Jumanne tarehe 20 Februari, 2018
Leo ni Jumanne tarehe 3 Jamadithani 1439 Hijria, sawa na tarehe 20 Februari, 2018.
Siku kama ya leo miaka 1428 iliyopita alikufa shahidi Bibi Fatima al Zahra, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima. Alipewa malezi na wazazi wake wawili yaani Bibi Khadija na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kupata maarifa aali ya dini kutoka kwa baba yake. Bibi Fatima alifikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi ndani ya nyumba ya wahyi na ufunuo. Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib ambaye alikuwa kielelezo halisi cha takwa na uadilifu, Bibi Fatima alikuwa na nafasi kubwa na alitoa mchango wa aina yake katika jamii ya Kiislamu. Alikuwa dhihirisho la uchamungu, ukarimu, kujitolea, subira, kujipinda katika ibada na kuwasaidia watu wote na alilea watu adhimu kama Imam Hassan na Hussein (as).

Katika siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, vita kati ya Ufaransa na wapigania uhuru wa Mexico vilimalizika kwa ushindi wa Ufaransa na kushika hatamu za uongozi mwanamfalme wa Austria, Maximilian. Katika vita hivyo vilivyoendelea kwa kipindi cha miaka 5, awali Ufaransa iliungana na Uhispania na Uingereza na baada ya muda mfupi nchi hizo mbili zilijitenga na Ufaransa ambayo iliendeleza vita dhidi ya wapigania uhuru wa Kimexico waliokuwa wakiongozwa na rais wa zamani wa nchi hiyo Benito Juárez. Benito Juárez aliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kifaransa hata baada ya kurudi nyuma na kukimbilia katika maeneo ya milimani ya Mexico. Kiongozi huyo hatimaye alifanikiwa kuangusha utawala wa Maximilian akisaidiwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo.
Katika siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Februari 1947, Uingereza hatimaye ilikubali kuipatia India uhuru wake baada ya kuikoloni nchi hiyo kwa zaidi ya karne mbili. Uhuru wa India ulipatikana kutokana na mapambano ya muda mrefu yaliiyoongozwa na Mahatma Gandhi. Katika kipindi chote cha utawala wake wa kikoloni huko India, Uingereza ilipora utajiri na maliasili za nchi hiyo na kuwasababishia hasara kubwa raia wa India. Mwezi Agosti mwaka huohuo India ikajipatia rasmi uhuru wake na ikagawanyika katika nchi mbili za India na Pakistan.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Esfand 1366 Hijria Shamsia, ndege ya abiria ya Iran ilishambuliwa na kutunguliwa kwa kombora la majeshi ya utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein wa Iraq na kuangushwa, wakati wa vita vya Iran na Iraq. Katika tukio hilo, Hujjatulislam Fadhlullah Mahallati, mwakilishi wa Imam Khomeini kwenye Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) aliuawa shahidi akiwa pamoja na maafisa wa serikali na wabunge 39 wa Iran.
Na tarehe 20 Februari miaka miwili iliyopita aliaga dunia Sheikh Ahmad A'mir, qari na msomaji maarufu wa Qur'ani tukufu wa Misri. Alizaliwa mwaka 1927 katika eneo la Salihiyah huko mashariki wa Misri na kuhifadhi Qur'ani yote akiwa bado mdogo. Baadaye alijiunga na jeshi na mwaka 1963 alifanya kazi kwenye radio ya nchi hiyo.
Qari huyo mashuhuri wa Misri alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kusoma Qur'ani na alifika nchini Iran mara kadhaa katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu kama jaji wa mashindano hayo. Mara ya mwisho msomaji huyo mkubwa wa Qur'ani alitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 2013 na kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu. Baada ya mashindano hayo, Sheikh Ahmada A'mir alisoma Qur'ani katika majlisi iliyohudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei wakati huo akiwa na umri wa miaka 86. Qiraa ya Sheikh Ahmad A'mir katika majlisi hiyo iliwagusa sana hadhirina na kuwafanya wengi wabubujikwe na machozi.