Aug 24, 2018 21:01 UTC
  • Jumamosi, 25 Agosti, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1439 Hijria, sawa na tarehe 25 Agosti 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 923 iliyopita, vilianza Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa ni kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu na kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba. Baada ya vita vingi na Waislamu, wapiganaji wa msalaba hatimaye waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Baitul Muqaddas mnamo mwaka 1099, ambako waliua raia wengi na kupora mali zao. Mji huo ulikombolewa mwaka 1187 na wapiganaji wa Kiislamu waliokuwa wakiongozwa na Salahuddin Ayyubi. ***

Vita vya Msalaba

Katika siku kama ya leo miaka 193 iliyopita,  nchi ya Uruguay ilipata uhuru. Tangu Uruguay ivumbuliwe na wagunduzi wa Kihispania mwaka 1516, ilitawaliwa na Wareno na Wahispania. Baina ya mwaka 1810 na 1814 kulitokea uasi uliopelekea umwagaji damu mkubwa, ambapo baada ya matukio hayo, nchi hiyo ikawa huru kwa kiasi fulani. Hata hivyo mwaka 1820 Brazil ikaikalia tena kwa mabavu na miaka mitano baadaye Uruguay ikajikomboa na kujipatia uhuru kamili. ***

Uruguay

Miaka 151 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Uingereza Michael Faraday.  Faraday alizaliwa mwaka 1791 mjini London na licha ya kuwa hakuwa na elimu ya juu lakini alifanikiwa kupata maendeleo muhimu katika fizikia na kemia kwa kutumia majaribio na tajiriba.  Michael Faraday aligundua chombo cha mkondo wa umeme kinachojulikana kwa kitaamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.***

Michael Faraday

Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita yaani tarehe 13 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1338 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi, msomi mkubwa na mwanamapambano wa Iran. Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi ni mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia na aliyepambika kwa elimu na uchaji-Mungu huko mjini Shirazi, moja ya miji ya Iran ya leo. Msomi huyo alipata umashuhuri kutokana na kuongoza mapinduzi ya Waislamu dhidi ya Uingereza. Baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi kugundua kuwa Uingereza ilikuwa na lengo la kudhibiti nchi za Kiislamu kupitia pendekezo la kutaka kukubaliwa mwakilishi wa Londoni nchini Iraq kuwa rais wa nchi hiyo, alitoa fatuwa mashuhuri iliyopewa jina la fatwa ya kujilinda ambayo ilihalalisha mapambano ya silaha ya wananchi wa Iraq dhidi ya mkoloni Mwingereza. Fatwa hiyo iliitia hofu Uingereza ambayo ililazimika kuachana na mpango huo wa kikoloni. ***

Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, wakati wa kujiri  Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, majeshi ya nchi waitifaki yaliivamia na kuikalia kwa mabavu Iran. Wasiwasi ulikuwa umezikumba nchi za Marekani, Ufaransa na Uingereza kufuatia kusonga mbele vikosi vya Ujerumani katika ardhi ya Umoja wa Kisovieti. Kwani nchi hizo zilikuwa zikitambua kwamba, endapo Ujerumani itaushinda Umoja wa Kisovieti maslahi yao katika eneo la Mashariki ya Kati yangekuwa hatarini. Ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana madola hayo yakapeleka huko Umoja wa Sovieti silaha na vifaa vingi vya kijeshi kupitia ardhi ya Iran. Licha ya Iran kutangaza kutounga mkono upande wowote katika vita hivyo, Umoja wa Sovieti ulianza kuishambulia Iran kutoka upande wa magharibi na mashariki, huku majeshi ya Uingereza yakitelekeza mashambulio kama hayo kwa upande wa kusini. ***

Kukaliwa kwa mabavu Iran katika Vita vya Pili vya Dunia

Na katika siku kama ya leo miaka 50 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikwea kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za maeneo mengi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia. ***

Ayatullah Agah Bozorge Tehrani (wa katikati)