Jan 07, 2019 10:30 UTC
  • Sayansi na Teknolojia Mpya (25)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni Matumaini yangu kuwa utakuwa nami hadi mwisho.

Aina mpya ya mbegu za mpunga na maharagwe ambazo zinastahimili mabadiliko ya tabianchi imeanza kusambazwa ili kusaidia wakulima kupanda mazao hayo ambayo ni chakula tegemezi kwenye maeneo mbalimbali.

Shirika la Nishati ya Atomiki la Umoja wa Mataifa, IAEA, limesema hatua hiyo ilitokana na ukweli kwamba, mabadiliko ya tabianchi yanayoendana na viwango vya joto visivyotabirika, yalisababisha mavuno kupungua na wakulima kutojua la kufanya.

“Mbegu hizo mpya za mpunga pamoja na maharagwe zinahimili kiwango cha juu cha joto katika maeneo yenye ukame,” amesema María Caridad González Cepero, mwanasayansi kutoka taasisi ya kitaifa ya sayansi nchini Cuba ambaye alishiriki kwenye utafiti huo unaonufaisha wakulima kutoka nchi lukuki hivi sasa ikiwemo Cuba.

Bi. Cepero amesema mbegu mpya ya mpunga iitwayo ‘Guillemar’, ambayo inastahimili ukame imewapa manufaa makubwa wakulima nchini Cuba ambako mavuno yameongezeka kwa asilimia 10.

Taarifa ya IAEA inasema kuwa mataifa mengine kama India, Pakistan, Ufilipino, Tanzania na Senegal, nayo pia yanajiandaa kutumia mbegu mpya za mpunga zinazoendana na hali ya joto ya nchi zao.

Mradi huo wa utafiti wa miaka mitano wa kusaka mbegu mpya unahusisha wataalamu kutoka IAEA na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO.

Watafiti hao walianza kwa kutafiti ni kwa jinsi gani mpunga na maharagwe vinabadilika na kukua kwa kuzingatia mazingira ya kawaida ya tabianchi na  yasiyo ya kawaida.

Walitumia minururisho kuongeza kasi ya  kawaida ya kuongezeka kwa idadi ya mimea na hatimaye wakachagua ile inayofaa.

Kwa njia hiyo walipata aina lukuki za mazao ya mpunga na maharagwe ambayo yanaweza kuhimili viwango vya joto kupindukia na pia kuwa na mavuno mengi na mojawapo ya mbegu hiyo ni Guillemar inayotumika Cuba.

IAEA inasema kupata aina mpya za mbegu za mimea kunaweza kusaidia wakulima kupanda mazao mengi ya chakula yanayohimili mabadiliko ya tabianchi, lakini vilevile kusaidia wanasayansi kujifunza zaidi jinsi mimea inaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

@@@

Asilimia 51.2 ya watu wote duniani sawa na watu bilioni 3.9 watakuwa wanatumia mtandao wa intaneti ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2018, kwa mujibu wa makadirio mapya yaliyotolewa wiki hii na ITU ambalo ni Shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya habari na teknolojia ya mawasiliano au ICT.

Akizungumzia makadirio hayo ya upimaji wa teknolojia ya mawasiliano katika jamii, Katibu Mkuu wa ITU Houlin Zhao amesema makadirio hayo ya ITU ya kimataifa na kikanda kwa 2018 ni ishara ya mafanikio makubwa yanayofanywa na dunia kuelekea kuwa na jumuiya jumuishi ya mawasiliano kimataifa.”

Ameongeza kuwa “Ifikapo mwisho wa 2018 tutapita kiwango cha 50/50 cha matumizi ya intaneti. Na hii ni hatua kubwa ya kuwa na jumuiya jumuishi ya mawasiliano, hata hivyo bado kuna watu wengi sana duniani wanasubiri kufaidi matunda ya uchumi wa kidijitali. Ni lazima tuweke mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji na kuunga mkono teknolojia na biashara bunifu ili mapinduzi ya teknolojia yasimwache yeyote nje ya mtandao”

ITU inasema makadirio hayo yanaonyesha kwamba kunaendelea kuwa na mwenendo wa kuongezeka kwa fursa ya watu kupata na kutumia habari na mawasiliano ya teknolojia  pia fursa ya mitandao ya mawasiliano inaendelea kuongezeka hususan katika simu za mkononi au mobile. Licha ya mafanikio hayo ripoti inasema bado uwezo wa kumudu mawasiliano hayo ni mtihani ambao utaendelea kupewa kipaumbele na shirika hilo ili kuhakikisha uchumi wa kidijitali ni ndoto inayotimia kwa wote.

 Kwa mujibu wa ITU katika Mataifa yaliyoendelea ongezeko sio kubwa sana japo idadi inaendelea kupanda ya watu wanaotumia intaneti ikitoka asilimia 51.3 mwaka 2005 na kufikia asilimia 80.9 mwaka 2018. Na katika Mataifa yanayoendelea ongezeko limekuwa kubwa sana kutoka asilimia 7.7 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 45.3 mwisho wa mwaka 2018 huku ukuaji mkubwa ukiripotiwa barani Afrika  ambako asilimia ya watu wanaotumia intaneti imeongezeka kutoka asilimia 2.1 mwaka 2005 na kufikia asilimia 24.4 mwaka 2018.

Kwa mujibu wa ripota hii maeneo yaliyokuwa na ukuaji mdogo wa watumiaji wa intaneti ni Ulaya na Marekani na kwa nchi za Jumuiya ya Madola watu watakaokuwa wakitumia intaneti kufikia mwisho wa mwaka huu itakuwa ni asilimia 71.3, kwa mataifa ya nchi za Kiarabu asilimia 54.7, wakati maitaifa ya Asia itakuwa asilimia 47.

Fursa ya matumizi ya simu za mkononi au rununu kwa huduma ya kawaida ya mawasiliano inazidi kutawala, huku usajili wa matumizi ya simu za ndani ukizidi kupungua kutokana na ongezeko la asilimia 12.4 ya simu za runini kwa mwaka 2018, Na hivi sasa ITU inasema idadi ya usajili wa matumizi ya simu za rununu ni mkubwa kuliko idadi ya watu duniani.

@@@

Na mapema mwezi huu wa Disemba, mamia ya madaktari wataalamu wa moyo na upasuaji moyo kutoka Iran na nchi za Ulaya walishiriki katika Kongamano la Pili la Kimataifa la Iran na Ulaya la CTO-Capsian. Kongamano hilo lilifanyika katika Hospitali ya Razavi katika mji wa Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran. Katika kongamano hilo kulitolewa mihadhara 300 kuhusu maudhui mpya ambapo wahadhiri wa kigeni walitoa mihadhara 200 na mihadhara iliyosalia imetolewa na wataalamu Wairani. Kongamano hilo lilijikita zaidi katika kuelimisha ambapo pia wataalamu waliwafanyia upasuaji wagonjwa katika Hospitali ya Razavi. Kwa njia hiyo wataalamu bingwa wameweza kutoa mafunzo kwa wanafunzi walioshiriki katika kongamano hilo. Mkutano huo umejikita zaidi katika kutoa mafunzo ndani ya hospitali ya magonjwa ya moyo na kati ya madaktari bingwa walioshiriki walikuwemo profesa Gurlin Charlene wa Uingereza, Proges Joana Dangel wa Poland na Daktari Ibrahimu wa Marekani.

Akizungumza katika kongamano hilo Hujjatul Islam Sayyid Ibrahim Raisi mfawidhi wa Taasisi ya Haram Tukufu ya Imam Ridha AS alisema Hospitali ya Razavi ambayo inasimamiwa na taasisi hiyo inalenga kutoa huduma kwa watu wenye pato la chini katika jamii.

Naye Ridha Saidi mkuu wa Hospitali ya Razavi amesema wanajitahidi kuandaa mazingira bora ya ustawi wa kisayansi kwa kuwaleta pamoja madakatari bingwa.

@@@

Naam wapenzi wasikilizaji na kwa habari hiyo kuhusu Kongamano la Pili la Kimataifa la Iran na Ulaya la CTO-Capsian ambalo limewaleta pamoja wataalamu na wapasuaji wa moyo kutoka Iran na Ulaya ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya Sayansi na teknolojia kwa leo. Hadi wakati mwingine panapo majaliwa yake Mola, Kwaherini.