Alkhamisi tarehe 3 Mei 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Shaabani 1439 Hijria sawa na tarehe 3 Mei, 2018.
Siku kama ya leo miaka 211 iliyopita ulitiwa saini Mkataba wa Finckenstein kati ya Iran na Ufaransa wakati mfalme Napoleon wa Ufaransa alipokuwa katika vita na nchi nyingine za Ulaya. Kwa mujibu wa mkataba huo uliokuwa na vipengee 16, ilipangwa kuwa Iran ingepata silaha za aina mbalimbali kutoka Ufaransa kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Warusi. Ufaransa pia iliahidi kutuma wataalamu wa mizinga na wahandisi wa masuala ya kijeshi nchini Iran kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo. Kwa upande wake, Iran iliahidi kukata uhusiano wake na Uingereza na kuisaidia Ufaransa katika kupeleka majeshi yake huko India. ***
Siku kama ya leo miaka 503 iliyopita yaani tarehe 3 Mei 1515 manowari za Ureno zilianza kushambulia kisiwa cha Hormoz cha Iran na hivyo kuanzisha wimbi la uingiliaji na ukoloni wa nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati. Kisiwa hicho kiko katika eneo la kiistratijia la lango la Hormoz lililoko katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, kusini mwa Iran. Kutokana na kuwa Iran ilikuwa dhaifu katika upande wa jeshi la majini, wakoloni wa Kireno walivikalia kwa mabavu visiwa kadhaa vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi, kikiwemo cha Bahrain ambacho wakati huo kilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Hatua kwa hatua, Iran iliimarisha jeshi lake la majini, na ilipofika mwaka 1652, iliweza kuvikomboa visiwa vyote vilivyokuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno.

Siku kama ya leo miaka 549 iliyopita alizaliwa Niccolò di Bernardo dei Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."
Siku kama ya leo miaka 589 iliyopita, Jeanne d'Arc alianzisha harakati ya kihistoria ya kuzikomboa baadhi ya ardhi za Ufaransa zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Jeanne d'Arc alikuwa kamanda wa jeshi ambaye alipewa jukumu na Mfalme wa Ufaransa la kuongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Uingereza yaliyolikalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Ufaransa. Hatimaye Kamanda huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kimaonyesho nchini Uingereza kwa tuhuma za kuritadi na kuacha dini na mwaka 1431, aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai.
Tarehe 16 Shaabani miaka 827 iliyopita alifariki dunia Ibn Dahhan mfasiri, mwandishi na malenga wa Kiislamu. Ebne Dahhan alizaliwa Baghdad na kujifunza lugha baada ya masomo yake ya utangulizi na kupokea hadithi nyingi kutoka kwa maustadhi wakubwa. Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitoa kipaumbele maalumu kwa fani ya fasihi, khususan kutunga mashairi na kuwapa moyo pia wanafunzi wake kutunga mashairi.

Na siku kama ya leo miaka 851 iliyopita alifariki dunia mfasiri, faqihi, mpokezi wa hadithi na alimu mkubwa wa Kiislamu Ibn Shahrashub. Alizaliwa mwaka 489 katika mji wa Mazandarani ulioko kaskazini mwa Iran na kuaanza kutafuta elimu na maarifa katika kipindi cha ototoni. Bin Shahrashub alikuwa amekwishahifadhi Qur'ani nzima akiwa na umri wa miaka 8. Alipata ruhusa ya kunukuu hadithi za Mtume (saw) kutoka maulamaa wakubwa wa zama hizo kama Zamakhshari, Muhammad Ghazali na Khatib Khorazmi na alikuwa hodari katika kutunga mashairi. Moja ya mashairi yake ya kuvutia ni lile alilotunga akitaja sifa na matukufu ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Shairi hilo linapatikana katika kitabu cha Manaqib Al Abi Twalib. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika elimu za hadithi na sayansi ya Qur'ani Tukufu.