Dec 30, 2018 11:39 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 805, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 22 na 23 ambazo zinasema:

احْشُرُوا الَّذِينَ ظَلَمُوا وَأَزْوَاجَهُمْ وَمَا كَانُوا يَعْبُدُونَ

Wakusanyeni walio dhulumu, na wenzao, na hao walio kuwa wakiwaabudu. 

مِن دُونِ اللَّـهِ فَاهْدُوهُمْ إِلَىٰ صِرَاطِ الْجَحِيمِ

Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu! 

Katika darsa iliyopita tulisema, wakati watu wa motoni watakapoiona Jahannamu watajuta kwa waliyoyafanya duniani. Wataanza kujilaumu, kujisikitikia na kupiga mayowe kwa kusema eh ole wetu sisi, tuliokuwa tukiikadhibisha siku hii! Kufuatia hayo, aya tulizosoma zinasema: Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawaamuru malaika wa Motoni kwa kuwaambia watenganisheni makafiri, madhalimu na waabudiwa wao na watu wengine kisha wao muwalekeze motoni. Ni wazi kwamba kuna aina na anuai mbalimbali za dhulma. Katika misamiati ya Qur’ani neno dhulma, mbali na maana yake ya kijamii, ambayo ni kuwadhulumu watu lina maana pia ya mtu kujidhulumu nafsi yake mwenyewe. Kumshirikisha Allah, nao pia ni mfano mmojawapo hai wa dhulma. Kuhudhurishwa na kuingizwa motoni wale na vile vilivyofanywa miungu na watu huenda kufanyika kwake kukatokana na hali mbili: Moja ni kwa sababu baadhi ya waabudiwa kama mataghuti na watawala makafiri na madhalimu ni watu ambao walikuwa wakitiiwa na kuabudiwa badala ya Allah SW. Lakini hali ya pili ni kwamba kuingizwa pamoja motoni na mtu mwenyewe waabudiwa na miungu bandia isiyo na uhai kama masanamu ya mawe na miti kutafanywa ili kumdunisha na kumdhalilisha yeye aliyekuwa akiviabudu vitu hivyo. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: watu hao wataongozwa njia kupelekwa motoni; taabiri ambayo, yenyewe ni hali fulani ya kumdhalilisha mtu dhalimu. Hii ni kuonyesha kwamba mtu ambaye duniani alikuwa na hiyari lakini hakutaka yeye mwenyewe kuifuata njia ya uongofu ya Allah, Siku ya Kiyama ataongozwa njia kwa nguvu ya kuelekezwa motoni! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama kila mtu atafufuliwa na kuwa pamoja na yule aliyekuwa akimpenda na mwenye fikra moja na yeye; kwa hivyo kama mahabubu na maabudu wake huyo litakuwa ni jiwe na mti atafufuliwa nalo pamoja pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hakuna mtu yeyote wala kitu chochote kitakachoweza kumsaidia mtu na kumwokoa na adhabu ya Moto.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 24 hadi 26 ambazo zinasema:

وَقِفُوهُمْ ۖ إِنَّهُم مَّسْئُولُونَ

Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa: 

مَا لَكُمْ لَا تَنَاصَرُونَ

Mna nini? Mbona hamsaidiani?

بَلْ هُمُ الْيَوْمَ مُسْتَسْلِمُونَ

Bali hii leo, watasalimu amri.

Katika aya zilizotangulia tumeona kuwa malaika wataamrishwa na Allah wawakusanye madhalimu na kuwapeleka motoni. Aya hizi zinasema: malaika wataambiwa, wasimamisheni kwanza madhalimu, kwa sababu kabla ya kuingizwa motoni kuna masuali ambayo wanatakiwa wayajibu; japokuwa jawabu za masuali hayo zinafahamika wazi, na wala hakuna chochote kinachoweza kufichika mbele ya Allah, hata kiweze kubainika na kudhihirika kwa majibu ya masuali hayo. Alaakulli hal faida kubwa zaidi ya kufanya hivyo ni kuwafanya waovu wakiri na kuungama wao wenyewe, ambayo pia ni hali mojawapo ya kudhalilika, na pia wajue kwamba hawakuonewa kwa adhabu watakayopewa.

Katika kuendelea kuwatupia masuali madhalimu kuhusu imani na amali zao, watu hao wataulizwa, kwa nini hamwombi msaada kwa umati mkubwa wa wenzenu na masahibu zenu mlio na fikra moja? Wakati wa matatizo duniani mlikuwa mkiwakimbilia wao kupata hifadhi, kwa nini basi hapa pia hamuwaombi wao wakusaidieni? Hapo watakiri kuwa, si wale wenye nguvu za madaraka wala wenye utajiri wa mali wanaoweza kuwasaidia wao, kwa kuwa wao wenyewe hawajijui hawajitambui; na wala si wale washirika wao na wenye hali sawa na wao wenye uwezo pia wa kuwasaidia. Kwa sababu wote hao watasalimu amri mbele ya qudra na uwezo mutlaki wa Allah SW na hawatoweza kufanya chochote mbele ya irada Yake Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama tutahojiwa na kusailiwa. Tutaulizwa kuhusu tulivyoutumia uhai na ujana wetu, fikra na imani zetu pamoja na amali na matendo yetu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mataghuti na majabari, wote watasalimu amri mbele ya amri ya Allah Siku ya Kiyama. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kinyume na duniani, waovu na wahalifu hawatoweza kusaidiana Siku ya Kiyama.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 27 hadi ya 30 ambazo zinasema:

وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ

Watakabiliana wao kwa wao kuulizana.

قَالُوا إِنَّكُمْ كُنتُمْ تَأْتُونَنَا عَنِ الْيَمِينِ

Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia. 

قَالُوا بَل لَّمْ تَكُونُوا مُؤْمِنِينَ

Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini

وَمَا كَانَ لَنَا عَلَيْكُم مِّن سُلْطَانٍ ۖ بَلْ كُنتُمْ قَوْمًا طَاغِينَ

Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu.

Aya hizi zinatoa taswira ya moja ya hali za Siku ya Kiyama, ambapo viongozi na wafuasi wa batili na upotofu watebebeshana dhima na kutupiana lawama, huku kila mmoja akimsakama mwenzake kwa masuali. Kwanza wafuasi watasema: Ni nyinyi ndio mliotufuata kwa njia ya urafiki na kama kwamba mnatutakia heri, mkatushikilia kwa viapo tufuate na kutuingiza kwenye njia hii. Laiti kama si nyinyi, leo tusingefikwa na haya. Lakini jawabu ya viongozi kwa wafuasi wao hao walioghilibiwa na kuhadaiwa ni kwamba, nyinyi wenyewe hamukuwa waumini wa haki; kwani kama si hivyo, msingewaacha Mitume na Vitabu vya mbinguni na kuja kutufuata sisi na kuyakubali maneno yetu. Kwa hivyo jilaumuni wenyewe, kwa sababu sisi hatukukuingizeni kwenye njia hii kwa nguvu na mabavu. Mlitufuata sisi kwa sababu batini zenu na hulka zenu zilikuwa za kuchupa mipaka na kuikengeuka haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama watu waovu waliokuwa wakiwafuata vinara na viranja wa shirki na ukafiri watataka kuwabebesha mizigo yao ya madhambi viongozi wa upotofu waliowafuata katika jamii ili waweze kujitoa hatiani, lakini hoja yao hiyo haitakubalika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa vinara wa ukafiri na shirki huwa wanawaghilibu na kuwapotosha watu kwa njia ya kujifanya kuwa wanawatakia mema. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba sababu za nje na za mazingira hazimtezi nguvu mtu na kumlazimisha afanye madhambi. Ni upotofu wa batini na wa ndani ya nafsi ya mtu mwenyewe pamoja na irada na hiyari yake ndivyo vinavyomfanya achanganyike na watu waasi na waovu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 805 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe washirika wema maishani ambao watakuwa sababu ya kuwa na mwisho mwema hapa duniani. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Tags