Jumapili, Aprili 8, 2018
Leo ni Jumapili tarehe 21 Rajab 1439 Hijria, sawa na tarehe 8 Aprili 2018, Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1191 iliyopita, yaani mwezi wa Rajab mwaka 248 Hijiria, alifariki dunia Abu Hatam, Sahal bin Muhammad Sajestani. Abu Hatam alikuwa ametabahari katika elimu ya Qur'ani, hadithi, fasihi na mashairi. Mbali na kuwa alikuwa akiisoma Qur'ani Tukufu na kuifundisha kwa hamu kubwa, Abu Hatam pia alijishughulisha na masuala ya kijamii. Msomi huyo ameacha vitabu vingi miongoni mwavyo ni I'irabul Qur'an', na Akhlaqul Insan.
Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, alizaliwa Edmund Husserl, msomi wa hisabati na falsafa wa nchini Austria. Husserl alielekea Ujerumani kwa ajili ya kujiendeleza kielimu ambapo akiwa huko alifanikiwa kufikia daraja ya Uprofesa. Kadhalika Edmund Husserl alifanya utafiti mwingi kuhusiana na elimu ya falsafa. Husserl alitambuliwa pia kuwa mwasisi wa kanuni ya Phenomenology katika falsafa, ambayo ilikuwa na taathira kubwa kwa wanafalsafa wa Kimagharibi. Aidha aliamini kwamba lazima falsafa iambatane na hisabati, kama ambavyo aliamini kwamba dunia lazima iwe nzuri na ya kuvutia. Ameacha athari mbalimbali ikiwemo 'Falsafa ya Hisabati' 'Uchunguzi wa Kimantiki' na vitabu vingine.
Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Swadrud-Din Swadr, mmoja wa maulama wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu mjini Kadhimiya, Iraq. Alipata kusoma alimu ya msingi katika mji aliozaliwa na baada ya hapo akasoma elimu ya fasihi na hisabati huku akijiunga na hauza ya elimu ya mjini Najaf na kufikia daraja ya ijtihadi. Akiwa na umri wa miaka 32 alielekea mjini Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran ambapo alisalia mjini hapo hadi mwaka 1348 Hijiria, ambapo alielekea nchini Iraq. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Mukhtasar Taarikhul-Islami.'
Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliishambulia shule ya msingi ya Bahrul Baqar iliyoko umbali wa kilomita 80 kaskazini mwa mji wa Cairo. Katika mashambulizi hayo ya kutisha watoto 46 waliokuwa wakisoma shuleni hapo waliuawa. Mashambulizi hayo ya kikatili yaliibua hasira ya watu katika nchi mbalimbali duniani. Kwa muda wa miezi mitatu ya awali ya mwaka 1970 ndege za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia maeneo ya kiraia huko kaskazini mashariki mwa Misri. Tarehe 12 Februari mwaka huohuo Wazayuni pia walikishambulia kiwanda kimoja katika eneo hilo na kuua pamoja na kuwajeruhi wafanyakazi 168. Kadhalika Wazayuni waliwaua watu 12 katika mashambulizi dhidi ya mji wa al-Mansura ulio kaskazini mashariki mwa nchi hiyo tarehe 31 mwezi Machi mwaka huohuo wa 1970.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita utawala wa Baathi nchini Iraq uliwaua Shahidi Sayyid Muhammad Baqir-Sadr na dada yake, Bintul Huda. Sayyid Sadr alijifunza Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za kidini akiwa mdogo na kupata daraja ya ijtihadi akiwa kijana. Alikuwa mmoja wa walimu wakubwa wa chuo cha kidini mjini Najaf, Iraq kiasi kwamba nadharia zake katika elimu ya usulu fiqhi zilipewa umuhimu mkubwa na wasomi wengine wa Kiislamu. Msomi huyu aliyekuwa na uelewa na uwezo wa hali ya juu wa kielimu, aliuarifisha Uislamu kwa njia sahihi. Kwa kipindi kifupi Ayatullah Sadr aligeuka na kuwa kiongozi wa kifikra na kisiasa wa wananchi wa Iraq na kuyapa mwelekeo mpya mapambano ya wananchi wa nchi hiyo. Baada ya muda fulani utawala wa nchi hiyo ambao ulihisi hatari kutokana na harakati za Ayatullahi Sadr ulimtia mbaroni na kisha kumuua shahidi mwanazuoni huyo mashuhuri pamoja na dada yake, licha ya malalamiko makubwa ya maulama na wananchi Waislamu wa Iraq. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kitabu cha "Uchumi Wetu", "Hamasa ya Nuru", "Falsafa Yetu", "Mwanadamu wa Leo na Matatizo ya Kijamii", na "Ukhalifa wa Mwanadamu na Ushuhuda wa Mitume."