Mar 06, 2018 11:49 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (109)

Ni wasaa na wakati mwingine mnapojiunga nami Salum Bendera katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Sehemu iliyopita ya mfululizo huu ilizungumzia suala la ushindani. Tulisema kuwa, ushindani umegawanyika katika sehemu mbili za ushindani mzuri na mbaya.

 

Aidha tulibainisha kwamba, ushindani salama na usio na rafu ndani yake na ambao unachunga na kuheshimu vigezo vya kimaadili pamoja na miamala ya kiutu na kibinadamu ni jambo la kupendeza kwa mujibu wa akili na sheria, na ni ushindani ambao umekokotezwa na kuusia na mafundisho ya Kiislamu.

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 109 kitazungumzia maudhi na kuwakera watu wengine na jinsi suala hilo lilivyokemewa na kukatazwa katika Uislamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Heshima na kumuenzi ndugu Muumini ni jambo ambalo limekokotezwa na kutiliwa mkazo mno katika mafundisho ya Kiislamu, kiasi kwamba, hakuna mtu mwenye haki ya kumuudhi muumini. Hii ni kutokana na kuwa, kimsingi kuwaudhi watu wengine ni katika madhambi makubwa na mambo machafu ya kimaadili ambayo huyakwaza maisha ya mtu binafsi na ya kijamii.

Mwislamu ni yule ambaye Waislamu wanasalimika kwa ulimi na mkono wake

Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema: Yeyote atakayemuudhi Muumini, kwa hakika ameniudhi mimi na mwenye kuniudhi mimi kwa hakika amemuudhi Mwenyezi Mungu na yeyote mwenye kumuudhi Mwenyezi Mungu kama ilivyokuja katika Torati, Injili na Qur’ani yuko mbali na rehma ya Mwenyezi Mungu. (Jamius Sa’adaat J2).

Maudhi na kuwakera watu wengine ni jambo ambalo halina sura maalumu, bali kila kitendo au neno ambalo hupelekea kuwatafirisha na kuwaudhi watu wengine bila sababu linahesabiwa kuwa ni kuwaudhi wengine.

Kuna wakati maneno yasiyo ya mahala pake au kumuangalia mtu kwa dharau au kutoa sauti ya juu huwafanya watu wengine waudhike. Hali hii ya kuudhi au ya kukera watu wengine iwe ni kwa maneno au kwa vitendo, iwe ina madhara ya kimaada au ya kiroho iwe ni kwa ajili ya mtu mmoja au jamii nzima, iwe ni katika mazingira ya kazi au ya nyumbani, katika mkusanyiko wa watu au katika mazingira ya shule, kwa kujua au kwa kutokujua, iwe ni kwa nia njema au kwa nia mbaya, kwa hali yoyote ile ni maudhi na mtu anayefanya maudhi na kuwakera wengine kwa hakika anakuwa amefanya dhambi kubwa kiasi kwamba, Bwana Mtume SAW siku moja aliwaambia masahaba zake: Je nikujulisheni Mwislamu ni nani? Mwislamu ni yule ambaye Waislamu wanasalimika naye kwa mikono na na ulimi wake.

Ewe Mola! tunakuomba utujaalie tabia njema

Hadithi hii mashuhuri inataka kutufahamisha kwamba, Mwislamu halisi ni yule ambaye hawaudhi watu wengine iwe ni kwa ulimi au kwa mikono yake.

Kwa hakika dini tukufu ya Uislamu haimpi idhini Mwislamu yeyote yule awaudhi na kuwakera watu wengine hata kwa namna anavyowaangalia.

Mtume SAW ambaye ni mbora wa viumbe na ambaye alitumwa na kubaathiwa na Allah kwa ajili ya kuja kukamilisha maadili mema anasema:  Muumini hana haki ya kumuangalia ndugu yake kwa namna ambayo itamfanya audhike.

Watu wengi hudhani kwamba, maudhi ni kwa matusi na maneno machafu tu, bali baadhi ya miamala kama kumtazama mtu kwa dharau au kwa kusonya na kubinua mdomo ni mambo ambayo nayo yanaingia katika suala la maudhi na kero kwa wengine. Haya ni mambo ambayo tunayashuhudia katika maisha yetu ya kila siku katika jamii tunazoishi. Baadhi ya watu kutokana na kukumbwa na maradhi ya kujivuna na kujiona au kujikweza huwadharau watu wengine.

Aidha wengine kutokana na kulewa vyeo na madaraka au mali na utajiri hujiona wao ni wabora na hivyo kuwadharau watu wengine hali ambayo huwafanya wanaodharauliwa kuudhika na kupata machungu. Imam Ja’afar bin Muhammad Swadiq AS anazungumzia maudhi ya mtu kwa mwenzake na jinsi hatua hiyo ilivyokuwa na madhara makubwa ambapo ni sawa na kutangaza vita na Mwenyezi Mungu.

Ni katika tabia njema kumtendea wema aliyekufanyia ubaya 

Imam huyo wa Sita katika mlolongo wa Maimamu 12 kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume saw anasema: Mwenyezi Mungu aliyetuka utajo wake amesema: Kila ambaye atamuudhi mja wangu Muumini, kwa hakika ametangaza vita na mimi.

Katika hadithi hii, Mwenyezi Mungu amemnasibisha Muumini na Yeye na hii inaonyesha adhama, heshima, utukufu na ukamilifu wa Muumini mbele ya Mola Muumba. Mtume Muhammad SAW na Ahlul-Baiti wake watoharifu AS, kama ambavyo walikuwa wakikemea vikali suala la mtu kumuudhi Mwislamu mwenzake, walizungumzia mno suala la mtu kuonyesha huba na mapenzi kwa ndugu yake Mwislamu.

Mtume SAW amesema: Kila ambaye atazungumza na ndugu yake Mwislamu kwa maneno ya huba na mapenzi na akamuondolea huzuni na ghamu aliyonayo, basi ataendelea kuwa katika kivuli cha rehma pana ya Mwenyezi Mungu madhali yungali katika hali hiyo. Aidha amesema katika hadithi nyingine kwamba: Hakuna mja katika uma wangu ambaye atamfanyia huba na wema ndugu yake, isipokuwa Mwenyezi Mungu atamfanya kuwa miongoni mwa wahudumu wa peponi.

Dhambi ya maudhi na kero kwa Muumini ni miongoni mwa madhambi ambayo huambatana na taabu na mashaka ya dunia. Kwa maana kwamba, mtu anayeudhi watu wengine, hukabiliwa na matatizo na mashaka hapa duniani na siku zote huwa mtu wa majanga na masaibu. Mtume SAW katika kuwausia watu analizungumzia suala la kutowaudhi watu wengine kuwa ni bima ya afya na usalama wa mtu. Mbora huyo wa viumbe anawataka watu wajiweke mbali na suala la kuwaudhi watu wengine akilitaja jambo hilo kama ni sadaka.

Mtume SAW amesema: Aliyekamilika zaidi miongoni mwa waumini  ni yule ambaye ana tabia njema zaidi

Mbali na maudhi kwa wengine kuwa na mateso na adhabu hapa duniani, huko akhera pia yule aliyekuwa akiwaudhi watu hapa duniani hatasalimika na adhabu ya siku hiyo, siku ambayo mali wala watoto havitamfaa mtu isipokuwa yule ambaye atamjia Mwenyezi Mungu akiwa na kapu lililojaa amali njema. Siku ambayo cheo au nasaba ya mtu havitamsaidia chochote na wala havitamuongezea kitu katika mizani ya amali zake za kheri.

Kiongozi wa waumini, Ai bin Abi Twalib AS anakitambua kitendo cha kuwaudhi wengine kwamba, kinakinzana na utu na ubinadamu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Tunamuomba Allah atuepushe na kauli na vitendo vya maudhi kwa wengine na atupe tawfiki ya kuishi na wenzetu kwa amani na utulivu.

Hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ninakuegeni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh….