Feb 16, 2018 01:35 UTC
  • Ijumaa tarehe 16 Februari 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na 16 Februari, 2018.

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1992 aliuawa shahidi katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, huko kusini mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon. Hujuma hiyo iliamsha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon.

Sayyid Abbas Musawi

Siku kama leo miaka 72 iliyopita, yaani 16 Februari 1946 kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya zamani katika Umoja wa Mataifa. Siku hiyo mwakilishi wa Urusi, alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa na mataifa mengine duniani zimepewa nchi tano tu wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwepo malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa.

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1918, Lithuania ilijitangazia uhuru wake baada ya kudhoofika Russia kutokana na kushiriki kwake katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kutokea mapinduzi nchini humo mwaka 1917.  Pamoja na hayo, Moscow iliendeleza mipango yake ya kuiunganisha tena Lithuania na ardhi za Umoja wa Kisovieti, ambapo mwaka 1940 ilifanikiwa kufikia lengo hilo. Ujerumani ya Kinazi iliikalia kwa mabavu Lithuania kwa zaidi ya miaka mitatu katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Bendera ya Lithuania

Miaka 165 iliyopita katika siku sawa na hii ya leo, alizaliwa katika mji wa Tabriz ulioko Kaskazini Magharibi mwa Iran alimu na mjuzi wa lugha wa Kiirani Ayatullah Sheikh Muhammad Qasim Ardubadi. Baada ya kumaliza masomo yake ya kati alisafiri hadi Najaf ambapo alisoma kwa maulama mashuhuri wa mji huo. Msomi huyo mkubwa baada ya kufikia daraja ya ijtihadi alirejea mjini alikozaliwa na kuanza kufundisha huko. Ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwake ni kitabu kiitwacho "Al Shihabul Mubin fii I'jaazil Qur'an." Alifariki dunia mwaka 1333 Hijria.

Na miaka 160 iliyopita mwafaka na leo alifariki dunia mmoja wa wataalamu na malenga wa lugha ya Kiarabu, Abdul Baqi bin Sulaiman Farooqi. Alikuwa na kipawa cha kusoma mashairi ya kuvutia tangu yu kijana. Aidha Abdul Baqi alikuwa mmoja wa wapenzi wa kizazi cha Mtukufu Mtume Muhammad (saw) ambapo aliyadhihirisha mapenzi yake hayo katika mashairi yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Al Baqiyatus Swalihat."