Nov 27, 2018 15:17 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 11 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kuhusu umuhimu wa kulindwa haki za raia katika utendajikazi wa vyombo vya mahakama na pia sisitizo lake kwa majaji na mahakimu kuepuka misimamo mikali ya kufurutu ada ambayo kwa kawaida hupelekea kupotezwa haki za wanyonge. Leo pia tutaendelea kubainisha suala hilo, hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi. 
Ndugu wasikilizaji moja ya misingi mingine ya uadilifu wa kimahakama katika mtazamo wa Imamu Khomeini (MA) ni kuchunga haki za wafungwa na kutendewa miamala stahiki na iliyo bora na viongozi wa vyombo vya mahakama. Katika uwanja huo, Imam Khomeini aliwataka viongozi na askari magereza sambamba na kuchunga haki za wafungwa, wawafanyie miamala ya kiubinaadamu na Kiislamu na kujiepusha kuwatesa. Aidha Imam alitoa pendekezo la kugeuzwa jela  na kuwa mahala pa malezi ya Kiislamu kwa ajili ya wafungwa. Katika uwanja huo, aliamini kuwa jela zinapaswa kuwa shule kamili kwa ajili ya kuwafunza na kuwalea kimaadili wafungwa ili kwa njia hiyo, wakosefu wahisi ladha ya uadilifu wa Kiislamu na kuvutiwa na dini hii ya mbinguni. Imam alisema: “Ninatoa amri kwa wajumbe wote wa kamisheni na askari magereza, kuhakikisha wanaamiliana na wafungwa kwa misingi ya ubinaadamu na Uislamu sambamba na kujiepusha na maudhi dhidi yao, vitendo ambavyo vimekatazwa katika Uislamu na utawala wa kiadilifu wa Kiislamu. Bali miongoni mwa mambo ambayo yanatakiwa kuzingatiwa zaidi ni ustawi wa hali za wafungwa, sawa sawa liwe ni kundi la wafungwa walioshika silaha dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kumwaga damu za watu wasio na hatia kwa kushambulia mitaa na masoko, au wawe watu ambao wamehusika na ulanguzi na usambazaji wa madawa ya kulevya kwa raia na kusababisha uharibifu katika jamii, au aina nyingine yoyote ya wafungwa. Wote hao ni mateka wenu, hivyo wafanyieni upole na huruma kwa kuwachukulia kama ndugu.” Mwisho wa kunukuu.


**********

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 11 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mfano mwingine wa adilifu wa kimahakama katika mtazamo wa Imam Khomeini (MA) ni kukubali uwezekano wa kutazamwa upya hukumu na hakimu wa Kiislamu. Kutazamwa upya hukumu katika kufikiwa uadilifu na kuzuiwa kupotezwa haki ya mwenye haki, ni jambo lenye umuhimu mkubwa katika Uislamu. Na umuhimu huo huongezeka mara dufu wakati upande mmoja wa mashitaka ni serikali na mihimili yake ambapo kwa kutumia madaraka na ushawishi wake huweza kukandamiza haki ya raia wa kawaida katika kesi, na hivyo kufikia malengo yake kwa kukabiliwa na matatizo na vizuizi vichahce. Inafaa kuashiria kuwa, mwanzoni Imam Khomeini alikuwa amesema kwamba utazamaji upya hukumu ni jambo lisilofaa, lakini baada ya kupita muda unaokaribia miaka mitatu tangu kujiri Mapinduzi, alibaini kwamba kutokana na kuwepo matatizo mengi katika masuala ya utoaji hukumu kwa upande mmoja, na pia kuwepo majaji na mahakimu wasiokuwa mujtahid na ambao hawana weledi wa kutosha, utoaji hukumu usioweza kutazamwa upya ni jambo lisilo na maslahi kwa serikali, na kwa ajili hiyo akaruhusu kubadishwa nadharia yake hiyo, ambapo suala hilo liliingizwa katika sheria za mahakama. Katika uwanja huo iliwezekana kubadilisha mtazamo katika hukumu na kuwezekana kwa mtu kulalamikia hukumu iliyotolewa awali. Aidha kwa mujibu wa mtazamo wa Imam kuhusiana na udharura wa kulindwa haki za wananchi na raia wa kawaida, mkabala na uwezekano wa serikali na vyombo vyake vya utendaji kufanya makosa, mahakama ya uadilifu wa kiidara iliundwa. Mahakama hiyo ni moja ya matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu ambapo raia wa kawaida anaweza kuwasilisha mashtaka yake kulalamikia utekelezwaji wa sheria au maamuzi yasiyo sahihi yanayoweza kudhuru maslahi ya mtu binafsi au ya jamii kwa ujumla. Aidha mahakama hiyo inalinda haki za raia mkabala wa serikali na kushinikiza kubatilishwa baadhi ya maamuzi mabaya ya serikali.

********

Ndugu wasikilizaji kama tulivyosema katika vipindi vilivyopita,  suala zima la uadilifu wa kimahakama, yaani watu kupata haki zao na kusalimika na wale wanaopoteza haki za wadhulumiwa, ni moja ya malengo na nara muhimu zilizokuwa zikipigwa na wananchi katika kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu ambapo mwasisi wa mapinduzi hayo, Imam Khomeini (MA) alilisisitiza sana. Ni kwa msingi huo, ndipo katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kipengee kimoja kimetengwa kwa ajili tu ya vyombo vya mahakama ambapo chini ya kipengee hicho kuna vipengee vingine ambavyo vinafafanua kwa uwazi nyenzo za kuweza kufikiwa uadilifu. Mbali na hayo, kuna kipengee kingine ambacho kinabainisha haki za wananchi ambapo idara zote za serikali hususan vyombo vya mahkama, zinasisitizwa kukitekeleza. Vipengee vyote hivyo vilibuniwa kwa kwa ajili ya kuwadhaminia wananchi wa kawaida uadilifu na usalama. Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavitaja vyombo vya mahakama vya Iran kuwa nyenzo muhimu za kufikiwa uadilifu wa Kiislamu ambapo kipengee cha tatu cha katiba hiyo kunafafanua wazi kwamba moja ya nyadhifa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni kudhamini uadilifu wa kimahakama. Aidha kwa mujibu wa katiba, uadilifu ni moja ya nguzo kuu za mfumo ambapo wabunge wana jukumu la kuilinda nguzo hiyo.


********


Katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jukumu kuu la kufikiwa uadilifu na usalama wa kimahkama, limekabidhiwa vyombo vya mahakama. Kwa mujibu wa kipengee cha 156, vyombo vya mahkama ni vyenye kujitegemea ambavyo vinatakiwa kulinda haki za mtu binafsi na za kijamii ambapo ili kufikiwa lengo hilo vinawajibika kufuatilia, kuchunguza na kupeleleza mashtaka kwa makini. Aidha ili kuweza kutatua ugomvi na kumaliza mivutano  kati ya pande mbili vinatakiwa kutoa maamuzi stahiki. Moja ya daghadagha za Imamu Khomeini (MA) kwa ajili ya kufikiwa uadilifu wa kimahkama katika jamii, ilikuwa ni kuteuliwa watu wenye sifa, ujuzi na utaalamu wa kutosha kuhusu sheria za Kiislamu kwa ajili ya kusimamia masuala ya vyombo vya mahkama.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 11 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.