Nov 27, 2018 14:58 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya nane ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa, raia wa Iran wanayo haki ya kusimamia utendajikazi wa viongozi wa serikali, kupitia magazeti, vyombo vya habari na kadhalika asasi za kiraia na za kisheria, ambazo zinatambulika kama wawakilishi wa wananchi juu ya utendaji kazi wa viongozi hao, ambapo vyombo hivyo aghlabu hukosoa kwa uhuru kamili dosari yoyote ya serikali. Katika kipindi cha leo tutazungumzia suala la uhuru wa vyombo vya mahakama hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Ndugu wasikilizaji mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kuhusu vyombo vya mahakama na usimamizi katika kutoa  hukumu wa vyombo hivyo, kimsingi umeakisiwa katika kitabu chake cha Tahrirul-Wasilah. Katika kitabu hicho, mtukufu huyo alitenga kifungu cha maudhui za hukumu katika Uislamu ambapo ndani yake alielezea kwa upana mitazamo yake kuhusiana na vyombo vya mahakama katika Uislamu. Hata hivyo hatuwezi kubainisha kikamilifu mtazamo wake wote katika kipindi hiki kama ilivyofafanuliwa katika kitabu cha Tahrirul-Wasilah. Hii ni kwa kuwa mbali na cheo cha ufahamu wa sheria za Kiislamu na umarjaa, aliwahi pia kusimamia nafasi ya hakimu wa Kiislamu kwa muda wa muongo mmoja na kutekeleza nadharia zake za kisheria ambapo katika kipindi hicho alipata kubainisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja pande tofauti kuhusiana na masuala ya mahkama. Katika kipindi hicho aliweka wazi kwa ujumla masuala mapya na ya kisasa, ijtihadi na fatwa mpya, ili yaweze kutatua matatizo yanayojitokeza kwa kuzingatia zama na nyakati. Kwa ajili hiyo, katika kufafanua mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kuhusiana na masuala ya vyombo vya mahkama, ni lazima mbali na pande za kimtazamo na kisheria, tutazame pia upande wa kivitendo na usimamizi wake katika uwanja huo. Huenda uzoefu huo wa kivitendo ukawa kama fundisho la kufahamu fatwa na mitazamo yake ya kifiqhi ambayo, mbali na ongezeko la kuinua mwelekeo wa ijtihadi wa madhehemu ya Shia, ikaandaa pia uwanja kwa ajili ya kutambua vyema mitazamo ya mtukufu huyo.

********

Msingi mkuu wa mtazamo wa Imam kuhusiana na vyombo vya mahakama na hukumu zake umejengeka juu ya maana ya 'uadilifu' ambao ndio chimbuko la mtazamo wake wa kidini. Imam Khomeini sambamba na kufafanua kifiqhi udharura wa hukumu katika utawala wa Kiislamu kupitia uadilifu, alitilia mkazo misingi kadhaa ifuatayo. Kwanza ni kwamba, hukumu ni moja ya vyeo na nafasi za kisheria na moja ya shughuli za faqihi (mtaalamu wa sheria za Kiislamu) aliyetimiza masharti. Mtukufu huyo kando na kutoa fatwa na usimamizi wa kisheria, alikutambua kutoa hukumu kuwa moja ya nguzo za utawala wa Kiislamu. Pili ni kwamba, Imam Khomeini (MA) aliutaka mfumo wa utoaji hukumu uwe kwa namna ambayo utawezesha hukumu za Mwenyezi Mungu kukita mizizi katika uga wa kijamii, sambamba na kuenezwa  na serikali hukumu za kisheria katika maisha ya wananchi. Msingi wa tatu ni kwamba, katika mfumo wa utoaji hukumu, suala ambalo Imam alilipa umuhimu ni hili kwamba, mfumo wa vyombo vya mahakama ni lazima ufanye kazi kwa namna ya kutetea haki za wananchi, kiasi kwamba, uadilifu na usalama wa vyombo hivyo uwe ni kwa maslahi ya raia hao. Mtazamo huo una kiini katika msingi wa dini ya Uislamu na madhehebu ya Shia. Hii ni kwa kuwa katika dini tukufu ya Uislamu na suna na sira ya Mtume Muhammad (saw) pamoja na Maimamu watoharifu, na katika pande zote za majaji na shughuli zao, yaani katika mazingira ya utoaji hukumu na mienendo ya majaji hao, wanapaswa kuchunga kwa makini haki ya upande wa mshtakiwa na upande wa mashtaka na masuala mengine.

*********

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya nane ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Aidha Imamu Khomeini (MA) alilitaja suala la utoaji hukumu katika Uislamu na serikali ya Kiislamu kuwa kadhia muhimu na mustakbali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kuhusiana na suala hilo mtukufu huyo alisema: "Suala la utoaji hukumu ni kadhia muhimu. Mtu ni lazima afahamu kwamba kazi yake, watu na mali na heshima zao, vyote hivyo viko chini ya usimamizi wa vyombo vya mahkama na iwapo hakimu ataenda kinyume na vile ambavyo Mwenyezi Mungu anataka, akawa hana sifa, akawa hana usahihi katika kusimamia matukufu na nafsi za watu, matokeo ya jambo hilo yanajulikana wazi..….Hii leo vyombo vya mahakama na mahakama za Mapinduzi zina jukumu zito la kulinda heshima ya Jamhuri ya Kiislamu na Uislamu na iwapo kutafanyika uzembe katika utoaji hukumu, ni wazi kuwa jambo hilo litawafanya wanachi kupoteza imani na vyombo hivyo vya mahakama, Jamhuri ya Kiislamu na viongozi wa dini." Mwisho wa kunukuu. Kwa kufahamu umuhimu huo, Imam Khomeini na bila kuchelewa, baada tu ya kupasishwa katiba na kuundwa nguzo za msingi wa serikali, aliwateua majaji sambamba na kutoa hukumu na hotuba mbalimbali juu ya nafasi ya majaji na vyombo vya mahkama na pia umuhimu wao katika nchi.

*******

Kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kutoa hukumu na kutatua mizozo kati ya wananchi Waislamu  ni kati ya nyadhifa nzito ambazo Mwenyezi Mungu alimpa Mtume Mtukufu wa Uislamu na baada ya kuaga kwake, akawaachia jukumu hilo Maimamu watoharifu katika kizazi chake (as) na baada yao, hususan katika kipindi cha ghaiba, faqii aliyekamilisha masharti. Kwa msingi huo katika kipindi hiki, ni faqihi na mujtahidi mwadilifu pekee na aliyekamisha masharti ndiye aliye na haki ya kutoa hukumu, na wala hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kusimamia suala hilo. Kwa maneno mengine ni kuwa ni haramu kwa mtu asiyekamilisha masharti kutekeleza wajibu huo. Imam Khomein alikuwa miongoni mwa wanazuoni na mafuqaha kama vile Seyyid Javad Amili, Marehemu Shaikh Kashif al-Ghitwa, na Seyyid Ali Twabatwabai na kinyume na Sheikh Answar, ambao waliamini kuwa si sharti kwa hakimu kuwa mwanaume. Katika uwanja huo Imam aliuchukulia uadilifu kuwa sharti muhimu katika utoaji hukumu sahihi katika mfumo wa Uislamu na kusema: "Iwapo mahakama zetu zitatenda kinyume na vigezo vya Uislamu na kinyume na uadilifu, basi zitachafua mfumo wetu." Mwisho wa Kunukuuu 

Ndugu wasikilizaji sehemu ya nane ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.