Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-7
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya saba ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Katika kipindi kilichopita, tulizungumzia haki na uhuru wa kisiasa ambao umeandaliwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa raia wake. Katika uwanja huo tumeashiria kwamba wafuasi wa Uzartoshti na Mayahudi kila wana wawakilishi wao bungeni, huku Wakristo wa Ashuri na Wakeldani (Wakaldu) nao wakiwa na mwakilishi mmoja. Mbali na hayoi ni kwamba Wakristo wa Armenia, kaskazini na kusini mwa nchi wana mwakilishi mmoja bungeni ambaye anawakilisha kila moja ya makundi hayo ambapo wawakilishi hao huchaguliwa na wafuasi wa jamii hizo. Leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi.
*************
Ndugu wasikilizaji, moja ya asili nyingine ya uadilifu wa kisiasa katika fikra ya Imam Khomeini (MA) ni kutambua haki ya usimamizi wa kijamii wa wananchi juu ya utendajikazi wa viongozi na haki yao ya kuwakosoa katika fremu kuu ya kuamrisha mema na kukataza mabaya. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, si tu kwamba raia wote wana haki, bali ni wadhifa wao kusimamia utendajikazi wa viongozi wao na kwamba, upana wa usimamizi huo haumtofautishi hata walii faqihi kama shakhsia namba moja wa mamlaka. Katika mfumo huo, wote wako sawa mbele ya sheria na wala hakuna mtu anayemzidi mwenzake kuhusiana na haki hiyo kwa kutumia nafasi aliyonayo iwe ni ya kisiasa au vinginevyo, kukwepa sheria. Mara chungu nzima, Imam Khomeini (MA) na katika maelekezo yake, alisisitiza kwamba katika mfumo wa Kiislamu, viongozi wote wanapasa kuwajibishwa kuhusiana na kazi zao, ambapo nao wananchi wana haki ya kusimamia kazi zao zote, hata kama atakuwa ni walii mtawala, na wakati wowote watawala hao wanapokosea, basi wananchi wanayo haki ya kuwakosoa na kuwalalamikia. Kuhusiana na suala la kuwakosoa watawala wa mfumo wa Kiislamu, Imam Khomeini alisema: "Kila mtu miongoni mwa wananchi, anayo haki ya kumuhoji moja kwa moja kiongozi na pia kumkosoa, na kwa hilo kiongozi huyo anatakiwa kutoa majibu ya kutosha na kinyume na hivyo iwapo kiongozi huyo alitenda kinyume na wadhifa wa Kiislamu, basi atatakiwa kuuzuliwa." Mwisho wa kunukuu. Zahifeye Nur J 2 Ukurasa wa 409.
*********
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya saba ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndugu wasikilizaji, haki ya kuunda vyama na mirengo ya kisiasa, kiraia na makundi mengine kwa ajili ya raia na pia haki ya kufanya mikusanyiko ya malalamiko, ni miongoni mwa uadilifu wa kisiasa katika jamii ambao ulihimizwa na Imam Khomeini (MA). Katika hilo, mwanzilishi huyo wa mfumo wa Kiislamu nchini Iran aliutambua umuhimu wa kuundwa vyama na mirengo ya kisiasa na kiraia, kuwa ni kulinda maslahi ya kitaifa na kuhusiana na hilo alisema: "Aina yoyote ya mikusanyiko na vyama vinavyoundwa na wananchi kwa lengo la kulinda maslahi yao, ni suala huru na Uislamu umeainisha mipaka yake." Mwisho wa kunukuu. Sahifeye Nur Juzu ya 4 Ukurasa wa 266. Imamu Khomein bila kuweka mipaka ya itikadi na kisiasa katika kuundwa vyama na mirengo, shughuli zozote za mirengo ya kisiasa aliziwekea sharti la kuwa za amani, kujiepusha na vitendo vya ukatili na utumiaji silaha, kutofungamana na ajenabi na kutodhoofisha umoja na mshikamano wa kitaifa nchini. Mtazamo huo umebainishwa vizuri katika vifungu vya 26 na 27 vya katiba ya Jamhuri ya Kiislamu. Katika uwanja huo kipengee cha 26 kinasema: "Vyama, jumuiya, taasisi za kisiasa na kimrengo pamoja na asasi za Kiislamu au za jamii ya walio wachache na zilizotambuliwa kuwa za kidini, zimewekewa sharti la kwamba zinatakiwa kutokiuka misingi ya kujitawala na uhuru, umoja wa kitaifa, mipaka ya Kiislamu na katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hakuna mtu mwenye haki ya kuzuia harakati za asasi hizo, au kuzilazimisha asasi hizo kushiriki katika shughuli yoyote ile kinyume na matakwa yao." Mwisho wa kunukuu. Kadhalika katika kipengee cha 27 cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumebainishwa kwamba: "Kuundwa mijumuiko na maandamano bila ya kubeba silaha, kwa namna ambayo haitovunja misingi ya Kiislamu, ni suala lililo huru." Mwisho wa kunukuu.
********
Kwa msingi wa fikra ya Imamu Khomeini (MA) kuhusiana na uadilifu wa kisiasa na ulioakisiwa katika misingi tofauti ya katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hii leo raia wore wa nchi hii wanayo haki ya kupiga kura na kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya nchi yao. Aidha raia wa Iran wanayo haki ya kusimamia utendajikazi wa viongozi wa serikali, kupitia magazeti, vyombo vya habari na kadhalika asasi za kiraia na za kisheria, ambazo zinatambulika kama wawakilishi wa wananchi juu ya utendaji kazi wa viongozi, ambapo katika fremu hiyo, vyombo hivyo aghlabu hukosoa kwa uhuru kamili utendajikazi wa viongozi wa serikali. Aidha nchini Iran kuna vyama na mirengo mingi ya kisiasa na kiraia ambayo inawakilisha wananchi katika kutetea kwa uhuru matakwa yao. Kwa muhtasari tunaweza kusema kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, umefanya juhudi kubwa kupitia miongozo ya Imam Khomeini (MA), kuweza kusimamisha uadilifu katika jamii, kwa lengo la kufikia matukufu na viwango stahiki.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya saba ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.