Jan 02, 2019 06:27 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 806, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 31 hadi ya 33 ambazo zinasema:

فَحَقَّ عَلَيْنَا قَوْلُ رَبِّنَا ۖ إِنَّا لَذَائِقُونَ

Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu. 

فَأَغْوَيْنَاكُمْ إِنَّا كُنَّا غَاوِينَ

Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu.

فَإِنَّهُمْ يَوْمَئِذٍ فِي الْعَذَابِ مُشْتَرِكُونَ

Basi hakika wao siku hiyo watashirikiana pamoja katika adhabu.

Katika darsa iliyopita tulisema, Siku ya Kiyama watu waliopotoshwa watataka kuwabebesha dhima ya mzigo wa madhambi yao viranja na vinara wa ukafiri na viongozi wao wa jamii waliopotoka; na watasema, wao ndio waliotupotosha sisi. Lakini viongozi wao hao watawajibu, nyinyi wenyewe mliamua kufuata upotofu, mkaridhia kutufuata sisi kwa sababu ya dhati ya batini zenu, ya uasi na kuipa mgongo haki. Na si kwamba sisi tulikulazimisheni kwa kutumia nguvu na mabavu ili mfuate upotofu. Sisi wenyewe tulikuwa tumepotoka, na nyinyi mlioamua kutufuata, tukakupotosheni pia. Baada ya maelezo hayo, aya tulizosoma zinasema: waliokuwa viongozi wa upotofu pamoja na wafuasi wao waliowafuata watafikia natija na hitimisho kwamba kuzozana na kulumbana kwao huko hakuna faida yoyote siku hiyo ya Kiyama, kwa sababu amri ya Allah kuhusu adhabu yao imeshatolewa, na muda si muda wataionja adhabu yao hiyo. Watajumuishwa pamoja katika adhabu hiyo, na makazi yao yatakuwa motoni. Tab’an ni wazi kwamba viwango na ukubwa wa adhabu zao vitatafautiana. Kila mtu ataadhibiwa kulingana na kiwango cha madhambi yake na taathira yake katika kuwapotosha wenzake; kwa hivyo adhabu watakazopewa waovu na wafanya madhambi hazitolingana. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama wafanya madhambi watakiri kuhusu ahadi ya kufikwa na adhabu ambayo Mitume waliwapa hapa duniani, lakini kukiri kwao huko hakutakuwa na faida yoyote kwao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuchanganyika na kusuhubiana na watu wapotofu kunamwandalia mazingira mtu ya kupotoka; na matokeo yake ni kwenda kuwa na makazi mamoja na watu hao huko motoni. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuwakubali watu waharibifu kuwa viongozi wa jamii na kisha kuamua kuwatii na kuwafuata hupelekea kupata nguvu madhalimu na wapotofu na matokeo yake ni watu kuchanganywa pamoja na madhalimu hao katika adhabu yao watakayopewa. Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 34 na 35 ambazo zinasema:

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَفْعَلُ بِالْمُجْرِمِينَ

Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu.

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ

Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa 'Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna. 

Aya hizi zinaashiria kaida na utaratibu wa kudumu wa Allah katika kuamiliana na waovu na wafanya madhambi na kueleza kwamba: wakati Mitume walipokuwa wakiwalingania watu Tauhidi na kumwabudu Mola pekee wa haki, baadhi yao walitakabari na hawakuwa tayari kuyasikiliza maneno yao au kutaamali na kuyatafakari waliyoambiwa. Watu hao walihitari kufuata njia ya ukafiri na shirki kutokana na inadi na ukaidi; hivyo Siku ya Kiyama watapata adhabu kali. Ukaidi na kutakabari kwao watu hao, baadhi ya wakati kulitokana na kujivuna na kujiona kwao bora kwa sababu ya mali, hadhi na vyeo walivyokuwa navyo; na wakati mwengine kulitokana na kushikilia kwao kufuata kibubusa yale yaliyokuwa yakifanywa na wazee wao waliopita au viongozi wa jamii zao, na kuzing’ang’ania kwa ukereketwa na taasubi fikra na itikadi za watu wao hao. Kwa vyovyote vile hivi ni vizuizi vikubwa kwa mtu kuwa tayari kuisikiliza na kuikubali haki. Kutakabari mbele ya haki hufikia hadi ya kumfanya mtu kwenye kiburi asiwe tu anaikana na kuikadhibisha haki lakini hata amfanyie kejeli na stihzai mwenye kuutangaza wito wa haki na kumvurumizia tuhuma na sifa mbaya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ya duniani na akhera itathibiti tu, na hilo halitoghairika katu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa chimbuko la dhambi, maasi na upotofu ni kutakabari mbele ya Tauhidi, haki na ukweli. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Mitume walikuwa wakiwalingania watu kumfuata Mola pekee wa haki na si kuwafuata wao. Katika ulinganiaji wao, wajumbe hao wa Allah hawakuwa wakitaka kunufaika wala kufaidika kwa namna yoyote ile, lakini pamoja na hayo walikuwa kila mara wakiudhiwa na kuandamwa na anuai za tuhuma za wapinzani wa haki.

Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 36 hadi 38 ambazo zinasema:

وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ

Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mshairi mwendawazimu?

بَلْ جَاءَ بِالْحَقِّ وَصَدَّقَ الْمُرْسَلِينَ

Bali huyu ameleta Haki, na amewasadikisha Mitume.

إِنَّكُمْ لَذَائِقُو الْعَذَابِ الْأَلِيمِ

Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu.

Aya hizi zinaashiria hoja za washirikina za kuhalalisha na kutetea kukataa kwao wito wa Mitume na kueleza kwamba: wao walikuwa wakiwatuhumu Mitume kwamba maneno yao ni mithili ya maneno ya washairi yanayotokana na udhanifu na hisia za moyoni na si fikra na mantiki. Isitoshe walikuwa wakidai kwamba ayasemayo Bwana Mtume SAW ni ushairi na mashairi aliyojifunza kwa majini na wala hana chochote kitokanacho na yeye mwenyewe. Simulizi za historia zinaonyesha kuwa watu wa Bara Arabu walikuwa wakiitakidi kwamba washairi walikuwa wanajifunza fani ya ushairi kupitia mawasiliano yao na majini na ni kwa njia hiyo wanaweza kutunga mashairi mazuri na ya kuvutia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na taasubi na ukereketwa juu ya fikra na itikadi potofu na za khurafa kunamzuia mtu kuikubali haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tuhuma na udunishaji ni miongoni mwa silaha zinazotumiwa na wakanushaji ili kuzuia wito wa Mitume usienee na kuwafikia watu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba mafundisho ya Mitume yalikuwa na lengo na muelekeo mmoja. Manabii wote hao wa Allah waliwalingania watu Tauhidi na kumwabudu Mola pekee wa haki. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 806 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, azitakabali dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/  

 

 

 

Tags