Dec 19, 2018 09:56 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani.

Hii ni darsa ya 804, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 12 hadi ya 15 ambazo zinasema:

بَلْ عَجِبْتَ وَيَسْخَرُونَ

Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara. 

وَإِذَا ذُكِّرُوا لَا يَذْكُرُونَ

Na wanapo kumbushwa hawakumbuki.

وَإِذَا رَأَوْا آيَةً يَسْتَسْخِرُونَ

Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara.

وَقَالُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ

 Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri. 

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa makafiri wanakanusha Kiyama. Aya tulizosoma zinamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW kuwa: wao hawakikanushi tu Kiyama lakini pia wanakifanyia stihzai na kukitumia kama wenzo wa kukufanyia wewe pia shere na kejeli. Lakini wewe, ambaye una yakini na uhakika kamili juu ya Kiyama unashangazwa na ukanushaji na ufanyaji kejeli wao kwamba inakuwaje wanakanusha bila ya hoja jambo ambalo hawana elimu wala ujuzi nalo. Basi angalau wangenyamaza kimya tu na kusema: Sisi hatujui kama Kiyama kitasimama au la? Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: sababu ya ukanushaji wao si ujinga na ujahili, ila ni inadi na ukaidi. Kwa hivyo kila linapozungumziwa jambo hilo, huwa hawako tayari kusikiliza wala kuzingatia wanayoelezwa. Lakini zaidi ya hayo, hata wanapoona muujiza sio tu hawauamini lakini wanawachochea watu wengine pia wamfanyie stihzai Mtume wa Allah na kuwahadaa watu hao kwa kuwaambia: Haya si lolote ila ni mambo yanayofanywa na wachawi. Wanadai hayo ilhali kuna tofauti ya wazi kabisa kati ya muujiza na uchawi. Mchawi na mfanya mazingaombwe ni mtu anayetumia miaka kadhaa kujifunza na kujizoeza mambo hayo, lakini Mtume wa Allah hufanya miujiza na mambo yasiyo ya kawaida bila ya kupewa mafunzo wala mazoezi yoyote yale; bali hufanya hivyo kwa irada na idhini ya Allah tu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kama moyo wa mtu hauko tayari kuikubali haki hauwezi kuathiriwa hata na maneno ya waja wateule wa Allah. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, stihzai na kejeli ni moja ya mbinu zinazotumiwa na wapinzani wa haki. Kwa hivyo watetezi na wafuasi wa haki wasihofishwe na mbinu hiyo na kuacha kuitangaza njia ya haki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba washirikina walikuwa wanakiri kuwa Qur'ani si maneno ya kawaida, lakini walichokuwa wakifanya ni kuituhumu kuwa ni sihiri na uchawi.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 16 hadi ya 18 ambazo zinasema:

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ

Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa? 

أَوَآبَاؤُنَا الْأَوَّلُونَ

Hata baba zetu wa zamani?

قُلْ نَعَمْ وَأَنتُمْ دَاخِرُونَ

Sema: Naam! Na hali nanyi ni madhalili.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kwa kusimulia mazungumzo yaliyojiri baina ya Mtume na Allah na wakanushaji wa maadi, yaani ufufuo. Katika aya hizi pia watu hao hawatoi hoja yoyote ya kupinga uwezekano wa kutokea maadi isipokuwa kuonyesha mshangao na kudai kuwa ni baidi jambo hilo kutokea. Kwa hivyo wanamuuliza Bwana Mtume katika hali ya kutoamini, kwamba itawezekana kweli watu waliokufa na viwiliwili vyao vilivyooza na kugeuka mchanga wafufuliwe na kuwa hai tena Siku ya Kiyama? Hasahasa wazee wetu waliopita ambao yameshapita makumi, bali hata mamia ya miaka tangu walipokufa kukiwa hakuna athari yao yoyote iliyobaki; kwani hata kama tutayafukua pia makaburi yao hatutaona chochote ndani yake isipokuwa udongo mtupu. Kwa kawaida masuali ya aina hii huwa yanawapitikia watu wote, lakini waumini, wao wana imani na qudra na uwezo mutlaki wa Allah SW na wanajua kwamba, Yeye Mola ni Muweza wa kuwaumba tena wafu kutokana na udongo. Wao wanasadiki habari walizopewa na Mitume na Vitabu vya mbinguni kuhusu kujiri kwa Kiyama na kufufuliwa tena viumbe wote. Lakini wale watu ambao hawamwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake ni vigumu na muhali kuamini jambo kama hilo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wakanushaji wa maadi hawana mantiki wala hoja imara za kutoa, zaidi ya kuishia kusema tu kuwa ni baidi na ni jambo lililo mbali kwa kitu hicho kutokea. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hata kama tutatupiwa masuali kwa nia mbaya na inadi lakini inapasa tuyatolee majibu wadhiha na kwa hoja zilizo wazi kabisa. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuifanyia haki inadi, ubishi na ukaidi kutamfanya mtu adhalilike huko akhera.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 19 hadi ya 21 ambazo zinasema:

فَإِنَّمَا هِيَ زَجْرَةٌ وَاحِدَةٌ فَإِذَا هُمْ يَنظُرُونَ

Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!

وَقَالُوا يَا وَيْلَنَا هَـٰذَا يَوْمُ الدِّينِ

Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo. 

هَـٰذَا يَوْمُ الْفَصْلِ الَّذِي كُنتُم بِهِ تُكَذِّبُونَ

Hii ndiyo Siku ya upambanuzi mliyo kuwa mkiikadhibisha.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kwa kuashiria qudra na uwezo wa Allah SW wa kuwafufua tena watu na kueleza kwamba: msidhani kama ilivyopangwa ni kuwa siku hiyo ya Kiyama mabilioni yote ya watu wote waliokufa katika zama zote za historia wataanza kufufuliwa mmoja mmoja au kundi moja baada ya jengine; la hasha! Ukelele mmoja tu utokao mbinguni wa kudhihirisha irada ya Allah utawafufua wafu wote kwa mpigo na kuwatoa ardhini wakiwa wanaangalia huku na kule. Ni jambo la kutarajia kwamba wakati makafiri watakapoona watu wote wamefufuliwa namna hiyo kwa wakati mmoja wataungama kile ambacho walikuwa wakikikanusha duniani na kusema: haya ndiyo tuliyokuwa tukiyakadhibisha duniani. Ole wetu sisi! Tutafanyaje leo? Tutafikwa na hali gani? Wakati watakapokiri hayo, malaika nao watalitilia mkazo hilo kwa kuwaambia, leo ni siku ya kupambanuka haki na batili na kutenganishwa waumini na wakanushaji. Ni siku ya kutenganishwa wema na wabaya na siku ya Mwenyezi Mungu kutoa hukumu baina ya waja wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kujiri kwa Kiyama na kufufuliwa viumbe ni jambo litakalotokea ghafla na kwa mpigo, si hatua kwa hatua na kwa kuchukua muda. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa washirikina watatahayari na kupigwa na bumbuwazi Siku ya Kiyama huku wakijionea kwa macho yao mwisho mbaya utakaowafika. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Siku ya Kiyama ni siku ya majuto. Kwa hivyo tujitahidini hapa duniani kuchagua na kufuata njia ambayo haitakuja kutufanya tujute Siku ya Kiyama, kwani majuto ya siku hiyo hayatatufalia kitu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 804 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atupe imani ya yakini juu ya Kiyama ya kutufanya tushikamane barabara na mema na kujiepusha kikamilifu na mabaya ili kuwa miongoni mwa watakaofuzu Siku ya Kiyama. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags