Oct 07, 2018 11:19 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (127)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala la kutunza na kufichua siri.

 

Tulisema kuwa, moja ya sifa za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo ni kutunza na kuhifadhi siri. Elimu isiyo na kikomo ya Mola Jalali imeenea na kuvizunguka vitu vyote na Mwenyezi Mungu ana habari ya kila kitu, lakini utunzaji na ufichaji siri wake hauna mithili na haiwezekani kuutolea wasifu. Mtu muumini pia ambaye ni mja wa Allah na mwakilishi wa Allah katika ardhi, anapaswa kuwa kama Muumba wake yaani awe ni mwenye kulinda na kuhifadhi siri na afunike aibu na mapungufu ya watu wengine. Kwa maana kwamba, asitoboe na kufichua siri za watu na aibu zao. Tulibainisha juu ya sisitizo la kulinda siri ni kubwa kiasi kwamba, Imam Ja'far bin Muhammad al-Swadiq as analitaja jambo hilo kuwa lina umuhimu kama damu inavyozunguka katika mishipa ya mwanadamu. Anasema kuwa:  Siri yako ni sehemu ya damu yako, hivyo basi damu hiyo haipaswi kuzunguka katika mishika isiyokuwa ya kwako. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 127 ya mfululizo huu kitazungumzia suala la kusalimia na kutoa salamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Salaam, ni jina miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu na kwa msingi huo kulitaja jina hilo ni sababu ya kupata baraka na amani. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 23 ya Surat al-Hashr:

هُوَ اللَّهُ الَّذِی لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْمَلِکُ الْقُدُّوسُ السَّلامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَیْمِنُ الْعَزِیزُ الْجَبَّارُ الْمُتَکَبِّرُ سُبْحَانَ اللَّهِ عَمَّا یُشْرِکُونَ

Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anaye fanya analo litaka, Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo mshirikisha.

Neno salaam lililokuja katika aya tuliotangulia kuisoma lina maana ya amani. Kwa msingi huo wakati waja wa Mwenyezi Mungu wanaposalimiana kimsingi wanakuwa wanapeana ujumbe wa amani. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana, kutoa salamu au kusalimia ni jambo ambalo limetiliwa mkazo mno katika Uislamu na linahesabiwa kuwa miongoni mwa haki ya Mwislamu kwa Mwislamu mwenziwe.

Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuu kutoka kwa Bwana Mtume SAW ya kwamba amesema: Mwislamu ana haki kadhaa kwa ndugu yake Mwislamu: Haki ya kwanza ni kumsalimia pindi anapokutana naye na nyingine ni kumtembelea anapokuwa mgonjwa… na kadhalika na mwisho ni kumpendelea ndugu yake Mwislamu kile anachokipenda na kutomtakia kitu ambacho yeye mwenyewe hakipendi.

Kwa hakika na kwa kuwa Uislamu unahimiza wanadamu kuishi katika mazingira ya utamaduni wa amani na salama, kwa ajili hiyo dini hii tukufu imeweka sheria ya kuanza kuamkia kwa salama: Assalaamu Alaykum. Imepokewa kutoka kwa Bwana Mtume SAW ya kwamba amesema: Hakika salamu ni jina miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi lisambazeni baina yenu. Na imepokewa kutoka kwake akisema kwamba: Mtu bakhili zaidi ni bakhili wa salam.

Kwa hakika kusalimia katika Uislamu ni jambo mustahabu, linalopendekezwa na la hiari.  Kila mtu anayeweza awe wa kwanza kumsalimia mwenzake na kuchuma thawabu zake. Hata hivyo kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu katika kusalimia ni bora na inapendeza zaidi kuzingatia nukta moja muhimu.  Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq AS anaiashiria nukta hiyo inayopaswa kuzingatiwa kwa kusema: Mdogo anapaswa kumsalimia mkubwa, mpita njia amsalimie aliyekaa na kundi dogo lilisalimie kundi kubwa la watu. Aidha anasema katika sehemu nyingine kwamba:  Aliyeko katika kipando (gari, farasi, ngamia au punda na kadhalika) amsalimie atembeaye kwa miguu na aliyesimama amsalimie aliyekaa.

 

Hadithi hii inatuonyesha kwamba, katika jambo hili la Suna la kusalimia ni vyema kuzingatia nukta hii muhimu kwani mdogo anapomsalimia mkubwa au aliyepanda kipando anapomsalimia atembeaye kwa miguu huwa ni kuonyesha heshima maalumu. Taba'an, Imam Swadiq AS yeye akifuata sira na mwenendo wa babu yake, yaani Bwana Mtume SAW daima alikuwa akiwatangulia watu wengine katika kutoa salamu. Imam Swadiq AS amenukuu kutoka kwa Bwana Mtume SAW ya kwamba amesema:  Vitu vitano sitoacha kuvifanya mpaka katikka lahadha ya mwisho ya kifo changu. Moja ya vitu hivyo ni kuwasilimia watoto.

Jambo jingine muhimu katika suala zima la kusalimia, maamkizi na kutoa salamu ni kutokuwa na ubaguzi katika kusalimia. Hususan kwa kuzingatia mali na utajiri, kwani jambo kama hili humkasirisha Mwenyezi Mungu. Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS anasema: Endapo mtu hatamsalimia Mwislamu fakiri na masikini kama anavyomsalimia mtu tajiri na mwenye mali, Mwenyezi Mungu atamghadhibikia Siku ya Kiyama.

Imam Hussein bin Ali Sayyid Shuhadaa AS anasema: Kusalimia (kutoa salamu) kuna thawabu sabini ambapo sitini na tisa kati ya thawabu hizo sabini, anapewa msalimiaji na thawabu moja anapatiwa mwitikiaji wa salamu au anayejibu salamu.

 

Miongoni mwa adabu njema za salamu ni kutoa jibu kamili zaidi la salamu au kwa uchache kujibu salamu kama ulivyosalimiwa. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 86 ya Surat an-Nisaa kwamba:

وَإِذَا حُیِّیتُم بِتَحِیَّةٍ فَحَیُّواْ بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا إِنَّ اللَّهَ کَانَ عَلَى کُلِّ شَیْءٍ حَسِیبًا

Na mnapo amkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuhisabu kila kitu. 

Makusudio ya jibu kamili la salamu ni kwamba, kama mtu atakusalimia kwa kukwambia Salaam, wewe katika kujibu sema: Waalaykum Salam, au kama atasalimia kwa kusema, Assalaam Alaykum, katika kujibu ili jibu la salamu liwe kamili useme, Waalaykum Salaam Warahmatullahi. Au kama atasalimia kwa kusema Assalaam Alaykum Warahmatullahi basi jibu linapaswa kuwa, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh, hapo jibu lako la salamu litakuwa kamili zaidi.

Tunakamilisha kipindi chetu cha wiki hii kwa kusema kuwa, licha ya kuwa kuna aya na hadithi nyingi zilizonukuliwa zinazokokoteza na kuzungumzi kuhusiana na kusalimia na kutoa salamu, lakini inasikitisha kwamba, baadhi ya watu wamekuwa wakitoa visingizio visivyo na maana na kukwepa kutekeleza suna hii ya Mwenyezi Mungu na kwa msingi huom kujinyima fadhila kubwa zinazopatikana kutokana na kusalimia.

Hii ni katika hali ambayo, Imam Hussein bin Ali Sayyid Shuhadaa AS anasema: Kusalimia (kutoa salamu) kuna thawabu sabini ambapo sitini na tisa kati ya thawabu hizo sabini, anapewa msalimiaji na thawabu moja anapatiwa mwitikiaji wa salamu au anayejibu salamu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Msisite kujiunga nami juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu.

Hadi wakati huo ninakuegeni nikikutakieni kila la kheri maishani. Wasslaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh………