Mar 30, 2019 06:56 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 826 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 38 ya S’aad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 26 ambayo inasema:

يَا دَاوُودُ إِنَّا جَعَلْنَاكَ خَلِيفَةً فِي الْأَرْضِ فَاحْكُم بَيْنَ النَّاسِ بِالْحَقِّ وَلَا تَتَّبِعِ الْهَوَىٰ فَيُضِلَّكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَضِلُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا نَسُوا يَوْمَ الْحِسَابِ

Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika ardhi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanao ipotea Njia ya Mwenyezi Mungu wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, Nabii Daud (as) alitokewa na mtihani wa kuhukumu kesi ya ugomvi uliozuka baina ya ndugu wawili wanaume, ambapo baada ya kutoa hukumu hiyo ikambainikia kuwa hakufanya hivyo kwa umakini wa kutosha bali alifanya pupa katika maelezo na hukumu aliyotoa. Kwa hivyo akamuelekea Mwenyezi Mungu na kuomba maghufira. Na kutokana na moyo huo wa khushuu na unyenyekevu aliokuwa nao, Allah SW akamsamehe; na Mtume huyo mteule akabaki na daraja ileile aliyokuwa nayo mbele ya Mola wake. Aya hii tuliyosoma inasema: Ewe Daud! Sisi kukupa wewe daraja ya Utume, maana yake ni kwamba wewe ni khalifa wetu duniani, kwa hivyo mwenendo wako inapasa uendane na mafundisho yetu, na tabia na matendo yako viakisi sifa zetu. Kwa sababu hiyo, jihadhari unapohukumu baina ya watu, uhakikishe unahukumu kwa haki na uadilifu, usitekwe na matamanio ya nafsi na wala usitangulize na kufadhilisha lile ulipendalo wewe badala ya haki. Kwa sababu kufanya hivyo kutakukengeusha na njia ya Mwenyezi Mungu, ambayo ndiyo njia ya haki. Ni wazi kwamba Mitume wa Allah ni waja maasumu na hawawezi kukengeuka njia ya Allah na kufuata upotofu; kwa hivyo kutokana na aya hii tunaweza kufahamu kwamba, hadhi ya umaasumu haiwafanyi Mitume wasiwe na hiari na uhuru wa kufanya wayatakayo; kwa maana kwamba, wanao uwezo wa kufanya makosa na madhambi kama wanadamu wengine. Kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu anawapa indhari kwamba wazichunge nafsi zao, kwani yamkini badala ya njia ya Allah, wakafuata matamanio ya nafsi zao na hivyo kuwafanya wafikwe na adhabu kali ya Mola. Aya hii aidha imeendeleza maudhui ya kutoa hukumu baina ya watu iliyozungumziwa katika aya iliyotangulia. Kutokana na maelezo yake, mtu anayetawala katika uso wa dunia, inampasa azingatie na kutekeleza haki na uadilifu katika masuala yote ya jamii. Tab'an sharti la kumwezesha kufanya hivyo, ni kurejea kwenye usuli na hukumu za dini ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kuifahamu kwa usahihi haki na uadilifu na kuendesha mambo kwa mujibu wa mawili hayo na si kwa namna anavyopenda yeye na yanavyopendezwa matamanio ya nafsi yake. Kwa sababu katika hali hiyo, haki za watu zitakuwa mhanga wa matakwa ya watawala au wenye nguvu katika jamii. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, dini na siasa havitenganiki; na moja ya mambo yaliyokuwa yakiwahusu Mitume ilikuwa ni kuwaongoza watu kiutawala na kuendesha masuala ya jamii, japokuwa ni wachache tu miongoni mwa viongozi hao waliotumwa kuwaongoza wanadamu, waliokuwa katika mazingira yaliyowawezesha kuunda utawala. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, haki ndiyo inayopasa kuwa kipimo na kigezo kikuu cha sheria na hukumu za kimahakama, na si matakwa ya watawala au mahakimu. Vile vile aya hii inatufunza kwamba, kama utashi na matamanio ya nafsi ya watu ndiyo yatakayotawala,  haki itawekwa kando. Kwa sababu kufuata hawaa na matamanio ya nafsi kunaenda sambamba na kukengeuka njia ya haki. Kwa hivyo waja wateule wa Allah huwa muda wote wanadhibiti matashi ya nafsi zao ili kila wanayoyafanya katika masuala mbalimbali ya maisha yasimame juu ya msingi wa haki.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 27 na 28 ambazo zinasema:

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yao bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata.

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

Je! Tuwafanye walio amini na wakatenda mema kama wafanyao uharibifu katika ardhi? Au tuwafanye wachamngu kama waovu?

Katika aya iliyotangulia, Allah SW alimhutubu Nabii Daud (as) kwamba: Tawala na hukumu kwa haki na uadilifu, kwa sababu wewe ni khalifa wetu katika ardhi. Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Sisi tumeuumba ulimwengu kwa msingi wa haki na hakuna chochote cha batili chenye nafasi ndani yake, kwa hivyo haipasi kingine ghairi ya haki kitawale katika ardhi. Bila ya shaka kwa watu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na wenye kumkanusha Mola na tadbiri yake ya uendeshaji mambo, huwa wanadhani mfumo wa ulimwengu umeumbwa bila ya lengo wala mpangilio wowote, na wala hakuna mustakabali wowote uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu huu. Lakini watakapoingizwa motoni, ndipo itapowabainikia kwamba, dhana hiyo waliyokuwa nayo ilikuwa batili. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Si mfumo wa uumbaji tu uliosimama kwa haki, lakini hata mfumo wa adhabu na thawabu, nao pia uko juu ya haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo, Allah SW hawatazami wema na wabaya kwa jicho moja, wala haamiliani nao kwa namna moja. Ni wazi kwamba wale wanaoamini kuwa Allah ndiye Muumba na Mwenye kuwatawalia mambo yao, na wakaiamini Siku ya Kiyama, mwenendo wao katika ardhi ni tofauti na wale wanaomkanusha Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama. Kundi hilo la mwanzo hufanya juhudi na bidii za kujirekebisha wao wenyewe na kufanya yenye maslaha kwao na kwa jamii; na kundi la pili, hima yao kubwa huwa ni kufanya ufisadi na uharibifu katika ardhi. Kundi la mwanzo, mwenendo na matendo yake yanafuata misingi na miongozo iliyoainishwa na Allah kwa ajili ya wanadamu, na mwenendo wa kundi la pili, huwa wa kuzingatia manufaa ya kimaada na ya kibinafsi. Kwa hivyo matokeo ya mtazamo wa kundi la mwanzo ni kupatikana usafi na uchaMungu; na matokeo ya mtazamo wa kundi la pili ni kuenea ufisadi na uharibifu katika jamii. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika mtazamo wa dini, uumbaji una lengo maalumu na umefanywa kwa hekima. Lakini katika fikra isiyo ya dini, uumbaji haukufanyika kwa lengo lolote na wala haujatokana na mpango wowote ulioainishwa tangu kabla. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kwa vile mfumo wa ulimwengu umesimama juu ya msingi wa haki, mfumo na kanuni zinazotawala katika jamii za wanadamu inapasa zitokane na mafundisho ya haki ili ziendane na mfumo wa maumbile. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, ili haki itendeke, lazima utekelezwe uadilifu duniani na akhera. Kuwatizama kwa jicho moja wema na wabaya katika jamii hakuendani na msingi wa uadilifu. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa, kumuasi Allah na kuyaacha maamrisho yake husababisha kuenea maovu na ufisadi katika ardhi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 826 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwafikishe kusimamia haki ili uadilifu uweze kupatikana duniani. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/