Jumatano tarehe 25 Aprili 2018
Leo ni Jumatano tarehe 8 Shaaban 1439 Hijria sawa na tarehe 25 Aprili 2018.
Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 5 Ordibeheshti mwaka 1359 Hijiria Shamsia, Marekani ilishambulia kijeshi ardhi ya Iran kwa kutumia helikopta na ndege kadhaa za kivita. Serikali ya Marekani ilifanya mashambulizi hayo baada ya kushindwa njama zake mbalimbali za kutaka kuuangusha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran. Hata hivyo mashambulizi hayo yalikatishwa na tufani kubwa ya mchanga iliyopelekea kuanguka baadhi ya ndege, kushika moto helikopta za Marekani na kuuawa baadhi ya askari wa nchi hiyo huku waliobakia wakiikimbia ardhi ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita Wamarekani laki mbili walifanya maandamano mjini Washington wakiendeleza upinzani wao dhidi ya mashambulizi ya nchi hiyo huko Vietnam. Maandamano hayo yalikuwa miongoni mwa vielelezo vikubwa vya upinzani wa wananchi wa Marekani dhidi ya siasa za kichokozi za serikali ya nchi hiyo huko Vietnam. Katika vita vya Vietnam vilivyoanza mwaka 1964 Marekani ilituma askari laki tano nchini humo ambako makumi ya maelfu miongoni mwao waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa sababu hiyo wananchi wa Marekani walizidisha upinzani dhidi ya vita hivyo na mwaka 1975 Marekani ililazimika kufunga virago na kuondoka Vietnam kutokana na mashinikizo ya ndani na ya kimataifa na kushindwa mara kwa mara jeshi la nchi hiyo katika medani za vita.
Siku kama ya leo miaka 526 serikali ya mwisho ya Kiislamu barani Ulaya ilisambaratika huko Granada. Baada ya kudhihiri dini ya Uislamu na kupanua mamlaka yake katika maeneo ya Asia na kaskazini mwa Afrika, jeshi la Waislamu liliingia kusini magharibi mwa Ulaya kupitia lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) na kulitawala eneo hilo kwa kipindi cha karne 8. Eneo hilo ambao kwa sasa linaitwa Uhispania, wakati huo lilijulikana kwa jina la Andalusia. Katika kipindi cha ustawi wa ustaarabu wa Kiislamu eneo la Granada lilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu huo na makao makuu ya kueneza Uislamu hususan barani Ulaya. Dola la Kiislamu la Andalusia liliangushwa kupitia njia ya kueneza ufuska na maovu baina ya watawala na makhalifa wa wakati huo.
Na katika siku kama ya leo miaka 878 alizaliwa Ibn Rumiyya mpokezi wa hadithi, mtaalamu wa mimea na dawa wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Rumiyya alijifunza hadithi kutoka kwa wasomi na wapokezi hadithi wakubwa wa zama hizo na kujifunza pia elimu ya utaalamu wa mimea sambamba na elimu ya dini. Akiwa Andalusia, Ibn Rumiyya awali alianza kuchunguza na kutambua sifa za mitishamba na baadae alifanya safari katika nchi mbalimbali kama Misri, Iraq na Hijaz. Alijishughulisha na masuala ya utafiti wa mitishamba akiwa huko bila kusahau na kujifunza hadithi. Ibn Rumiyya aliandika vitabu vingi kuhusu mitishamba, fiqih na hadithi, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya vitabu hivyo vimepotea.