Feb 09, 2018 22:09 UTC
  • Jumamosi, 10 Februari, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe tarehe 23 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1439 Hijria mwafaka na tarehe 10 Februari 2018 Miladia.

 

Siku kama ya leo miaka 255 iliyopita kulitiwa saini mkataba baina ya Uingereza na Ufaransa huko katika mji wa Paris. Wafaransa waliutaja mkataba huo kuwa mbaya sana. Hii ni kutokana na kuwa, kwa mujibu wa mkataba huo, baada ya miaka mingi ya vita na mivutano na Uingereza, Ufaransa ilikubali kufumbia macho madai yake yote na maslahi yake ya kikoloni huko India na Canada. Sababu ya kutiwa saini mkataba huo ni kwamba, katika zama hizo Ufaransa ilikuwa imedhoofika kutokana na kujihusisha na vita mbalimbali barani Ulaya na kwa upande wa kijeshi na kiuchumi haikuwa na ubavu wa kuendelea kupigana vita na Uingereza. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 132 iliyopita  kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Muhammad Ibrahim mashuhuri kwa lakabu ya Sayyid al-Ulamaa, alimu na fakihi wa Kiislamu wa nchini India. Alikuwa mmoja wa maulama watajika na mahiri mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria. Baada ya kufariki dunia baba yake, Muhammad Ibrahim alichukua jukumu la baba yake la kueneza mafundisho ya dini katika baadhi ya miji ya India. Mwanazuoni huyo alifanya hima kubwa ya kueneza misingi na itikadi za Kiislamu katika ardhi ya India. Sayyid al-Ulamaa ameacha athari nyingi pia katika uga wa uandishi wa vitabu. ***

Sayyid Muhammad Ibrahim (Sayyid al-Ulamaa)

 

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa amani baina ya tawala waitifaki na zile zilizokuwa zikihasimiana katika Vita vya Pili vya Dunia. Katika siku hii, Marekani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza na Ufaransa zilitiliana saini na nchi zilizoshindwa katika vita hivyo zilizojumuisha Italia, Finland, Poland, Bulgaria Romania na Hungary. Kwa utaratibu huo nchi hizo sita kwa mara nyingine tena zikajipatia mamlaka ya kujitawala. Hata hivyo nchi nne za Poland, Hungary, Romania na Bulgaria ambazo mwishoni mwa vita hivyo zilikuwa zimekaliwa kwa mabavu na jeshi la Umoja wa Kisovieti, zililazimika kuwa chini mfumo wa kikomunisti. ***

Tarehe 10 Februari mwaka 1950 yaani miaka 68 iliyopita Joseph Mc Carthy Seneta wa chama cha Republican cha nchini Marekani aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo akiwatuhumu kuunga mkono ukomunisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Hatua hiyo ilipelekea kuanza kwa kile kilichojulikana kama "McCarthyism" huko nchini Marekani, ambapo kwa mujibu wake wanafikra, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Marekani walifuatiliwa nyendo zao na kusakwa baada ya kutuhumiwa kuwa na mitazamo na fikra za Kikomunisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Kamisheni ya McCarthyism ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa, iliweza kuwafuta kazi karibu watumishi wa serikali wapatao 2000 huku idadi kubwa ya wataalamu na wasomi wakiswekwa jela kwa tuhuma zisizokuwa na msingi.***

Joseph Mc Carthy

 

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, Abbas Iqbal Ashtiyani, mhakiki, mwandishi, mtambuzi wa lugha na mwanahistoria wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1275 Hijria Shamsia na baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran mwaka 1304 alifanikiwa kupata shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Sorbonne cha Ufaransa. Ashtiyani alirejea hapa nchini na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran ***

Abbas Iqbal Ashtiyani

 

Na katika siku kama ya leo  miaka 39 iliyopita, majenerali wa utawala wa Shah waliongeza muda wa serikali ya kijeshi katika mji wa Tehran. Majenerali hao walichukua hatua hiyo ili kuwazuia wananchi kuwaunga mkono na kuwasadia wanajeshi wa kikosi cha anga ambao walikuwa wakishambuliwa na kikosi cha gadi ya Shah, na kwa njia hiyo waweze kumtia mbaroni Imam Khomeini (MA) pamoja na shakhsia wengine muhimu waliokuwa katika harakati za Mapinduzi au kuwauwa. Lakini Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuona mbali na kusoma vyema nyakati, aliwatolea mwito wananchi kupuuza kizuizi hicho kilichowekwa na majenerali wa Shah cha kuongeza muda wa serikali ya kijeshi au sheria za kutotoka nje. Wananchi wanamapinduzi wa Iran pia waliitikia agizo hilo la Imam Khomeini na kumininika katika mitaa mbalimbali na kueneza mapambano yao katika vituo vingine vya kijeshi vya utawala wa kidikteta wa Shah katika mji wa Tehran na miji mingine.**