Sep 09, 2018 14:27 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya tano ya kipindi hiki kipya cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia namna ambavyo Imamu Khomeini (MA) alivyoitaka serikali kuhakikisha inasimamia uadilifu katika jamii kwa lengo la kuyafanya maisha ya wananchi kuwa mazuri na ya kuridhisha. Tukasema tena kwamba, mtukufu huyo aliitaka serikali, viongozi na hata mubalighina kufuatilia maisha ya watu masikini na kwenda maeneo wanayoishi na kisha kutatua shida zao ambapo alisisitiza kwamba serikali ni mali ya kila mwananchi. Leo tutazungumzia suala la udharura wa kutokomezwa matabaka katika jamii, karibuni.

Ndugu wasikilizaji Imamu Khomeini (MA) alikutaja kusambaratisha mpasuko wa kimatabaka na kugawanywa kwa usawa nyenzo na utajiri wa jamii, kuwa ni mambo muhimu yanayofanikisha kufikiwa uadilifu wa kijamii na nyenzo mbili zinazohitajika kutumiwa na serikali, na hivyo kuilazimisha serikali kwa mara nyingine kuyasimamia vyema mambo hayo. Katika kubainisha nyenzo ya kijamii na inayohitajika, anawataka matajiri wa jamii kugawa utajiri wao na kuwazingatia watu masikini wa jamii, ili kwa njia hiyo angalau waweze kuondoa mgawanyiko wa kimataba. Ugawaji huo wa utajiri ni kwa maslahi ya watu wa matabala tofauti kwa kuwa haraka suala hilo hunaondoa hasira na malalamiko ya watu masikini na kuhusiana na hilo Imamu Khomeini anasema: “Hii haikubaliki kwamba watu fulani waishi maisha ya juu na kila kitu kiwe kwa ajili yao, na watu wengine waishi maisha ya chini. Jambo hilo si tu kwamba halikubaliki na matiki ya Uislamu, bali sio usawa. Mnatakiwa kufikiria kusiwepo  utofauti huu wa kimataba, ni lazima kuwepo mgao, Uislamu unataka mabadiliko.” Mwisho wa kunukuu. (Sahifeye Nur cha Imamu juzu ya 8 uk 37.) Kadhalika mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitaja hatua ya serikali ya kugawa kwa usawa utajiri katika jamii kuwa inayokamilisha hatua za kujitolea kwa kusema: “Sisi wenyewe tutawafuatilia wale watu wenye mali nyingi, sambamba na kuchunguza utajiri wao. Serikali ya Kiislamu ni mfumo wa kiuadilifu.” Mwisho wa kunukuu.

******

Mtazamo wa Imamu Khomeini (MA) kuhusiana na uadilifu wa kiuchumi, umeakisiwa vizuri katika hati ya kisheria ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika misingi tofauti ya katiba suala hilo limefanywa kuwa msingi mkuu wa dhihirisho la kisheria na fikra za uasisi wa Jamhuri ya Kiislamu katika uga wa uadilifu wa kiuchumi. Mwanzoni mwa katiba na kwa uwazi, wadhifa wa serikali ya Kiislamu umeashiriwa kuwa ni kuandaa mazingira bora kwa ajili ya kuibua vipaji na matokeo yake, kuweza kudhamini nyenzo  sawa na kuibua nafasi za kazi na kujishughulisha kwa ajili ya watu wote na pia kuondoa mahitaji muhimu kwa lengo la kuendeleza harakati kamilifu. Aidha kumesisitizwa kuimarisha uadilifu kama lengo kuu la uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika uwanja huo, serikali inahimizwa kuondoa ubaguzi na badala yake kuweka nyenzo za kupatikana uadilifu kwa ajili ya watu wote na katika nyuga zote za kimada na kimaanawi. Aidha katika kipengee cha tatu cha katiba, kumebainishwa udharura wa kufikiwa uchumi sahihi na wa kiadilifu kwa ajili ya ustawi na kuondoa umasikini na kutokomeza tabaka la watu wasiokuwa nacho katika uga wa chakula, makazi, ajira, afya na kuwadhaminia bima.

*******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu tano ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mbali na kusisitizia juu ya kudhamini mahitaji muhimu ya raia, imeelezea masuala yasiyofaa ambapo ili kufikiwa uadilifu wa kiuchumi, inakataza mfumo wa kujirundikia utajiri. Masuala kama vile kuzuia fursa za kazi kwa ajili ya watu wngine, kuzuia kumdhuru mtu mwingine, kuzuia mfumo wa kuwawekea vikwazo watu wengine, ulimbikizaji mali, riba na miamala mingine ya batili na iliyo haramu, ikiwemo kufanya israfu (kufanya ufujaji mali nk) na ubadhirifu katika masuala yote yanayohusiana na uchumi, matumizi ya fedha, uwekezaji, uzalishaji na ugavi na utoaji huduma, kuzuia kujijali na kukithirisha kujilimbikizia mali kwa watu na makundi fulani ya watu maalumu na pia jukumu la serikali kama muhusika mkuu la kuzuia kuwafanyisha kazi watu kwa nguvu au kuzuia kubagua kazi, ni kati ya mambo ambayo yamesisitizwa na katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa uchumi na kwa ajili ya kufikiwa uadilifu wa kiuchumi katika jamii. Kadhalika kipengee cha 29 cha katiba kimetaja usimamizi wa bima katika nadharia ya ustaafu, ukosefu wa ajira, uzee, kufukuzwa kazini, kukosa usimamizi, kupata ajali, majanga, uhitaji wa huduma za afya na matibabu na usimamizi wa kidaktari, kuwa ni haki ya kiujumla ambapo serikali inatakiwa kuyasimamia vyema katika kuunga mkono kifedha na kuhakikisha yanaweza kuwaingizia wananchi kipato na kuwafanya waweze kushiriki katika shughuli za kijamii.

*******

Ndugu wasikilizaji, ili kufikiwa nadharia ya Imamu Khomeini (MA) katika sekta za uchumi wa nchi, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kando na sekta ya serikali na ubinafsishaji, imezitaka sekta za ushirika pamoja na serikali kulipa umuhimu suala hilo, kama ambavyo pia inazitaka kuhakikisha kwamba zinafanya juhudi ili kufikiwa uadilifu. Kipengee cha 44 cha katiba kinazungumzia sekta ya ubinafsishaji kuwa inayokamilisha shughuli za kiuchumi nchini, ambapo serikali na sekta za ushirikaa zimetakiwa kuizingatia na kufanya juhudi  katika uga huo. Kwa msingi huo, sekta ya ushirika inatajwa kuwa tegemezi muhimu kwenye uchumi wa Iran ambapo sehemu kubwa ya watu wengi wa jamii ni wale ambao hawana uwekezaji wa kutosha na hawawezi kushindana na sekta ubinafsishaji. Suala hilo ni muhimu kwa ajili ya kufikiwa uadilifu wa kiuchumi na kuzuia kurundikana utajiri katika mikono ya watu na kundi la wachache ambapo kwa njia hiyo watu wengi wa jamii wataweza kufikia uadilifu. Hii ni kwa kuwa sekta ya ushirika inazuia njia ya kupenda kujitanua kwa sekta ya ubinafsishaji sambamba na kuzuia mwenendo wa kubadilika serikali na kuwa ya kimabavu.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya tano ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.  

Tags