Mafanikio ya Sayansi Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
Makala hii tumekutayarishia kwa munasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 40 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Katika makala ya leo tutaangazia mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran.
TEKNOLOJIA YA SELI SHINA
Ustawi wa sayansi na teknolojia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, umeshuhudiwa katika nyuga mbali mbali na ustawi huo unaendenlea kwa kasi. Ustawi huo umekuwa mkubwa zaidi katika baadhi ya nyuga. Moja ya sekta ambazo Iran imepata ustawi mkubwa zaidi ni katika uga wa seli shina au stem cells. Mwili wa binadamu una mamia ya seli (chembechembe hai) za aina tofauti zenye umuhimu kiafya. Seli hizi zina jukumu la kuendesha mifumo mbalimbali ya miili yetu, kwa mfano, kuendesha mapigo ya moyo, kuwezesha fikra akilini, usafishaji wa damu kwenye figo, kutengeneza ngozi mpya, na kadhalika. Kazi ya kipekee ya seli shina ni kuwa chimbuko la kuzalisha aina nyingine ya seli. Seli shina pia hufanya shughuli ya ugavi wa seli mpya mwilini. Seli hizi zinapojigawanya huzidisha idadi ya seli shina nyingine au seli nyingine za kawaida. Seli shina ni muhimu kwa sababu, kwa mfano tunapoumia ama kupata maradhi, seli zetu pia huumia au kufa. Hali hii ikitokea, seli shina huanza kufanya kazi. Kwa msingi huo kadiri utafiti wa seli shina unavyozidi kuimarika, kuna uwezekano kuwa katika siku za usoni kutakuwa na uwezekano wa kutibu magonjwa sugu kama vile Saratani, Alzeima, Parkinson n.k. Nchini Iran katika muongo wa 1990, kulianza utafiti wa kina kuhusu seli shina ambapo, mwaka 1991 tulishuhudia kufunguliwa Taasisi ya Utafiti ya Royan na hivyo utafiti wa seli shina ulifuatiliwa kwa karibu. Kutokana na kufuatiliwa utafiti wa seli shina kwa kina, hivi sasa Iran inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika uga wa seli shina na katika bara la Asia inashikilia nafasi ya nne.
Hivi sasa Taasisi ya Utafiti ya Royan kwa kutumia teknolojia ya seli shina imeweza kupandikiza mboni ya jicho (cornea), kupandikiza ubongo, kupandikiza mfupa, kutengeneza seli za kutengeneza damu, kukarabati moyo n.k. Aidha Taasisi ya Royan ina benki kubwa zaidi ya damu ya vitovu. Hii ni damu ambayo hutoka katika kitovu wakati wa kuzaliwa ambayo ikihifadhiwa inaweza kutumika katika matibabu ya mwenye damu hiyo katika siku za usoni. Damu hiyo huwa na idadi kubwa ya seli shina na shina zinginezo za mfumo wa kinga mwilini na iwapo mwenye seli hizo atakumbwa na matatizo baadaye, huweza kutumika katika matibabu.

Kwa ujumla Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata mafanikio makubwa sana katia uga wa sayansi ya jenetiki na imeweza kushika nafasi ya kwanza Asia Magharibi katika uga huo. Mbali na kutibu magonjwa ya binadamu, wataalamu Wairani wameweza kutumia sayansi ya jenetiki kurekebisha na kuboresha mazao ya mimea na wanyama. Mwaka 2009 wataalamu Wairani katika Kituo cha Utafiti cha Royan mjini Esfahan, walifanikiwa kuzalisha mbuzi wa kwanza kwa njia ya Cloning katika kituo hicho.
Kuzaliwa kwa mbuzi huyo kwa njia ya cloning kunafuatia silsila ya utafiti wenye mafanikio wa wanasayansi wa Kiirani wa kituo cha Royan, na hayo ni baada ya huko nyuma, kuzaliwa kondoo kwa njia hiyo hiyo ya cloning ambaye alipewa jina la Royana. Wanasayansi Wairani waliwashangaza wengi duniani kwa uwezo wao huo ambao utawezesha kuzuia kuangamia vizazi vya wanyama wanaokabiliwa na hatari ya kuangamia.
TEKNOLOJIA YA NANO
Teknolojia ya nano pia ni uga muhimu wa sayansi katika dunia ya leo na ni nchi chache sana duniani zilizo na uwezo wa teknolojia hii muhimu. Teknolojia ya nano nchini Iran imestawi sana, na hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatambulika duniani kama miongoni mwa nchi zilizostawi sana katika uga wa teknolojia ya nano. Hivi sasa Iran ni ya nne duniani katika uga wa teknolojia ya nano ambapo hapa nchini kuna mashirika 180 yanayojihusisha na uga huu. Hivi sasa Iran kuna bidhaa mpya 420 ambazo zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya nano. Karibu asilimia 35 ya bidhaa hizo ziko katika uga wa vifaa vya maabara na viwanda na bidhaa zilizosalia ziko katika sekta za tiba, ufumaji na ujenzi. Katika ustawi huu mkubwa wa sekta ya teknolojia ya nano, si tu kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa huduma kwa Wairani bali pia sasa bidhaa za nano zilizotengenezwa hapa nchini zinauzwa katika nchi zingine 47 duniani.
Teknolojia ya nano imetoa mchango mkubwa katika utengenezaji wa vifaa vya sekta ya tiba nchini Iran. Aidha mbali na teknolojia ya nano kutumika katika utengenezaji dawa, imeweza pia kutumika katika kuhakikisha kuwa dawa zinatumia njia erevu kufika katika maeneo yanayougua mwilini na hivyo kuboresha kasi ya kupona wagonjwa.

Leo sekta ya anga za mbali na kutumia satalaiti ina umuhimu mkubwa duniani. Salataiti zina umuhimu mkubwa katika sekta za mawasiliano, utafiti, kuchunguza mali asili iliyo chini ya ardhi, utabiri wa hali ya hewa, uchoraji ramani, kutambua mahali au sehemu katika uso wa dunia (positioning satellites), kwa mfano, GPS, na hata baadhi ya nchi hutumia satalaiti kwa ajili ya ujasusi. Kumiliki satalaiti na kuwa na uwezo wa kurusha satalaiti katika anga za mbali na kuwa na kituo ardhini cha kufuatilia kazi za satalaiti ni teknolojia inayomilikiwa na nchi chache sana.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kutambua umuhimu wa satalaiti. Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza kabisa inayojulikana kwa jina la Omid (Tumaini) mwaka 2009. Kwa hatua hiyo, Iran ilijiunga rasmi na kundi la nchi chache zilizo na uwezo wa kujitengenezea na kujirushia satalaiti katika anga za mbali. Tokea wakati huo Iran imerusha satalaiti kadhaa katika anga za mbali kwa mafanikio na katika kipindi cha miaka michache ijayo itaweza kumtuma mwanadamu katika anga za mbali.
TEKNOLOJIA YA NYUKLIA
Sekta nyingine ambayo Iran imeweza kupata mafanikio makubwa ni katika teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani. Madola ya Magharibi na hasa Marekani imejaribu sana kutoa madai kuwa eti shughuli za nyuklia za Iran ni hatari na imejaribu kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu vizingiti katika uga huu. Hii ni katika hali ambayo, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umeweza kuthibitisha kuwa Iran inafuatilia shughuli zake za nyuklia kwa malengo ya amani katika sekta kama vile, kilimo, tiba, na kuzalisha umeme. Leo hii, kutokana na kupungua kwa kasi nishati ya fosili, nchi nyingi sasa zinafuatilia vyanzo vingine vya nishati na moja kati ya nishati hizo ni nishati ya nyuklia. Ni nchi chache tu duniani zinazomiliki mzunguko kamili wa kuzalisha nishati ya nyuklia. Kutokana na jitihada zisizo na kikomo za wanasayansi Wairani, mnamo Aprili 2006, Iran ilitangazwa kuwa nchi ya sita duniani yenye kumiliki mzunguko kamili wa kuzalisha nishati ya nyuklia kwa kujitegemea. Hatua hiyo iliwashangaza wanasayansi wengi duniani kwani teknolojia ya nyuklia ni ngumu sana. Wakati huo Iran iliweza kurutubisha urani kwa viwango ya asilimia 3.5 na asilimia 5 pamoja na kuwa nchi hii ilikuwa chini ya vikwazo vya nchi za Magharibi. Aidha mwaka 2010 Iran iliweza kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 20 baada ya nchi za Magharibi kuzuia Iran iuziwe urani iliyorutubishwa kwa kiwngo hicho.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulihisi hatari kubwa kutokana na ustawi huo wa Iran katika uga wa teknolojia ya nyuklia na hivyo ukapanga njama na kuwaua shahidi wanasayansi wanne wa nyuklia wa Iran. Lakini pamoja na njama hiyo ya kigaidi, Wanasayansi Wairani hawakurudi nyuma na nchi hii imekuwa ikipiga hatua katika uga wa nyuklia kila siku. Hivi sasa Iran mbali na kumiliki kituo kimoja cha kuzalisha umeme wa nyuklia cha Bushehr kusini mwa nchi, ina mpango wa kujitengenezea vituo kadhaa vya kuzalisha nishati hiyo safi.
Utengenezaji dawa za kutibu au kuzuia magonjwa mbali mbali ni moja ya kazi muhimu za teknolojia ya nyuklia. Aidha teknolojia ya nyuklia hutumika katika kuboresha ukulima wa mazao ya chakula na pia kuyatunza baada ya mavuno. Hali kadhalika teknolojia ya nyuklia inaweza kutumika kubaini iwapo kuna vyanzo vya maji chini ya ardhi, kufanya uchunguzi kuhusu uchafuzi wa mazingira, utabiri wa hali ya hewa na uchimbaji mafuta ya petroli.