Aug 10, 2018 23:31 UTC
  • Jumamosi, 11 Agosti, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 28 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1439 Hijria, mwafaka na tarehe 11 Agosti 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1079 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Abul-Qassim Tabarani mmoja wa maulama wa Kiislamu wa mjini Isfahan Iran aliaga dunia. Alikuwa mmoja wa wanazuoni, wasomi na wapokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijria. Abul Qassim Tabarani alifanya safari katika ardhi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kukusanya hadithi. Baada ya miaka 33 ya uhakiki na mutwalaa alianza kufundisha na kufanikiwa kulea na kutoa wanafunzi wengi mno. Aidha msomi huyo hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu, kwani amevirithisha vizazi vilivyokua baadaye yake vitabu vingi vyenye thamani kubwa.***

Abul-Qassim Tabarani

Miaka 787 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 28 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 652 Hijria As’ad bin Hal’wan Dimashqi daktari na tabibu mashuhuri wa Kisyria alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 593 Hijria na baada ya kusoma elimu ya tiba aliibuka na kuwa katika orodha ya matabibu mashuhuri wa zama zake. Ibn Hal’wan alitabahari pia katika taaluma za fasihi, mantiki na hisabati na ameacha athari zenye thamani kubwa katika elimu hizo. ***

As’ad bin Hal’wan Dimashqi

Katika siku kama ya leo miaka 489 iliyopita, Martin Luther alitangaza rasmi madhehebu ya Protestant. Uprotestanti ulianzishwa na Martin Luther kama harakati ya kidini katika karne ya 16 kwenye ulimwengu wa Kikristo kwa lengo la kufanya mageuzi ya kidini. Harakati hiyo ilianza dhidi ya kanisa Katoliki na udikteta wa viongozi wa madhehebu hiyo kuhusu suala la msamaha wa dhambi unaotolewa makasisi na Papa. Martin Luther aliyekuwa Mjerumani alianza harakati hiyo ya uasi ndani ya kanisa Katoliki baada ya kufasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani tofauti kabisa na amri ya Papa kwa lengo la kuvunjilia mbali taasubi za kimadhehebu za Kikatoliki. ***

Martin Luther

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, Haile Selassie, mfalme wa Ethiopia alitia saini azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokuwa na lengo la kuiunganisha Eritrea na Ethiopia. Ardhi ya Waislamu ya Eritrea ambayo hapo kabla ilikuwa ikikoloniwa na Italia, katika Vita vya Pili vya Dunia ilikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Mwezi Desemba 1950 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha Eritrea kuongozwa kwa mfumo wa shirikisho sambamba na kuunganishwa na Ethiopia. Hata hivyo kutokana na kwamba wananchi wengi wa Eritrea hawakuridhishwa na hatua hiyo pamoja na kupuuzwa haki zao na utawala wa Ethiopia, walizidisha upinzani wao dhidi ya utawala wa Addis Ababa na hatimaye kuanzisha harakati ya kupigania uhuru wa nchi yao mnamo mwaka 1960. Mwaka 1993 mapambano ya wananchi wa Eritrea yalizaa matunda ambapo walishiriki katika kura ya maoni na kupiga kura ya kujitenga na Ethiopia. ***

Haile Selassie

Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Chad ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa na siku hii hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 wakoloni wa Ufaransa waliishambulia Chad na katika kipindi cha miaka mitatu wakaidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mwaka 1958 Ufaransa uliipa Chad hiari ya kujiongoza na miaka miwili baadaye na katika siku kama ya leo nchi hiyo ikapata uhuru kamili na kuchagua mfumo wa uongozi wa jamhuri. Nchi ya Chad inapakana na nchi za Libya, Cameroon, Sudan, Afrika ya Kati, Nigeria na Niger. ***

Bendera ya Chad

Na miaka 9 iliyopita katika siku kama ya leo duru ya 6 ya vita baina ya jeshi la Yemen na Shia Zeidia wa nchi hiyo ilianza katika milima ya kaskazini mwa nchi hiyo jirani na Saudi Arabia. Wapiganaji wa Kishia wa nchi hiyo kutokana kuongozwa na familia ya al-Houthi katika mapambano hayo wameondokea kujulikana kwa jina la Mahouthi. Mashia hao wamekuwa wakipigania kuondolewa ubaguzi wa kiuchumi na kiutamaduni katika eneo lao na kupunguzwa kiwango cha uhusiano na Marekani. Licha ya kuwa vita kati ya jeshi la Yemen na Mashia wa nchi hiyo vilianza mwaka 2004 lakini, duru ya sita ya vita hivyo ilikuwa shadidi na ya muda mrefu. Katika vita hivyo, vikosi vya anga vya Saudi Arabia vilifanya mashambulio katika ngome za  Mashia lengo likiwa ni kulisaidia jeshi la nchi hiyo. Mwanzoni mwa Novemba 2009 vikosi vya ardhini vya Saudia vilianza kupigana vita na kundi la al-Houthi. Hata hivyo kujipanga vyema wapiganaji wa al-Houthi na kuwao kwao katika maeneo ya milimani kulivifanya vikosi vya Yemen na Saudi Arabia kushindwa kufikia malengo yao na kwa upatanishi wa baadhi ya makabila kukafikiwa usitishai vita. ***

Uvamizi wa Saudi Arabia nchini Yemen