May 08, 2018 02:18 UTC
  • Leo ni Jumanne tarehe 8 Mei, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 21 Shaabani 1439 Hijria sawa na Mei 8, 2018.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Mei 1945, vilimalizika Vita vya Pili vya Dunia baada ya Wanazi wa Ujerumani kusalimu amri bila ya masharti. Ujerumani ilianza kushindwa vita hivyo tokea mwaka 1943. Vita vya Pili vya Dunia vinahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi kutokea katika historia ya mwanadamu, kwani karibu watu milioni 55 waliuawa katika vita hivyo vilivyosababisha pia hasara kubwa.

Kumalizika Vita vya Pili vya Dunia 

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita mwafaka na tarehe 8 Mei 1902, mji wa Saint-Pierre uliangamia baada ya kulipuka volkano kwenye mlima Pelee kusini mwa Ufaransa. Watu wasiopungua elfu 30 walipoteza maisha yao kwenye maafa hayo yaliyochukua muda wa dakika tatu tu.

Tarehe 8 Mei 1794 aliuawa Antoine Laurent - de Lavoisier mtafiti, mvumbuzi na msomi wa Kifaransa na mmoja kati ya waanzilishi wa elimu ya kemia ya kisasa, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kukatwa kichwa kutokana na amri ya utawala wa Kifalme baada ya mapinduzi ya Ufaransa. Lavoisier aligundua elementi zinazounda hewa katika utafiti wake. Baada ya hapo, mkemia huyo wa Kifaransa aliweza kuvumbua gesi ya oksijeni. Lavoisier anafahamika kama 'Baba wa Kemia ya Kisasa.

Antoine de Lavoisier, mtafiti na msomi wa Kifaransa
 

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita tatibu James Parkinson wa Uingereza aligundua ugonjwa wa Parkinson. Dalili kuu za ugonjwa huo ni zile zinazohusiana na kutetemeka sana kwa baadhi ya viungo vya mwili, kukaza misuli, mwendo wa pole yaani mtu hushindwa kutembea haraka pamoja na kupepesuka. Ugonjwa huo unasababishwa na baadhi ya matatizo ndani ya ubongo na hadi kufikia sasa tiba mujarabu ya maradhi hayo haijapatikana.

James Parkinson, Tabibu wa Uingereza aliyegundua ugonjwa wa Parkinson 
 

Na siku kama hi ya leo miaka 36 iliyopita mji wa Huweize ulioko kusini mwa Iran ulikombolewa katika operesheni kubwa iliyopewa jina la Baitul Muqaddas ya wanajeshi supavu wa Iran kutoka kwenye makucha ya jeshi vamizi la Saddam Hussein wa Iraq. Mji huo wa Huweize unatambuliwa kuwa moja kati ya nembo za ushujaa na ujasiri wa vijana wa Iran. Operesheni hiyo iliongozwa na Shahidi Alamul Huda na wenzake kadhaa waliopambana na maadui hadi tone la mwisho la damu zao katika miezi ya mwanzoni mwa uvamizi wa jeshi la Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ukombozi wa Huweize ulikuwa utangulizi wa ushindi mkubwa zaidi wa jeshi la Iran ya Kiislamu wa kukomboa mji wa Khorram-shahr.

Shahidi Hussein Alamul Huda, mmoja wa makamanda wa hamasa ya Huweize