Jumatano tarehe 4 Julai 2018
Leo ni Jumatano tarehe 20 Shawwal 1439 Hijria inayosadifiana na 4 Julai 2018.
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulama mashuhuri na marjaa taqlidi wa Kiislamu alifariki dunia. Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Allama Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Hauza ya Kiislamu ya mji wa Najaf akiwa bado kijana mdogo. Alijishughulisha na uandishi wa makala na vitabu na alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisi harakati ya kisiasa huko Iraq iliyojulikana kwa jina la "Hizbul Da'awa al Islamiyya". Ayatullah Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah na jambo hilo liliikasirisha sana Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilifanya majaribio kadhaa ya kutaka kumuua. Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani yenye juzuu 25 kwa jina la "Min Wahyil Qur'an."
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita alifariki dunia mwalimu mkubwa wa fasihi wa Iran Dakta Muhammad Muin baada ya kufanya juhudi kubwa za miaka mingi katika nyanja za utamaduni na mila za Kifarsi. Dakta Muin alizaliwa katika mji wa Rasht kaskazini mwa Iran. Alijifunza fasihi ya Kiarabu ujanani na baada ya kukamilisha masomo yake katika skuli ya Darul-Funun alielekea katika Chuo Kikuu cha Tehran na kujiunga na masomo katika kitengo cha fasihi na falsafa. Mwaka 1321 Hijria Shamsiya Ustadh Muin alianza kufanya kazi ya kufundisha na utafiti katika Chuo Kikuu cha Tehran akiwa mhitimu wa kwanza wa shahada ya udaktari wa lugha na fasihi ya Kifarsi.
Tarehe 4 Julai miaka 242 iliyopita wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini Tangazo la Uhuru wa nchi hiyo katika mji wa Philadelphia. Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa milki ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la Marekani. Wazungu hao wa Ulaya waliandamana na mamilioni ya watumwa kutoka Afrika ambao walitumiwa katika kazi ngumu na za sulubu mashambani na viwandani.
Na siku kama ya leo miaka 622 iliyopita mtaalamu wa lugha na mwandishi mashuhuri wa zama hizo Majduddin Abu Tahir Muhammad Yaaqub Firuzabadi aliaga dunia. Firuzabadi alikuwa pia hodari katika taaluma za hadithi na tafsiri ya Qur'ani na ameandika vitabu kadhaa katika taaluma hizo.
Hata hivyo kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni "al Qamus" ambacho ni miongoni mwa kamusi muhimu za lugha ya Kiarabu. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni "Sifrul Saada" na "Tanwirul Miqyas".
