Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-9
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya tisa ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa, kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kutoa hukumu na kutatua mizozo kati ya wananchi Waislamu ni kati ya nyadhifa nzito ambazo Mwenyezi Mungu alimpa Mtume Mtukufu wa Uislamu na baada ya kuaga kwake, akawaachia jukumu hilo Maimamu watoharifu katika kizazi chake (as) na baada yao, hususan katika kipindi cha ghaiba, jukumu hilo likawaendea mafuqaha waliokamilisha masharti. Kwa msingi huo katika kipindi hiki, ni faqihi na mujtahidi mwadilifu pekee na aliyekamisha masharti ndiye aliye na haki ya kutoa hukumu, na wala hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kusimamia suala hilo. Imam Khomeini, alibainisha misingi ya mahkama za Kiislamu na kusisitiza kwamba, ni lazima majaji waizingatie misingi hiyo. Akibainisha wadhifa wa hakimu wa Kiislamu aliashiria nukta kadhaa ambazo zinatakiwa kuzingatiwa na majaji waadilifu katika kuzifuata na kuacha upendeleo. Miongoni mwa nukta hizo ni mtazamo chanya wa jaji (hakimu) kuhusu pande mbili zinazozozana, jaji kuwa huru katika utendajikazi wake na kutoangalia nafasi au cheo cha watu wanaliofika mbele yake katika kutatuliwa shida zao, kutomdhalilisha mtuhumiwa, kuacha kujasusi hali za watu na kutoingilia siri za mtu binafsi.
*******
Moja ya misingi muhimu iliyosisitizwa na Imam Khomeini (MA) katika shughuli za vyombo vya mahakama ni 'usawa mbele ya sheria.' Ndugu msikilizaji, msingi wa usawa mbele ya sheria ni moja ya nguzo na misingi muhimu ya kufikiwa uadilifu katika mifumo yote ya vyombo vya mahakama na ambao Imam Khomein aliusisitizia sana. Kwa mtazamo wa kisheria, usawa una maana mbili. Wa kwanza una maana ya usawa wa ubininaadamu bila kujali ubaguzi, lugha, dini, itikadi, siasa na jinsia yao, kwa kuwa wau wote wana hali na utukufu wa kibinaadamu kwa usawa na katika uga wa kisheria na kimajukumu wote wanastahiki usawa huo bila kuzingatia tofauti zao za kidhahiri. Aina ya pili ni usawa mbele ya sheria ambapo, watu na raia wote wanatakiwa kutii sheria na kuhudumiwa na sheria hiyo kwa usawa bila kufanyika ubaguzi wowote wala kutazamwa cheo na nafasi ya muhusika. Kwa hakika msingi wa usawa mbele ya sheria ni moja ya nguzo muhimu za uadilifu katika mifumo yote ya kisheria ambapo viongozi wa serikali hawapasi kujichukulia maamuzi na kubadili sheria kwa ajili ya kuwapendelea baadhi ya watu. Hivyo usawa mbele ya sheria una maana ya sheria kutekelezwa kwa usawa mbele ya watu wote.
********
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu tisa ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Sambamba na kukubali msingi wa usawa mbele ya sheria, Imam Khomeini (MA) aliutambua uhuru kuwa moja ya sifa muhimu za jaji na vyombo vya mahakama. Hii ni kwa kuwa, bila kuwepo uhuru huo, ni vigumu kufikiwa uadilifu katika jamii. Katika uwanja huo, alisema: "Vyombo vya mahakama ambavyo ni kimbilio na marejeo ya watu waliodhulumiwa, ni vyombo vilivyo huru na hakuna kiongozi aliye na haki ya kukiingilia maamuzi yake." Mwisho wa kunukuu. Aidha Imamu Khomeini alitoa ujumbe kwa majaji akisisitiza kwamba sambamba na kulindwa kujitegemea katika uhuru wao, waweze kuwatendea haki wananchi kwa mujibu wa sheria na kwamba, fedha au cheo visiwe kizuizi cha kumfanya hakimu asiwafanyie usawa watu wanaoshitakiana na kuacha kuzingatia uadilifu katika utoaji hukumu wake. Imam Khomeini alisema: "Hakimu wa Kiislamu, ambapo vyombo vya mahakama vina uhuru, ana majukumu mazito. Hakimu katika mazingira yote anapaswa kuepuka kuegemea upande wowote, ambapo kwake rais na mfanyakazi kibarua hawana tofauti yoyote. Hayo ni miongoni mwa mambo ambayo hakimu ni lazima ayazingatie." Mwisho wa kunukuu. Kwa kuzingatia kwamba inawezekana baadhi ya viongozi wa kidini katika serikali wakatumia vibaya vyeo vyao kwa maslahi yao binafsi, kuliwekwa kipengele makhsusi kinachohusiana na msingi huu wa usawa mbele ya sheria, ambapo tarehe 3/3/1358 , sawa na tarehe 24 Mei 1979, Imam alitoa amri ya kuundwa mahakama maalumu ya viongozi wa kidini kwa ajili ya kuzuia ubinafsi na utumiaji vibaya wa madaraka ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika uwanja huo, alisema: "Licha ya kwamba katika Uislamu hakuna tofauti katika kuwaadhibu wahalifu ambapo watu wote wako sawa mbele ya sheria, ni lazima wanazuoni ambao wameamua kujihusisha na vitendo vya uhalifu nao waadhibiwe." Mwisho wa kunukuu. Amri ya kuundwa mahakama maalumu kwa ajili ya viongozi wa kidini ilitolewa na Imam Khaomeini (MA) kwa ajili ya kufuatilia na kuwaadhibu baadhi ya viongozi wahalifu wa kidini walioko serikalini, katika hali ambayo kabla ya Mapindizu ya Kiislamu nchini hapa, maafisa, viongozi wa serikalini na jamaa za ukoo wa kifalme walikuwa wakipendelewa na sheria na kutofikishwa mbele ya vyombo vya mahakama hata walipofanya makosa na kukiuka sheria ya nchi.
******
Ndugu wasikilizaji uadilifu katika hukumu una maana kwamba, katika jamii mtu ambaye anavirejea vyombo vya mahaka kwa ajili ya kupata haki, anapasa kuruhusiwa na kusaidiwa kufikia lengo hilo. Kwa ibara nyingine ni kwamba, uzembeaji na utovu wa nidhamu katika vyombo vya mahakama haupasi kuruhusiwa kuwafanya watu wapoteze imani na vyonbo hivyo na kuwapelekea wasifikishe malalamiko yao huko. Mtu anapowasilisha mashitaka yale mahakamani, vikao vya kuendesha kesi yake vinapasa kuandaliwa na watu wanaofaa ili kumuwezesha muhusika apate haki yake. Katika fremu hiyo Imam Khomeini (MA) sambamba na kusisitizia juu ya udharura wa kuchungwa masuala ya kisheria katika mahakama na pia kuchungwa misingi inayohusiana na uadilifu wa mahakama, alikemea vikali ubaguzi na ghasia katika mkondo wa kutolewa hukumu mahakamani. Kwa mfano tu, akitoa radiamali kuhusiana na hatua za baadhi ya watumishi wa vyombo vya mahakama ambao kiurahisi wanaweza kuwatuhumu watu wengine kwa ufuska alisema: "Msichukulie mambo kwa pupa. Ni lazima mtende kwa mujibu wa misingi ya sheria, si kwamba kwa kuwa hivi sasa mapinduzi yamefikiwa, basi ndio tumuadhibu yeyote tunayemtaka, kumjeledi yoyote, kumfunga jela au kumnyonga mtu yeyote tunayemtaka. Suala hapa ni la heshima ya Waislamu ambayo sote tunapaswa kuilinda." Mwisho wa kunukuu.