Feb 12, 2018 01:20 UTC
  • Jumatatu tarehe 12 Februari, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 25 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na 12 Februari, 2018.

Tarehe 12 Februari miaka10 iliyopita aliuawa shahidi Imad Mughnia maarufu kwa jina la Haj Ridhwan, ambaye alikuwa miongoni mwa makamanda wa Hizbullah ya Lebanon, katika shambulizi la kigaidi lililofanyika mjini Damascus, Syria. Kamanda Mughnia aliuawa katika mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa na vibaraka wa Israel katika gari lake. Shahid Mughnia alijiunga na harakati za mapambano baada ya uvamizi wa Israel nchini Lebanon. Baadaye kidogo alijiunga na harakati ya Hizbullah na kushika nyadhifa za juu katika harakati hiyo. Shahid Mughnia alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Hizbullah dhidi ya Israel katika vita vya siku 33 vya utawala huo nchini Lebanon mwaka 2006.

Imad Mughnia

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita serikali ya mpito ya Mapinduzi ya Kiislamu ilianza rasmi kazi zake katika siku za mwanzo kabisa za umri wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Wakati huo huo wananchi waliendeleza mapambano ya kuangamiza kikamilifu mabaki ya utawala wa Shah. Baadhi ya makundi ya wananchi yalichukua jukumu la kulinda taasisi muhimu za serikali katika miji mbalimbali. Wakati huo ulidhihiri udharura wa kuwepo chombo cha kushughulikia kadhia hiyo na kukabiliana na vibaraka na mabaki ya utawala wa Shah. Kwa msingi huo Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu.

کمیته انقلاب اسلامی

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita aliuawa shahidi mwasisi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin na mwanamapambano mashuhuri wa Misri, Ustadh Hassan al Banna. Hassan al Banna aliuawa shahidi katika njama iliyopangwa na Uingereza kwa kushirikiana na Mfalme Faruq wa Misri. Alianza mapambano yake dhidi ya ukoloni na vibaraka wake akiwa chuo kikuu ambapo alianzisha harakati ya kupambana na sera za kupinga dini ya Kiislamu za Uingereza kwa kuasisi hatakati ya Ikhwanul Muslimin hapo mwaka 1928. Harakati hiyo ilikuwa kwa kasi na kuenea katika nchi za Syria, Jordan, Lebanon, Palestina na katika baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika. Serikali ya Misri ilipiga marufuku harakati ya Ikhwanul Muslimin mwaka 1948 na kuwatia jela wanachama wake wengi na kisha kumuua shahidi kiongozi wake Sheikh Al Banna.

Siku kama ya leo miaka 209 iliyopita alizaliwa mtaalamu wa elimuviumbe wa Uingereza, Charles Darwin. Msomi huyo alifanya utafiti kuhusu namna ya kutokea viumbe mbalimbali na alifanya safari ya muda mrefu duniani kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wake wa kielimu. Baada tu ya kurejea aliandika kitabu maarufu cha "On the Origin of Species". Kwa mujibu wa nadharia ya Darwin ambaye ndiye aliyeanzisha mfumo wa Darwinism, chanzo cha viumbe vya leo ni viumbe vidogovidogo ambavyo vilibadilika kutokana na mazingira tofauti kwa miaka mingi na kufikia hali ya sasa.

Hassan al Banna

Katika siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Muawiya bin Yazid, Khalifa wa tatu wa ukoo wa Bani Umayyah aliaga dunia katika mazingira ya kutatanisha. Alichukua hatamu za uongozi baada ya kuaga dunia baba yake yaani Yazid bin Muawiya. Hakuwa na hamu ya kuendelea kuongoza kutokana na kuwa alikuwa akitambua kwamba, Ahlul Bayt (a.s) ndio waliostahiki katika hilo. Muawiya bin Yazid anayejulikana kama Muawiya wa pili alitoa hotuba na kulaani vita vya baba yake yaani Muawiya bin Abi Sufyan dhidi ya Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) na vita vya baba yake yaani Yazid dhidi ya Imam Hussein (a.s) na kuwasifu Ahlul Bayt (a.s).