Dec 24, 2018 11:00 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 798 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 66 na 67 ambazo zinasema:

وَلَوْ نَشَاءُ لَطَمَسْنَا عَلَىٰ أَعْيُنِهِمْ فَاسْتَبَقُوا الصِّرَاطَ فَأَنَّىٰ يُبْصِرُونَ

Na lau tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje?

وَلَوْ نَشَاءُ لَمَسَخْنَاهُمْ عَلَىٰ مَكَانَتِهِمْ فَمَا اسْتَطَاعُوا مُضِيًّا وَلَا يَرْجِعُونَ

Na lau tungeli taka tunge wageuza hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia namna watu waovu watakavyohudhurishwa mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah SW Siku ya Kiyama na jinsi viungo vya miili yao vitakavyotoa ushahidi wa madhambi waliyoyafanya. Aya hizi zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Adhabu ya Mwenyezi Mungu haihusiani na Siku ya Kiyama tu; kwani anapotaka Yeye Mola, papa hapa duniani pia huwashushia adhabu waovu na wafanya madhambi, na wala Yeye si mshindwa wa hilo. Kama Allah atataka, atayawekea utando macho yao wasiwe na uwezo wa kuona. Kiasi kwamba watashindwa hata kutembea na kupita kwenye njia ileile wapitayo kila siku, seuze tena watake kuwa wa mbele wa kuwapita na kuwatangulia wengine katika kufanya hivyo. Na hiyo ni adhabu ndogo kabisa watakayopewa. Aidha kama Mola atataka, atawageuza wawe masanamu tu yasiyo na roho ambayo hayana uwezo wa kujitikisa wala kufanya harakati yoyote ile. Si kuweza kwenda mbele wala kurudi nyuma. Huenda adhabu mbili hizo zikakuwepo pia Siku ya Kiyama. Maana watu waovu, ambao wataikosa njia ya saada ya milele ya kuingia Peponi watabaki wanamangamanga na kutangatanga katika uwanja wa kuhesabiwa Siku ya Kiyama. Kwa irada ya Allah, hawatoweza kutikisika au kukimbia ili kuikwepa adhabu ambayo ni matunda ya amali zao mbaya walizofanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba hapa duniani pia, mtu hawezi kuiepuka adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo tusije tukajisahau na kughafilika na hatari ya kufikwa na adhabu au kuondokewa na neema tulizopewa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kwa hapa duniani Mwenyezi Mungu hawaonjeshi watu adhabu isipokuwa katika kesi maalumu ili wasije wakakosa fursa na haki aliyowapa ya kuchagua njia ya kufuata.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 68 ambayo inasema:

وَمَن نُّعَمِّرْهُ نُنَكِّسْهُ فِي الْخَلْقِ ۖ أَفَلَا يَعْقِلُونَ

Na tunaye mpa umri mrefu tunampindua katika umbo. Basi je! hawazingatii?

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia zilizoashiria moja ya adhabu za Allah za hapa duniani kwa kueleza kwamba: Bila shaka wanadamu wote wanapozeeka hudhoofu na kupoteza nguvu za kimwili na uwezo wa kiakili na kurejea kwenye hali ya utotoni. Hii ina maana kwamba wakati mtu anapokuwa kwenye rika la ujana na umri wa makamo, aitumie fursa hiyo kuchagua na kufuata njia sahihi ya uongofu; kwani kutumai kwamba ataweza kurejea kwenye njia ya uongofu na kuwa mtu mwema katika umri wa uzeeni, ni kujipa matarajio hewa na yasiyo na uhakika. Kwa upande mwingine mtu hatakiwi adhani pia kwamba kuwa na umri mrefu, kunamfanya awe na nguvu na uwezo zaidi. Ukweli ni kwamba wanadamu wote, hata watawala na wafalme, wanapofikia umri wa uzeeni hudhoofu na kuishiwa na nguvu wakawa mithili ya watoto wadogo wanaohitaji mtu wa kuwalisha chakula au kuwavalisha nguo. Kwa hivyo kabla hatujafikia kipindi cha uzeeni na udhaifu wa mwili na akili, tuitumie fursa tuliyonayo kwa kujitahidi kufanya mambo mema na ya kheri kadiri ya uwezo wetu ili tuwe na faida na taathira njema kwa ajili ya nafsi zetu na jamii yetu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba umri mrefu haumzidishii mtu nguvu na uwezo; ila ni kinyume chake. Kurefuka kwa umri ni kushuka kutoka kwenye kilele cha nguvu na uwezo kuelekea kwenye udhaifu na unyong’onyefu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa umri wa mtu una kikomo huku matarajio yake yakiwa mengi mno. Mtu mwenye kufuzu ni yule anayeutumia vizuri mno umri wake wenye kikomo kwa kufanya mengi ya maana na ya kheri. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kinachomuokoa mwanadamu ni kutafakari na kuitumia akili kwa njia sahihi. Lakini kila kinachomfanya aghafilike na kuutumia vizuri umri wake, ikiwemo kipindi chake cha ujana huwa sababu ya yeye kuhasirika na kuangamia.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 69 na 70 ambazo zinasema:

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ

Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha.

لِّيُنذِرَ مَن كَانَ حَيًّا وَيَحِقَّ الْقَوْلُ عَلَى الْكَافِرِينَ

Ili imwonye aliye hai, na itimie kauli juu ya makafiri.

Baada ya aya zilizozungumzia Tauhidi na Maadi, aya hizi tulizosoma hivi punde zinabainisha ukweli wa Utume kwa kueleza kwamba: yale tunayomteremshia Nabii Muhammad SAW si mashairi, wala yeye Mtume mwenyewe si mshairi. Japokuwa aya nyingi za Qur'ani, hususan sura za mwishoni za kitabu hicho kitukufu zina urari na mtiririko maalumu, lakini historia inashuhudia kuwa Bwana Mtume SAW hakuwa mshairi wala hakutunga mashairi. Tab'an kumtuhumu Bwana Mtume SAW kuwa mshairi si kwa sababu ya Qur'ani kuwa na hali ya ushairi bali kulitokana na imani potofu waliyokuwa nayo Waarabu ya kuitakidi kwamba washairi wana mawasiliano na majini na hujifunza ushairi kupitia njia hiyo. Kwa kuwa maneno ya Bwana Mtume Muhammad SAW yalikuwa kitu kipya na kisichofahamika kwao, walimtuhumu mtukufu huyo kuwa, kama walivyo washairi, naye pia anasema maneno hayo ya ajabu kwa sababu ya kuathiriwa na majini. Aya zinaendelea kubainisha kuwa: Yale yatokayo kwenye kinywa cha Mtume ni maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo ni onyo na ukumbusho kwa watu. Maonyo na indhari hizo, humlinda na hatari na madhara ya matamanio ya nafsi na ushawishi wa shetani, kila mwenye kutaka kuijua haki na ukweli. Tab'an aya hizo haziwi na taathira yoyote wanaposomewa makafiri. Na sababu yake ni kwamba hulka ya inadi na ukanushaji haki imezigubika na kuzitawala nyoyo zao utadhani mioyo yao imegeuka mawe yasiyoweza kupenya ndani yake neno lolote la haki. Pamoja na hayo, kusomewa aya hizo kunatimiza na kuondoa dhima juu yao ili Siku ya Kiyama wasije wakasema: Wito wa haki haukutufikia sisi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Qur'ani haipingi ushairi na washairi; inachopinga ni Bwana Mtume SAW kuitwa mshairi na Qur'ani yenyewe kuambiwa ni mashairi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Qur'ani si mashairi, ambayo hutungwa kupitia hisia za udhanifu za kishairi za mtu. Ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mwenye hekima yaliyosimama juu ya msingi wa hekima na mantiki. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba watu wasioikubali haki hawana tofauti na wafu. Thamani ya mtu inategemea mwamko wa moyo wake na usafi wa roho yake. Kwa hivyo watu wenye imani ya kweli nyoyo zao zihai na wanaishi maisha ya kweli; ama wale makafiri wako sawa na wafu ambao wamekosa kuishi maisha halisi. Na sababu ni kuwa ukafiri unaua moyo wa mtu. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 798 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu imani ya kuifahamu na kuifuata haki na aziepushe na giza la kufru na upotofu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags