Mar 30, 2019 06:45 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 825 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 20 ambayo inasema:

وَشَدَدْنَا مُلْكَهُ وَآتَيْنَاهُ الْحِكْمَةَ وَفَصْلَ الْخِطَابِ

Na tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa hikima, na kukata hukumu.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizomzungumzia Nabii Daud (as). Mtume ambaye alikuwa akikithirisha kufanya munajati na kunong'ona na Mola wake mpaka milima na ndege wakawa wanashirikiana naye katika kumsabihi Allah SW. Aya hii tuliyosoma inasema: Mbali na kumpa Nabii Daud hekima kama alivyowapa Mitume wengine wote, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimtunuku pia Mtume huyo mamlaka ya utawala na utoaji hukumu. Kwa maneno mengine ni kwamba, Nabii Daud alikuwa miongoni mwa Mitume waliochanganya pamoja Unabii na utawala. Na huu wenyewe ni ushahidi kwamba, dini na siasa vinaweza kujumuishwa pamoja; na Mitume, hawakupewa kazi ya tablighi tu ya kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu, bali kila ilipowezekana, wao wenyewe walibeba jukumu la kutekeleza sharia na hukumu za Allah katika jamii. Wao hawakuwa wakitosheka na kukaa kwenye maabadi au msikitini tu, au kutoa mawaidha ya bishara na indhari tu, lakini kila ilipolazimu, walishika hatamu za uongozi na utawala, na pia nafasi ya kadhi na hakimu wa kutoa hukumu baina ya watu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, utawala inapasa ufanye kazi kwa msingi wa hekima na uadilifu ili haki za Allah na za watu, zote mbili ziweze kuchungwa na kutekelezwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, utawala na madaraka huwa na uhalali wa kukubalika, pale unapokuwa kwenye mamlaka ya waja wema na wateule wa Mwenyezi Mungu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 21 hadi 25 ambazo zinasema:

وَهَلْ أَتَاكَ نَبَأُ الْخَصْمِ إِذْ تَسَوَّرُوا الْمِحْرَابَ

Na je! Imekufikia khabari ya wagombanao walipo pindukia ukuta kuingia kwenye mihirabu?

إِذْ دَخَلُوا عَلَىٰ دَاوُودَ فَفَزِعَ مِنْهُمْ ۖ قَالُوا لَا تَخَفْ ۖ خَصْمَانِ بَغَىٰ بَعْضُنَا عَلَىٰ بَعْضٍ فَاحْكُم بَيْنَنَا بِالْحَقِّ وَلَا تُشْطِطْ وَاهْدِنَا إِلَىٰ سَوَاءِ الصِّرَاطِ

Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Sisi ni wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoe kwenye njia iliyo sawa.

إِنَّ هَـٰذَا أَخِي لَهُ تِسْعٌ وَتِسْعُونَ نَعْجَةً وَلِيَ نَعْجَةٌ وَاحِدَةٌ فَقَالَ أَكْفِلْنِيهَا وَعَزَّنِي فِي الْخِطَابِ

Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisiini na tisa; na mimi ninaye kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo! Na amenishinda kwa maneno.

قَالَ لَقَدْ ظَلَمَكَ بِسُؤَالِ نَعْجَتِكَ إِلَىٰ نِعَاجِهِ ۖ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْخُلَطَاءِ لَيَبْغِي بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَقَلِيلٌ مَّا هُمْ ۗ وَظَنَّ دَاوُودُ أَنَّمَا فَتَنَّاهُ فَاسْتَغْفَرَ رَبَّهُ وَخَرَّ رَاكِعًا وَأَنَابَ

Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa walio amini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daudi akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba maghufira Mola wake Mlezi, na akaanguka kunyenyekea na kutubia.

فَغَفَرْنَا لَهُ ذَٰلِكَ ۖ وَإِنَّ لَهُ عِندَنَا لَزُلْفَىٰ وَحُسْنَ مَآبٍ

Basi tukamghufiria kwa hayo. Naye kwa hakika anao ukuruba na marejeo mazuri Kwetu.

Kwa mujibu wa aya iliyotangulia, Allah SW alimpa Nabii Daud (as) mamlaka ya utoaji hukumu pia baina ya watu. Aya hizi tulizosoma zinaashiria kisa cha watu wawili waliokuwa wakishtakiana, ambao walimwendea Mtume huyo na kumtaka atoe hukumu kwa uadilifu katika mzozo uliokuwepo baina yao. Tab'an utaratibu waliotumia kwenda kwa Nabii Daud haukuwa wa kawaida. Wao walikuwa wakijua kwamba, walinzi wa Mtume huyo hawatowaruhusu waende kuonana naye wakati wowote ule wanaotaka wao. Kwa hivyo wakati wa Sala na munajati, ambapo Nabii Daud alikuwa ameshughulika na ibada kwenye mihirabu yake, waliparamia ukuta wa mihirabu hiyo na kumtokezea mbele yake mtukufu huyo kwa ghafla. Jambo hilo lilimfadhaisha Nabii Daud, akadhani watu wale walikuwa na nia mbaya ya kutaka kumuua. Lakini wao wakamwambia: Ewe Daud, usihofu, sisi ni watu wawili tunaoshtakiana, tumekuja kwako ili usikilize kesi yetu kisha utuhukumu. Uingiaji wa kushtukiza wa watu wale na hali ya mfadhaiko iliyojitokeza, vilimfanya Nabii Daud asikilize maelezo ya mshtaki tu; na badala ya kutoa nafasi kwa mshtakiwa, ili naye pia atoe utetezi wake, alifanya papara ya kutoa uamuzi na kuhukumu kwamba, mshtakiwa yule alimdhulumu mwenzake kwa kutaka kitu ambacho hakikuwa haki yake. Ajabu ni kwamba yeye mtuhumiwa mwenyewe hakulalamikia hukumu ile wala hakusema chochote; na wote wawili, mdai na mdaiwa wakamuaga Nabii Daud na kwenda zao. Ilikuwa ni baada ya wawili wale kuondoka, ndipo Mtume huyo wa Allah akabaini kuwa, hakutekeleza ipasavyo utaratibu wa utoaji hukumu, kwa sababu alitoa hukumu dhidi ya mtuhumiwa kabla ya kusikiliza maelezo yake pia. Kwa hivyo alimuelekea Mola wake akatubia; na Allah SW akaipokea toba yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, inatakiwa pande mbili zenye mzozo zimtake kadhi au hakimu awahukumu kwa kuzingatia haki na uadilifu, na si kila mmoja kumshinikiza hakimu atoe hukumu kwa manufaa yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kutekelezwa uadilifu katika jamii huwa sababu ya watu kufuata njia iliyonyooka na kuwaepusha na hatari ya kufanya au kutofanya mambo kwa kufurutu mpaka na kukengeuka haki. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, mwanadamu ni mwenye pupa na mtaka makuu na katu huwa hakinai na kutosheka na mali, utajiri na raha za dunia. Na ndiyo maana kwa kawaida, watu matajiri huwa ndio wenye uchu mkubwa zaidi wa kujilimbikizia mali kuliko watu wengine. Vile vile aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, usikilizaji kesi na utoaji hukumu unahitaji kuwepo anga na mazingira tulivu. Haifai kutoa hukumu katika mazingira na hali ya wahaka na hamaniko, kwa sababu husababisha papara na babaiko katika utoaji hukumu, ambalo si hasha likasababisha majuto baadaye. Wa aidha aya hizi zinatufunza kuwa, chumo safi linapatikana kupitia imani na amali njema. Kwa hivyo kama watu katika jamii watakuwa hawamwamini Allah, yamkini wakadhulumiana katika haki zao kwa sababu ya kila mmoja kutaka ajinufaishe zaidi.  Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 825 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa waadilifu na watenda haki katika yote tunayoyatenda na kuyatolea hukumu katika maisha yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../