Sep 09, 2018 11:29 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (66)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 66.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi chetu hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika sehemu iliyopita ya 65 tulisema kwamba kupitia uchaguzi wa kimaonyesho na wa mgombea mmoja tu wa urais, Abd Rabbuh Mansour Hadi, makamu wa aliyekuwa rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh, alichaguliwa kuwa rais ili kudhibiti mabadiliko ya kimapinduzi nchini humo na kukidhi matakwa ya wananchi. Hata hivyo katika kipindi cha utawala wa Mansour Hadi, na kutokana na serikali yake kutojali matakwa ya wananchi, kwa mara nyingine, Yemen iligeuka uwanja wa makabiliano kati ya makundi na mirengo tofauti ya kisiasa, na mashindano na mivutano baina ya wadau wa ndani na madola ajinabi ya nje ya nchi hiyo. Kutokana na kupamba moto malalamiko na manung'uniko ya wananchi sambamba na kushadidi hisia za kukata tamaa na kupotea matumaini ya kuthibiti kaulimbiu na ahadi zilizotolewa na serikali ya maridhiano ya kitaifa, kiongozi wa harakati ya Ansarullah, Abdulmalik Al-Houthi aliweza kuhamasisha na kuvutia uungaji mkono wa umma mkubwa wa wananchi, ambao wengi wao hawakuwa Waislamu wa madhehebu ya Zaydiyyah wala wa kabila la Houthi na kuweza kuingia kirahisi mji mkuu wa Yemen, Sana'a.  Kabla ya kuchukua uamuzi wa kubeba silaha, wafuasi wa harakati ya Ansarullah walitumia muda mwingi kufanya mgomo wa kuketi kwenye medani na viwanja vikuu vya mji mkuu huo wa Yemen, lakini badala ya viongozi wa serikali kushughulikia matakwa yao waliwabeza na kuwadharau. Kwa mtazamo wa wataalamu wengi, laiti kama harakati ya Ansarullah ingekuwa imechukua hatua hiyo pasi na kuwa na uungaji mkono mkubwa wa watu ndani ya jamii ya Wayemeni ambao hawakuwa Mazaydiyyah wala Wahaouthi, rais wa nchi hiyo angeweza, kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, kutoa amri ya kushambuliwa moja kwa moja ngome kuu ya harakati hiyo mkoani Sa'dah na vuguvugu lao kuzimwa papo hapo. Lakini uungaji mkono wa Wayemeni wengi kwa matakwa ya harakati ya Ansarullah ulimfunga mikono Abd Rabbuh Mansur Hadi na kumfanya ashindwe kuchukua hatua juu ya suala hilo, na badala yake akatumia mbinu maalumu ya kutangaza kuwa yeye hapendelei upande wowote katika vita na mgogoro uliojitokeza.

Umoja wa Kiislamu

 

Baada ya uongozi wa vuguvugu la mapinduzi ya Yemen kuwa chini ya udhibiti wa harakati ya Ansarullah huku Saudi Arabia ikiwa na hofu juu ya hatima na muelekeo wa mageuzi hayo, Riyadh ilimshawishi rais, waziri mkuu na serikali nzima ya Sana'a wajiuzulu kwa mpigo; na kwa njia hiyo ukorogaji jungu la fitna ya mgogoro kwa lengo la kuipigisha magoti harakati ya Ansarullah ukawa umeanza rasmi nchini Yemen. Hata hivyo kwa uongozi wa harakati ya Ansarullah, kamati za kimapinduzi ziliratibu na kupendekeza katiba ya muda na kuunda mabaraza ya usalama na ya urais na kuthibitisha uwezo wao wa kuendesha nchi na kuivukisha Yemen kwenye kipindi kigumu cha mpito. Ushindi huo uliwashtusha wengi duniani kote, na tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa kitovu cha mvuto na mazingatio katika upeo wa kimataifa, kwa sababu uongozi wa mapinduzi ya wananchi wa Yemen uliingia mikononi mwa kundi linalotokana na madhehebu ya Zaydiyyah, ambayo ni moja ya madhehebu za Kishia na ambayo miaka mitano kabla ya wakati huo ilikuwa imetengwa na kuwekwa nje kabisa ya ulingo wa siasa za Yemen. Hatua makini zilizochukuliwa na wanamapinduzi wa Yemen kwa ajili ya uendeshaji nchi, kudhibiti hali ya mambo na kukabiliana na hatua za kutaka kuigawanya Yemen vipande vipande ziliwezesha kuzimwa njama ya kutaka ionekane kwamba kuna ombwe la uongozi nchini na pia kutaka harakati ya Ansarullah ionekane kuwa haina uwezo wa kuendesha nchi, pasi na kutokea madhara yoyote kwa nchi. Kwa utaratibu huo wanamapinduzi waliendelea kupata mapenzi na uungaji mkono wa wananchi na wakati huohuo kuthibitisha kwamba wanao uwezo unaotakiwa kwa ajili ya kuendesha nchi yao.

Katika hali na mazingira hayo magumu yaliyokuwa yakiwakabili wananchi wa Yemen, baadhi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu zilianza kutekeleza mpango wa kufunga balozi zao zilizokuweko katika mji mkuu Sana'a, ili kwa kuifanya hali ya Yemen ionekane kuwa mbaya na ya mgogoro mkubwa, ziweze kuandaa mazingira ya kuwashinikiza kisiasa wanamapinduzi wa nchi hiyo. Sambamba na hatua hiyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo pia liliitisha kikao kwa ajili ya kupitisha azimio la kutoa kibali na kuidhinisha uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya Yemen. Hata hivyo njama hiyo ilizimwa kwa kura ya veto iliyopigwa na Russia. Kushindwa huko na tab'an kughadhibishwa viongozi wa utawala wa Aal Saud na waungaji mkono wao yaani Marekani na hali hiyo, kuliifanya Saudi Arabia ichukue hatua ya kuanzisha hujuma za kijeshi za mashambulio ya anga dhidi ya nchi ya Yemen. Aal Saud ilikitumia kisingizio cha kuihami serikali ya Mansour Hadi kuhalalisha uvamizi wake huo wa kijeshi; na hadi hivi sasa imeshateketeza roho za maelfu ya watu wakiwemo wanawake na watoto wasio na hatia na kuwajeruhi pia maelfu ya wengine. Si hayo tu, lakini kwa hatua yake ya kuzishinikiza baadhi ya nchi za Kiislamu kuzitaka ziiunge mkono na kushirikiana nayo katika hatua yake haramu ya kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Yemen, Riyadh imeshadidisha na kupanua mpasuko na utengano baina ya nchi za Kiislamu; katika hali ambayo kwa mujibu wa sheria za kimataifa, endapo nchi moja itataka kuchukua hatua ya kuivamia na kuishambulia kijeshi nchi nyingine itakuwa na haki ya kufanya hivyo baada ya kupata kibali cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa au endapo kama sehemu ya ardhi yake itakuwa imevamiwa na nchi hiyo, ambapo si lolote kati ya mawili hayo limethibiti katika hujuma na uvamizi wa Saudia dhidi ya Yemen.

 

Lakini yote hayo yanaonyesha kuwa sheria na uadilifu ni misamiati ya kale ambayo imeshafutwa kwenye kamusi ya jamii ya kimataifa, kwa sababu nchi nyingi za Magharibi ikiwemo Marekani, si tu hazijachukua hatua yoyote kukabiliana na hujuma na mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, lakini pia zimeiunga mkono nchi hiyo. Kinachoumiza zaidi ni kwamba nchi nyingi za Kiislamu pia, badala ya kuwahami na kuwaunga mkono wananchi madhulumu na wasio na ulinzi wa Yemen au angalau kuchukua hatua ya usuluhishi kwa lengo la kusimamisha jinai hiyo ya kivita, zimeamua, ama kwa sababu ya vitisho au kurubuniwa na viongozi wa utawala wa Aal Saud, kuunga mkono mashambulio ya kijeshi ya nchi hiyo dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen na kutoa ushirikiano katika usababishaji maafa makubwa ya kibinadamu ndani ya nchi hiyo. Suali tunalobaki kujiuliza hapa ni je, utafika wakati wa nchi za Kiislamu kuzinduka na kuelewa zinachokifanya?

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa lakini nikiwa na matumaini kwamba mtajiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 67 ya mfululizo huu. Basi hadi wakati huo nakuageni, huku nikikutakieni heri na fanaka maishani.

Tags