Jumatatu, Mei 21, 2018
Leo ni Jumatatu, tarehe 5 Ramadhani, mwaka 1439 Hijria Qamaria, sawa na tarehe 21 Mei mwaka 2018 Miladia, na sanjari na tarehe 31 Ordibehesht mwaka 1397 Hijria Shamsia.
Miaka 793 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 5 Ramadhani mwaka 646 Hijria Qamaria, alifariki dunia Afdhaluddin Abu Abdullah Khunji, mtoto wa kiume wa Abdul Malik Khunji, katika karne ya 7 Hijria Qamaria. Alizaliwa mwaka 590 Hijria Qamaria katika mji wa Khunji katikati mwa mkoa wa Khalkhal, kaskazini magharibi mwa Iran, ambako alijifunza elimu ya msingi. Msomi huyo wa Kiislamu ambaye alikuwa mtu mwenye hekima na busara, alikuwa mhadhiri wa masomo ya tiba na pia masomo ya Kiislamu kama Fiqhi na Hadithi. Miongoni mwa kazi zake ni kitabu kiitwacho "Kashful Asrar an Qhawamidhul Afkaar Fii Mantiq".
XXXXXXXXX
Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, Andrei Sakharov, mwanafizikia mashuhuri wa Russia alizaliwa. Alihitimu taaluma ya fizikia katika chuo kikuu cha Moscow mwaka 1941 na kisha akaanza kufanya utafiti wa kina kuhusiana na nishati ya nyuklia. Alikuwa na nafsi muhimu katika utengenezaji wa bomu la hydrogen nchini Russia. Sakharov pia alikuwa muungaji mkono mkubwa wa harakati za kutokomeza silaha za nyuklia na ndio maana akatunukiwa zawadi ya amani ya Nobel hapo mwaka 1975. Miaka mitano baadaye Sakharov alibaidishiwa katika mji wa Gorky, mashariki mwa Moscow kutokana na upinzani wake dhidi ya siasa za utawala wa kikomonisti wa Russia. Hata hivyo ubaidishaji huo ulifikia kikomo mwaka 1986 baada ya Mikhail Sergeyevich Gorbachev kutwaa madaraka. Mwanzoni mwa mwaka 1989 Sakharov alichaguliwa kuwa mbunge katika bunge la Russia lakini akaaga dunia baadaye mwezi Disemba mwaka huohuo.
XXXXXXXX
Na miaka 20 iliyopita na katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Suharto wa Indonesia alilazimika kujiuzulu baada ya kuitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 33. Aliingia madarakani mwaka 1965 baada ya kumpindua Ahmad Sukarno, mwanzilishi wa Indonesia huru ambaye alikuwa amechaguliwa na wananchi wa nchi hiyo. Uhuru wa kisiasa ulibanwa sana katika kipindi cha utawala wa Suharto. Hata hivyo nchi hiyo ilishuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi katika utawala wake katika miongo ya 80 na 90. Pamoja na hayo lakini mgogoro wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia Mashariki katika mwaka wa 1997 ulianzisha malalamiko na maandamano makubwa ya wanafunzi wa Indonesia na taratibu yakachukua mkondo wa kisiasa uliopelekea Suharto kuondolewa madarakani. Ufisadi wa kiuchumi uliofanywa na Suharto pamoja na familia yake ulichochea zaidi kuanguka kwa utawala wake, ambako kulitanguliwa na kujiuzulu kwake madarakani.