahumu kati ya nchi za Uhispania, Ufaransa na Uingereza juu ya umiliki wa kisiwa hicho, hatimaye Ufaransa iliidhibiti na kuitawala nchini hiyo mwaka 1674. Baada ya kupita karibu karne moja, mnamo 1783, Waingereza waliikoloni nchi ya Grenada kwa muda wa karne mbili, na hatimaye mwaka 1974 katika siku kama ya leo nchi hiyo ikajipatia uhuru wake.
