Jul 11, 2018 13:10 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (117)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya hususan huko nyumbani Afrika Mashariki. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Juma lililopita kipindi chetu kilizungumzia tabia mbaya ya kutuhumu watu wengine na tulisema kwamba, kutuhumu ni katika tabia mbaya za kimaadili ambazo zimekemewa mno na mafundisho ya Uislamu na kitendo hicho kinahesabiwa kuwa ni katika madhambi makubwa. Moja ya hadithi tulizokunukulieni na ambazo zinaonyesha athari mbaya ya kutoa tuhuma ni ile ya Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq AS ambaye amesema: Wakati muumini anapomtuhumu ndugu yake muumini, imani yake hufutika moyoni mwake kama chumvi inavyoyeyuka katika maji; na wakati imani ya muumini inapofutika na kutobakia athari yoyote ya imani katika moyo wake, mafikio yake huwa motoni. Juma hili kipindi chetu ambacho ni sehemu ya 117 ya mfululizo huu, kitazungumzia tabia nyingine mbaya ya kimaadili nayo ni uzuaji na usingiziaji au utungaji uwongo. Kuweni nami hadi tamati ya dakika hizi chache kutegea sikio kile nilichokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Wapenzi wasikilizaji uzushi ni kumzulia uwongo mtu na kumnasibisha na mambo mabaya mtu ambayo kimsingi hana. Tabia hii ambayo ni mwenendo mchafu wa kimaadili imekemewa na mafundisho ya Kiislamu na kutajwa kuwa moja yya madhambi makubwa. Kwa hakika tabia hii hupelekea kutokea mikwaruzano na ukosefu wa maelewano katika jamii na kuzusha mizozo na mifarakano. Wakati mwingine kumzulia mtu huharibu heshima ya mja mwenye maadili mema na kumfanya aonyeshewe kidole cha lawama na wana jamii. Mafundisho ya Uislamu ambayo yanawataka wanadamu waishi kwa amani, usalama, huba na mapenzi yanayoambatana na ushirikiano na kuoneana huruma, yamekemea kwa nguvu zake zote tabia hii mbaya na kuwataka watu wajitenge nayo hasa kutokana na kutokuwa na majaaliwa na hatima njema. Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq (as) anasema alipokuwa akiikemea dhambi mbaya ya kumzulia mtu jambo na kumpandikizia uwongo kwamba: Dhambi ya kumzulia mtu jambo ni nzito kuliko uzito wa milima.

Licha ya kuwa, maneno mawili ya kumtuhumu mtu na kumzulia mtu yanaweza kuonekana kuwa na maana moja, lakini ukweli wa mambo si hivyo kwani kuna tofauti ya kimsingi baina ya maneno haya. Kwenye kutuhumu, mwenye kutuhumu huwa hana uhakika na uwongo wa kile anachomtuhumu mwenzake. Hii ni kutokana na kuwa, dhana yake mbaya huwa ndio chimbuko la yeye kutoa tuhuma. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika kutuhumu huwa kuna viashiria vinavyomfanya mtu amhusishe nduguye na jambo fulani. Kwa mfano, amepita baa au sehemu ambayo watu hunywa pombe na kumuona Bwana fulani amekaa, hivyo akahukumu kwamba, Bwana yule siku hizi ni mlevi licha ya kuwa hajamuona kwa macho yake mawili akinywa pombe akiwa akiwa na bilauri ya kilevi.

Lakini katika uzuaji na uzushi, mtu mwenye kumzulia mwenzake huwa na uhakika kwamba, analolisema na kumsingia mwenzake ni uwongo mia kwa mia.

Ni kwa muktadha huo ndio maana katika hadithi, kuzua na kumzulia mtu kumetajwa kuwa ni dhambi ambayo ni nzito kuliko milima, mbingu na vilivyomo ambapo ni dhambi ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu tu ndio ambayo inaweza kulinganishwa na uzito wake. Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema kuwa: Kuzua na kuzusha ni mithili ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Katika mafundisho ya Kiislamu, mtu mwenye tabia ya kuwazulia watu mambo anahesabiwa kuwa mtu mbaya zaidi ambaye Siku ya Kiama atakumbwa na adhabu kali zaidi katika moto wa jahanamu. Moja ya misdaqi na mifano ya wazi ya uzuaji ni kuwaudhi waumini ambapo aya ya 58 ya Surat al-Ah'zab inasema:

Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio dhaahiri.

Mtume saw akiwa na lengo la kuwafanya Waislamu wajiweke mbali na dhambi ya kuwazulia watu anasema kuwa: Kila ambaye atamzulia muumini mwanamume au mwanamke au amnasibishe na kitu ambacho yuko mbali nacho, Mwenyezi Mungu atambakisha mtu huyo Siku ya Kiama katika moto wa Jahanamu mpaka atakaposafishwa na dhambi hiyo.

Aya ya 20 ya Surat Nisaa inaashiria na kuelezea mfano na misdaqi nyingine ya kumzulia mtu kwa kusema:

Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja wao mmempa chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mtachukua kwa dhulma na kosa lilio wazi?

Kwa kuzingatia kwamba, kuzulia watu na kuwabambikizia mambo ambayo hawajafanya ni dhambi isiyo na msamaha na wakati mwingine kisheria kitendo hicho kinahesabiwa kuwa ni uhalifu na hivyo kufuatiliwa mtu kisheria na kimahakama, si tu kwamba, mtu anapaswa kujiepusha na tabia hiyo, bali anapaswa hata kutokaa na kusikiliza.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anawausia waumini na kuwataka kutosikiliza maneno ya watu wengine kuhusu ndugu yao muumini ambaye wanamtambua kwamba, yuko barabara katika dini na njia ya haki.

Baadhi ya watu katika jamii huwa wepesi wa kuamini maneno ya watu wengine dhidi ya ndugu yao wanaemfahamu vyema na hivyo kutomtendea haki na insafu ndugu yao huyo kwa kuamini maneno ya wengine.

Nukta muhimu katika maudhui hii ni kwamba, waumini wanapaswa kuamini kile wanachokiona kwa macho yao na kutoamini wanachokisikia.

Jukumu jingine ni Mwislamu kumtetea nduguye Mwislamu ambaye amezuliwa na kusingiziwa jambo; kwani kufanya hivyo ni kulinda heshima ya Mwislamu mwenzio. Aya ya 16 ya Surat Nur inasema:

Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!

Baadhi ya hadithi zilizonukuliwav kutoka kwa Bwana Mtume saw zinaonyesha kuwa, kila mwenye kutetea heshima ya ndugu yake Mwislamu basi pepo ni wajibu kwake.

Hadithi hizo zinaonyesha ni kwa kiasi gani suala la kutetea heshima ya Mwislamu lilivyo na thamani kubwa.

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umefikia tamati hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo.

Wassalaamu alaykum warahmatullahi wabarakaatuh…….